By Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula amezindua kampeni ya Jiongeze! Tuwavushe Salama mama wajawazito.
Luhahula amezindua kampeni hiyo kiwilaya leo Ijumaa Novemba 29, 2019 katika ukumbumbi Mkubwa wa Halmashauri hiyo wakati akiongea na watumishi wa kada mbalimbali.
Mkuu wa Wilaya hiyo amewabaiinishia watumishi hao kuwa kampeni hiyo ni ajenda ya kitaifa kuhakikisha tunawalinda na kumpunguza vifo vya mama mjamzito vinavyotokana na uzazi na vifo vya watoto wachanga.
“ Lengo letu kubwa ni kuwajibika, kila mmoja atimize wajibu wake’’ amesisitiza Luhahula
Kuhakikisha kampeni hiyo inafanikiwa kwa ufanisi, Mkuu wa Wilaya hiyo amesaini mkataba na watendaji wa vijiji ili wakasimamie kuhakikisha vifo vinavyotokana na uzembe kwa wakina mama na watoto wachanga visiwepo.
Aidha amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Linno Mwageni kuwapeleka wataalamu katika kila kata kutoa elimu kwa watendaji hao ili kuifahamu kampeni hiyo vizuri.
Mapema akiongea katika uzinduzi huo Mganga Mfawidhi Hospitali ya Wilaya ya Iramba, Abel Mafuru amesema lengo la tamko la kiapo ni kuongeza kasi ya uwajibikaji kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga nchi nzima kwa kutekeleza mambo muhimu tisa.
Mafuru ameyataja mambo hayo tisa ambapo lakwanza ni upatikanaji wa huduma rafiki kwa vijana na huduma za afya ya uzazi, pili ni wajawazito kuanza kliniki mapema, kukamilisha mahudhurio mane au zaidi ya kliniki kipindi cha ujauzito na baada ya kujifungua ili kupata elimu, usahuri nasaha, vipimo na matibabu stahiki.
Huku akilitaja jambo latatu kuwa ni kupatikana huduma za dharura kwa matatizo yatokanayo na uzazi vituo vyote vya kutolea huduma ya uzalishaji, nne kupatikana muda wote damu salama na yakutosha inapohitajika, tano kuishirikisha jamii katika maswala ya Afya ya uzazi na mtoto, sita kutambuwa na kujadili taarifa ya kila kifo kitokanacho na uzazi na kifo cha mtoto mchanga ili kujua sababu ya kifo, hatu na mikakati ya kuzuwia kutokea kingine iwekwe, saba upatikanaji wa huduma kwa watoto wachanga waliozaliwa kwa uzito pungufu (njiti) na ambao ni wagonjwa, nane kupatikana huduma ya rufaa muda wote pale mama mjamzito na mtoto mchanga wanapohitaji na mwisho kuimarisha na kuboresha mifumo ya utoaji wa taarifa kwa njia mbalimbali.
Hata hivyo Mafuru amewakumbusha wananchi na wadau wa Afya ya uzazi na mtoto kuwa kila mmoja kwa nafasi yake anawajibika kuimarisha afya ya mama na mtoto mchanga mahali alipo kwa kuwatambuwa wajawazito wote waliopo katika maeneo yao kuwasaidia waweze kuhudhuria kliniki ya ujauzito na kuzingatia ushauri wanaopewa.
Huku akiwataka watalaamu wa Afya kufanya uchunguzi yakinifu ili kubaini mapema dalili zozote za hatari na kuchukuwa hatuwa stahiki kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya chanjo, ubora wa matibabu ya utotoni, ushauri kuhusu lishe, kuimarisha mfumo wa rufaa na upatikaniji wa huduma bora kwa akina mama wajawazito, kujifunguwa na baada ya kujifunguwa.
Mafuru amesisitiza ushiriki kamilifu wa wanaume katika suala zima la afya ya uzazi na mtoto huku akiwaomba viongonzi wa dini, wanasiasa na jamii kuifahamu elimu hii ili waweze kuwa sehemu ya suluhisho.
Kwa upande wake Afisa Lishe wa Wilaya hiyo, Monica Sarwat amewaeleza wananchi na wadau wa Afya ya uzazi na mtoto suala la kuboresha lishe na kupunguza athari za utapiamlo katika jamii huku akiitaka jamii kupitia uongozi wa kijiji kushiriki ipasavyo kupanga, kutekeleza na kufuatilia maendeleo ya utekelezaji wa mpango na afua ya lishe.
Sarwat amewaeleza wadau kuwa kijiji au mtaa kinawajibu kuhakikisha kuwa lishe ni ajenda ya kudumu katika vikao vya kisheria vya kamati ya halmashauri ya kijiji au mtaa, kuchochea na kiubua fursa za lishe, matatizo na suluhu za kutatua matatizo ya lishe yaliopo katika jamii, kuhakikisha vipaumbele vinajumuisha afua za chakula na lishe, afya, usafi, maji safi, mazingira safi na uchangamshaji wa watoto.
Pia kukusanya, kutathimini na kujadili taarifa za lishe kutoka kwenye kaya na maeneo mengine ya kijiji au mtaa na kufanya ufuatiliaji wa shughuli za lishe na kutoa taarifa.
Kampeni ya “Jiongeze ! Tuwavushe Salama” ilizinduliwa kitaifa na serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na wadau wa Afya ya uzazi na mtoto Novemba 06, 2018 Jijini Dodoma.
Katika uzinduzi huo wa kitaifa Wakuu wa Mikoa walisaini Tamko la Ahadi mbele ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Wakati kimkoa uzinduzi huo ulifanyika Novemba 21 chini ya Dkt, Rehema Nchimbi, Mkuu wa Mkoa wa Singida na kufuatiwa na Tamko la Ahadi kwa wakuu wa wilaya wa Mkoa huo.
Afisa Lishe wa Wilaya ya Iramba, Monica Sarwat amewaeleza wananchi na wadau wa Afya ya uzazi na mtoto Mbele ya Mkuu wa Wilaya hiyo suala la kuboresha lishe na kupunguza athari za utapiamlo katika jamii huku akiitaka jamii kupitia uongozi wa kijiji kushiriki ipasavyo kupanga, kutekeleza na kufuatilia maendeleo ya utekelezaji wa mpango na afua ya lishe. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.