Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula amepiga marufuku mikusanyiko yote isiyo ya lazima ikiwa ni pamoja na mikutano ya kisiasa, warsha, makongamano, semina na mafunzo wilayani Iramba.
Luhahula ametoa katazo hilo leo Jumatano Machi 18, 2020 wakati akiongea na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama pamoja na viongozi wadini mbalimbali katika ukumbi wa Mkuu wa Wilaya mjini hapa.
Akiongea katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya amepiga marufuku vilabu vyote vinavyouza pombe za kienyeji, mabanda yote yanayoonesha video, michezo yote ya pool table na ile inayokusanya watu zaidi ya watano.
Amesema kuwa wagonjwa waliolazwa hospitali wataruhusiwa kuonwa na kuhudumiwa na ndugu mmoja tu.
Katika kujilinda na ugonjwa wa virusi vya Corona Wilayani Iramba, Taasisi zote za umma na binafsi zichukue tahadhari ambayo imeelekezwa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Ummy Mwalimu.
“ Ninaelekeza Taasisi zote, maeneo yote ya biashara na maeneo yatakayokuwa na ulazima wa kusababisha mikusanyiko ikiwa ni pamoja na migahawa, hotel, maduka daladala na vyombo vyote vya usafiri kuwa na utaratibu wa kuhakikisha wateja wao wananawa mikono kwa maji yanayotiririka huku wakitumia sabuni,” amesisitiza Mkuu wa Wilaya
Naye Mkuu wa Magereza Wilayani humo, SSP. Frank Mwakijungu amewaomba viongozi wa dini kuwafikishia taarifa wananchi kuwa hawaruhusiwi kuja Magereza kwa lengo la kuwatembelea ndugu zao.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Hussein Sepoko amewataka wananchi kufahamu dalili za ugonjwa wa Covid-19 kuwa ni homa na mafua makali, kuumwa na kichwa, mwili kuchoka, kikohozi, kubanwa na mbavu, maumivu ya misuli, vidonda vya koo na kupumua kwa shida.
Sepoko amewataka wananchi hao kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo kwa kuzingatia kanuni za Afya na usafi ikiwa ni pamoja na kukaa mbali na mtu mwenye dalili za mafua na historia ya kusafiri katika maeneo yaliokumbwa na mlipuko wa ugonjwa huo.
Halikadhalika, kufunika mdomo na pua wakati wa kukohoa kwa kitambaa safi au nguo ulioivaa sehemu za mikono, kuepuka kugusana na mgonjwa mwenye dalili za magonjwa ya njia ya hewa na kuzingatia usafi binafsi ikiwemo kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni.
Pia, kuwahi kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya endapo utakua na dalili zilizoainishwa na kutoa taarifa kwenye kituo cha kutolea huduma za Afya karibu uonapo mtu mwenye dalili za ugonjwa huo.
Halmashauri ya Wilaya ya Iramba imetenga jengo la macho liliopo hospitali ya Wilaya na kituo cha Afya Kinampanda kwa ajili ya mgonjwa yoyote atakaye kuwa na dalili za viruri vya Covid-19.
MWISHO
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.