Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi awaasa wanaume kuacha tabia ya kuwapa mimba wanafunzi ili watimize ndoto zao kupitia safari ya utafutaji wa elimu.
Dkt Nchimbi ametoa wito huo leo Juni 18, 2020 wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo Shule ya Sekondari New Kiomboi mjini hapa.
Akiongea na hadhira katika hafla hiyo fupi, Dkt Nchimbi amesema kuwa angependa shule hiyo ingekua na kidato cha tano kutokana na miundombinu yake kuwa mizuri.
“Ndugu zangu natamani wakati ufike sasa Wanaume muache tabia ya kuwapa mimba wasichana ili watimize ndoto zao za maisha kupitia elimu,” amesema Dkt. Nchimbi na kuongeza kuwa
“Ndugu waandishi wa habari ni wakati wenu sasa nanyi mnaweza kutengeneza Makala mbalimbali za kuwaelimisha akina baba kuacha tabia mbaya ya kuwapa wanafunzi wa kike mimba.”
Katika hadhara hiyo, Dkt. Nchimbi ameishukuru Benki ya NMB kutoa vitanda kwa ajili ya bweni la wasichana ili waweze kujisomea na kupata elimu nyakati za usiku kwa pamoja .
Halikadhalika, Dkt, Nchimbi ameiomba Benki kutoa elimu ya ujasiriamali kwa vijana wanaozunguka maeneo ya shule kutafuta wasichana badala yake wajikite na shughuli za kiuchumi.
“Tuwafundishe watoto wa kiume na wababa kuacha tabia ya kuharibu wasichana, ebu tuwakinge vijana kwa kuwapa elimu ya kuwaweka bize kimaendeleo” amesema Dkt. Nchimbi
Akiongea katika ziara hiyo Meneja wa Kanda ya Kati wa NMB, Nsolo Mlozi amesema kuwa benki ya NMB inarejesha faida kwa jamii, hivyo tumetenga kwa mwaka huu takribani bilioni mbili kwa ajili ya shughuli za maendeleo nchi nzima
“Mhe, Mkuu wa Mkoa katika wilaya ya Iramba pekee Benki ya NMB imetoa zaidi ya Tshs 29milioni kwa ajili ya shughuli za elimu na afya ili kuunga mkono juhudi za Rais wetu Dkt. John Magufuli,” amesema Mlozi na kuongeza kuwa
“Leo hii benki ya NMB imetoa vitanda ambavyo vitawasaidia wasichana katika bweni hili na hivyo kuwakinga na vijana wanaonyemelea wasichicha shuleni kuepuka mimba na kukatisha ndoto zao.”
Hata hivyo, Meneja Mlozi amesema pamoja na vitanda benki ya NMB imeweza kusaidia madawati katika shule mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Iramba.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule hiyo, Amdeus Kiduu ameishukuru Benki ya NMB kwa msaada wa vitanda katika shule hii ambapo vitasaidia wasichana wanatoka mbali na shule hii kupata malazi.
Naye Dada Mkuu wa wanafunzi katika shule hiyo, Martina John amesma kuwa msaada huo wa vitanda utawafanya waweze kusoma kwa bidii ili kukuza taaluma na kuweza kufaulu mitihani yao kwenda kidato cha tano
Pia, amesema uwepo wa bweni hilo utawapunguzia adha ya umbali mrefu, kuondoa mimba za utotoni na kuongeza muda wa kujisomea kwa pamoja, hivyo kuongeza kiwango cha ufaulu.
MWISHO
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi akikabidhiwa madawati na Meneja wa Kanda ya Kati wa NMB, Nsolo Mlozi kwa ajili ya wanafunmzi wa kike katika shule ya Sekonda New Kiomboi. Picha na Hemedi Munga
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula pamoja na wataalamu mbalimbali na wanafunzi Shule ya Sekondari New Kiomboi. Picha na Hemedi Munga
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula wakwanza kushoto akiwa pamoja na wataalamu wa Benki ya NMB katika viwanja vya Shule ya Sekondari New Kiomboi. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.