Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula amegawa ndoo za maji tiririka 150 na sabuni za maji lita 664 kwa familia 244 zenye Watoto katika kituo cha huduma ya mtoto Shiloh Student Center kwa ajili kusaidia kupambana na maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosabishwa na virusi vya corona.
Mkuu huyo wa Wilaya amegawa vifaa hivyo leo Juni 4, 2020 wakati alipokua katika kanisa la TAG Shiloh Kinampanda Wilayani Iramba.
Ameziagiza familia hizo kwenda kutumia vifaa hivyo na sio kuziweka kuwa mapambo.
“Nendeni mkatumie vizuri na msiviweke kuwa mapambo ili kuendelea kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona,” amesema Luhahula na kuongeza
“Matumizi hayo si tu yanawakinga na virusi vya corona bali yanawakinga na magonjwa yatokanayo na uchafu kama vile kipindupindu.”
Pia, amewatoa hofu Wananchi wa Kinampanda na kuwataka kuendelea kukitumia kituo cha Afya cha kinampanda kupata huduma za Afya kwa kua kipo salama.
“Ni kweli tulipendekeza Kituo cha Afya kinampanda ikiwa mgonjwa angepatikana angeletwa hapo, lakini mpaka leo tunavyoongea hakuna mgonjwa yeyote wa corona aliyeletwa kwenye kituo hicho,” ametilia mkazo Luhahula nakuongeza
“Kwa maana hiyo Iramba tuko salama hatujawahi kupata mgonjwa na si kwa ujanja wetu bali ni kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, hivyo tuendelee kumuomba Mungu na kuchukua tahadhari kama wanavyoendelea kutuambia wataalam wa Afya.”
Halikadhalika, Mkuu huyo wa Wilaya ameahidi kutoa mifuko 20 ya simenti ikiwa ni sadaka yake ya kuendeleza ujenzi wa kanisa hilo.
Mapema akiwasilisha taarifa ya kituo cha huduma ya mtoto Shiloh Student Center chenye namba ya usajili TZ152, Mchungaji wa Kanisa la TAG, Noel Lameck amesema vifaa hivyo vimegarimu zaidi ya Tsh 2.26milioni ili kuiunga mkono Serikali katika mapambano ya kudhibiti maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona.
Amesema kituo hicho kinawahudumia Watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu takribani 244 ambapo wasichana ni 128 na wavulana ni 116 ambao wanajipatia mafunzo ya elimu, kimwili, kijamii na kiroho.
Amefafanua kua kituo huwapatia vifaa vyote vinavyomsaidia mtoto mazingira ya kujifunza kama vile sare za shule, madaftari na kalamu na hugaramia matibabu pindi watoto wanapougua.
Halikadhalika, kituo kimeanzisha miradi ya ufugaji wa kuku kwa kaya 25, vikundi vya kuweka na kukopa kwa lengo la kujikwamua kiuchumi pamoja na kujenga nyumba mbili zilizokabidhiwa kwa walengwa.
Kwa upande wake mmoja wa wazazi mwenye mtoto katika kituo hicho baada ya kupokea msaada huo, Jane Timotheo amesema kuwa baadhi ya familia zilikua zinashindwa kununua ndoo, hivyo zikawa zinatengeneza vigaloni, kwa hiyo wanashukuru na wataendelea kufuata masharti kuhakikisha corona haita ingia kinampanda.
Naye mmoja wa watoto wanaopata huduma kituoni hapo, Samwel Richard amelishukuru Kanisa na kituo cha huduma cha mtoto kuwapatia ndoo na sabuni, hivyo wanaweza kunawa ili kujikinga na janga la corona.
“Msaada huo ni mkubwa maana wengine walikuwa hawana uwezo wa kununua ndoo na sabuni hivyo tunawaahidi kuwa tutavitumia vizuri ili kujikinga na corona,” amesema Richard
MWISHO
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula akiwatoa hofu wananchi na waumini wa kanisa la TAG kinampanda kuendelea kupata huduma za Afya kituo cha Afya Kinampanda kwa sababu kipo salama. Picha na Hemedi Munga
Mchungaji wa Kanisa la TAG Tarafa ya Kinampanda Wilayani Iramba, Noel Lameck akifafanua namna wanavyo iunga mkono Serikali kupambana na maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona kwa kutoa ndoo 150 na sabuni lita 664. Picha na Hemedi Munga
Afisa Tarafa wa Kinampanda Wilayani Iramba, Chotto Maingu akiongea na Waumini wa kanisa la TAG Tarafa ya Kinampanda Wilayani Iramba. Picha na Hemedi Munga
Baadhi ya ndoo na sabuni za maji zilizotolewa na kanisa la TAG Tarafa ya Kinampanda Wilayani Iramba chini ya Mchungaji Noel Lameck. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.