Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula amewaomba viongozi wa madhehebu ya dini mbalimbali kutengeneza vifaa vya kunawia vinavyokanyagwa kwa mguu, ambacho ukikanyaga kwa mguu mara moja kinatoa sabuni na ukikanyaga mara nyingine kinatoa maji.
Maombi hayo yametolewa leo Ijumaa Aprili 24, 2020 na Mkuu wa Wilaya wakati akiongea na Viongozi wa Dini wa wilaya ya Iramba Mkoani Singida.
“Sisi na nyinyi ni viyoo vya jamii, hivyo niwaombe Watumishi wa Mungu kutengeneza hivi vifaa kwa kuwa mnamikusanyiko mikubwa,” amesema Luhahula
Pia, amewaomba Viongozi hao kupunguza muda wa ibada na kutoa nafasi kwa waumini wachache ili kuepukana na maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona.
Halikadhalika, amewakumbusha Viongozi hao kuwa madrasa na Sunday school zisiwepo kama alivyoelekeza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa.
Akiongea katika kikao hicho Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Daktari Hussein Sepoko amesema kuwa wameandaa sehemu ya jengo lililopo Hospitali ya Wilaya kwa wale wote watakao hisiwa kuwa na maradhi hayo na Kinampanda kwa wale watakaobainika kuwa na maradhi hayo kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Sepoko amesema kwa upande wa Doromoni kwenye Ziwa Kitangiri ambapo uvuvi wa samaki unaendelea kume kuwa na daftari la kuwasajili wote wanaoingia katika eneo hilo huku akiwataka Watendaji wa Kata na Vijiji kutoa taarifa ya mtu yoyote mwenye dalili ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona.
Pia, amesema tayari wameanza kuwapima joto abiria wote wanaoingia katika wilaya ya Iramba kwa kuweka kiziwizi eneo la Maluga.
Sepoko amesema wamekuwa wakiongeza uelewa na kutoa elimu kwa jamii kupitia vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo Standard FM, Iramba Website (www.irambadc.go.tz) na mitandao ya kijamii ya facebook (Irambadc), Instagram (Irambadckiomboi) na Twitter (Irambadc) ya Wilaya ya Iramba.
Katika kuhakikisha Wilaya inadhibiti maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona, Kamanda Mkuu wa Wilaya hiyo, P.C. Lusesa amewaomba Viongozi hao wa kiroho kuwahubiria bodaboda kuacha kubeba mshikaki.
“Sheikh Omari! ukizungumza pale Msikitini kuwa ni jambo lisilofaa, akalielewa kwa mtazamo wa kiroho anaweza asilifanye akitoka pale Msikitini,” amesema Lusesa na kuongeza
“kwa hiyo tuwaambie bodaboda hao kwa upande wa kiroho wanaweza kuelewa.”
Lusesa amewaomba Viongozi hao kuwaelimsha wananchi wao huku akiwataka kutoa taarifa kwa timu ya kufuatilia maambukizi ya virusi hivyo (Rapid Response Team).
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Usalama Barabarani, Alhaji Omari amesema kuwa tayari wametekeleza maagizo ya serikali kwa kusali huku wakiachiana nafasi kati ya mtu mmoja na mwingine na kwa muda mfupi.
Katika hatua nyingine, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya hiyo, Makwaya Charles amekiomba kikao hicho kujifunza kufanya tathimini kuhusu ugonjwa wa COVID-19.
“Tunapo kuja kwenye kikao chapili tunafanya tathimini ili kuwa na mbinu na mienendo ya kukabiliana na ugonjwa huu kulingana na wakati,” amesema Hakimu Charles
Kwa kuwa Viongozi wa Dini wanapata nafasi ya kukutana na watu, Hakimu Charles amewaomba viongozi hao kupunguza safari na mienendo ya familia kutoka kwenda kwenye mahitaji.
“Niwaombe Viongozi wa Dini kwa sababu mnapata nafasi ya kukutana na watu wenye familia, kuzielekeza familia hizo kupunguza idadi ya watu wanao safiri au kutoka kwenda kwenye mahitaji,” amesema
Pia, amewaomba Viongozi hao kuzielekeza familia kupunguza msongamano wa kutuma watoto sokoni, hivyo msongamano utapungua sokoni na namna ya kujikinga itakua nzuri.
Halikadhalika amewaomba kuwasisitiza wazazi kuwa makini na watoto wao ili kuwalinda na mimba za mapema kwa wanafunzi.
“Niwaombe Viongozi wa Kiroho kuendelea kuwasisitiza wazazi kuwa makini maana wakisahau jukumu hilo, ni kweli baada ya ugonjwa huu kuisha na shule kufunguliwa huenda tukawa na wazazi na sio wanafunzi tena,” amesisitiza Hakimu Charlrs
Pia, amewaomba Viongozi hao kuendelea kuwaelimisha watu kuwa karibu na vyombo vya habari kwa sababu vyombo hivyo vinamatangazo ya kila aina ya namna ya ugonjwa huu unavyosambaa duniani, hivyo itasaidia kama familia kujikinga na ugonjwa huo.
Naye Mchungaji Robert Kijanga wa Kanisa la Evangelist Assembies of God, ameishauri jamii kukaa katika hali ya upweke kati ya ndugu, jamaa na marafiki huku akiwataka kufahamu kuwa wamenunua kifaa cha kupima joto kwa kila muumini atakaye kuwa anaingia kanisani ili kukabiliana na maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona.
Kikao cha Viongozi wa madhehebu ya Dini mbalimbali kimefanyika leo ikiwa ni siku moja tu, Mkuu wa Wilaya alipokutana na timu ya karantini kwa ajili ya kuwatia moyo katika kupambana na kuchukua tahadhari ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona.
MWISHO
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Daktari Hussein Sepoko akitoa taarifa ya mikakati waliojiwekea kupambana na maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona. Picha na Hemedi Munga
Kamanda Mkuu wa Wilaya ya Iramba, P.C. Lusesa ameendelea kupiga marufuku bodaboda kubeba mshikaki ili kuepukana na maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona. Picha na Hemedi Munga
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Iramba, Makwaya Charles akiwaomba Viongozi wa Dini kuendelea kuwasisitiza wazazi kuwa makini na wanafunzi katika kipindi hichi waliopo nyumbani. Picha na Hemedi Munga
Viongozi wa madhehebu ya Dini mbalimbali wakisikiliza taarifa ya namna ya kuchukua tahadhari ya kupambana na maambukizi ya homa kali inayosababishwa na virusi vya corona. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.