Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula amefanya ziara katika kampuni ya SUN SHINE iliyopo kijiji cha Konkilangi kata ya Ntwike Tarafa ya Shelui kutoa elimu ya kuchukua tahadhari kujikinga na maambukizi ya virusi vya korona.
Elimu hiyo ameitoa leo Jumatatu Machi 23, 2020 alipofanya ziara hiyo akiwa na kamati ya Usalama ya Wilaya katika kampuni hiyo inayojishughulisha na uchimbaji wa madini ya dhahabu.
Mkuu wa Wilaya hiyo amewataka wafanyakazi wa kampuni hiyo kufahamu kuwa mripuko wa ugonjwa huo umekua tishio katika mataifa mbalimbali duniani hivyo kuwataka kuwa na vitakasa mikono kwa ajili ya kupaka mikononi ili kuua vijidudu vya ugonjwa huo.
Pia, amemuagiza meneja wa kampuni hiyo, ndugu Chen kuweka maji ya kuoshea mikono katika milango ya kuingilia na maeneo mbalimbali ya kampuni hiyo.
“ Ndugu zangu simamieni hayo maana afya ni zenu pia ni zetu akiumia Mtanzania hapa Serikali tunapata hasara, Mheshimiwa Rais aliporuhusu wawekezaji kama hawa tunategemea tuone faida,” amesema Luhahula na kuongeza
“ Mhakikishe mnasimamia kutimiza wajibu wenu.”
Akitaka kujua mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo, Hemedi Heri kuwa ndani ya kampuni hiyo kuna vitendea kazi kama nyundo na chepe ambavyo vinashikwa na kila mmoja kuhusu kujikinga na maambukuzi hayo watafanyaje.
Akijibu swali hilo, Mratibu wa uimarishaji ubora wa huduma za Afya Wilayani Iramba, Daniel Paul amesema kuwa vitakasa mikono vinapaswa kuwapo kila eneo kwa ajili ya kupaka kabla na baada ya kushika vifaa hivyo.
Paul amewatahadharisha wananchi hao juu ya ugonjwa wa korona unaoambukizwa kwa maji maji yanayosambaa kwa njia ya hewa kutoka kwa mtu mwenye maambukizi hayo anapokua anakohoa au kupiga chafya.
Halikadhalika, kugusa maji maji yanayotoka puani (kamasi), kugusa kitambaa au nguo na vitu vingine vilivyokua vinatumika na mtu mwenye maambukizi ya ugonjwa wa korona.
Pia, amewataka kuzijua dalili za ugonjwa huo kua ni homa na mafua makali, kuumwa na kichwa, mwili kuchoka, kikohozi, kubanwa na mbavu, maumivu ya misuli, vidonda vya koo na kupumua kwa shida, hivyo waonapo dalili hizo kutoa taarifa kupitia namba za bure za 0800110124, 0800110125 na 0800110037 na kufika katika vituo vilivyotengwa kwa wagonjwa hao ili kupata matibabu haraka.
Amewashauri wananchi hao kuzifahamu mbinu za kujikinga na ugonjwa huo kuwa ni kukaa mbali mbali angalau kwa mita mbili, kuacha kupeana mikono, kukumbatiana au kubusiana, kufunika mdomo na pua wakati wa kukohoa au kupiga chafya kwa kitambaa safi au kwa kutumia kiwiko cha mkono, kukaa mbali na mtu yoyote mwenye dalili za kifua au kikohozi na kunawa mikono mara kwa mara.
Naye katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Pius Songoma amewataka wananchi hao kufahamu kuwa serikali inapita kuhakikisha kuwa wananchi wanafuata yale ambayo Serikali inataka.
“ Mhakikishe kuwa hamgusani, hamshikani mikono, hamkumbatiani, hambusiani, pia mnakua na ndoo za kunawa maji yanayotiririka kwa sabuni pia kuwa na sanitaiza.” amesema Songoma
Mkuu wa Wilaya hiyo ameambatana na kamati ya Usalama ya Wilaya na Wataalamu wa Afya kutoa elimu ya kujikinga na ugonjwa wa Korona.
Ziara hiyo imetembelea na kutoa elimu katika kampuni ya SUN SHINE, Mgodi wa Sekenke kijiji cha Konkilangi
Kata ya Ntwike.
Pia imefika Mgodi wa Zambia uliopo kata ya Mgongo Tarafa ya Shelui.
MWISHO
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula akiwaelimisha wananchi wa Mgodini Sekenke kijiji cha Konkilangi kata ya Ntwike Tarafa ya Shelui namna ya kujikinga na ugonjwa wa Korona. Picha na Hemedi Munga
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula akiwaelimisha wananchi wa Mgodi wa Zambia kata ya Mgongo Tarafa ya Shelui namna ya kujikinga na ugonjwa wa Korona. Picha na Hemedi Munga
Mratibu wa uimarishaji ubora wa huduma za Afya wilayani Iramba, Daiel Paul akielezea dalili mbalimbali na njia za kujikinga na ugonjwa wa korona Mgodini Sekenke kijiji cha Konkilangi kata ya Ntwike Tarafa ya Shelui. Picha na Hemedi Munga
Katibu Tawala wa Wilaya ya Iramba, Pius Songoma akinawa maji yanayotiririka na sabuni wakati alipotembelea akiwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Emmanuel Luhahula pamoja na kamati ya Usalama ya Wilaya hiyo kutoa elimu ya namna ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa korona Mgodini Sekenke kijiji cha Konkilangi kata ya Ntwike Tarafa ya Shelui Wilyani Iramba. Picha na Hemedi Munga.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.