MKUU WA WILAYA IRAMBA AONGOZA KIKAO CHA TATHMINI YA MKATABA WA LISHE “JIONGEZE TUWAVUSHE SALAMA ROBO YA TATU YA MWAKA WA FEDHA 2024/2025
Iramba, Singida – Mei 20, 2025
Mkuu wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida, Suleiman Yusuph Mwenda, ameongoza kikao cha tathmini ya mkataba wa lishe wa Jiongeze Tuwavushe Salama katika ngazi ya wilaya kwa robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/2025 kuanzia Januari hadi Machi 2025. Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba.
Akizungumza katika kikao hicho, DC Mwenda amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika lishe bora kwa watoto, akieleza kuwa afya njema ya watoto ndiyo msingi wa taifa lenye watu wenye tija na uchumi imara. Ameeleza kuwa lishe bora ni msingi wa maendeleo ya mtu binafsi na ya taifa kwa ujumla.
“Tunapozungumzia lishe, tunazungumzia uwekezaji wa moja kwa moja katika rasilimali watu. Taifa letu linahitaji watu wenye afya bora ili waweze kushiriki kikamilifu katika uzalishaji na kulisaidia taifa kuepuka kuwa na wategemezi wengi,” alisema DC Mwenda.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amewakumbusha wajumbe kuwa suala la lishe ni ajenda ya kitaifa inayopewa kipaumbele na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ameeleza kuwa maagizo ya Rais kuhusu lishe yanapaswa kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa kwa kuwa na mikakati endelevu katika ngazi zote za utawala.
Kikao hicho kilihusisha maafisa kutoka idara mbalimbali, wadau wa afya na lishe, waliopo katika Wilaya ya Iramba, ambao kwa pamoja walieleza dhamira ya pamoja katika kuhakikisha lishe bora inakuwa sehemu ya ajenda ya maendeleo ya wilaya.
Mwisho wa kikao, wajumbe walikubaliana kuongeza jitihada katika kutoa elimu ya lishe kwa jamii na kufuatilia utekelezaji wa mikakati ya lishe kwa watoto na wajawazito ili kufikia malengo ya kitaifa ya kuwa na taifa lenye afya bora na uchumi imara.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.