Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula amewaagiza viongozi wa AMCOS kuwa waadilifu na kutoa elimu kwa wakulima wa mazao ya choroko, dengu, mbaazi, soya na ufuta kuhusu mfumo wa stakabadhi ghalani Wilayani Iramba.
Luhahula ametoa maagizo hayo kwa AMCOS leo Jumatano Aprili 29, 2020 wakati akizindua mfumo wa stakabadhi ghalani Wilayani Iramba.
Amewataka viongozi hao kutochezea mizani ya kupimia mazao hayo na kuhakikisha wanakua waadilifu katika kutekeleza mfumo huu.
“Niwaombe viongozi wote wa ngazi ya Halmashauri na wale mnaosimamia Ushirika kuwa makini ili tusiwapoteze Wakulima na matokeo yake wakawa wakiitukana Serikali,” amesema Luhahula
Halikadhalika, amewataka viongozi hao kuhakikisha wanasimamia Ushirika vizuri ili Halmashauri isipoteze mapato yake.
Mfumo wa Stakabadhi Ghalani kwa mazao ya dengu, choroko na mengineo yanayotokana na maagizo ya Serikali kuhusu mfumo wa ununuzi wa mazao hayo kwa Mikoa inayolima mazao hayo kuanzia mwaka 2020.
Akisoma tangazo kwa umma lililotangazwa na gazeti la Habari Leo la Februari 20, 2020, Mrajisi Msaidizi Mkoa wa Singida, Thomasi Nyamba amesema kuwa Serikali inataka mazao yanayozalishwa na Mkulima kuuzwa kupitia Mfumo wa Ushirika kwa lengo la kuhakikisha mazao ya jamii ya mikunde na mbegu kama vile choroko, dengu, mbaazi, soya na ufuta yanazalishwa na kuuzwa kwa tija na ubora unaotakiwa ili kumuwezesha Mkulima wa mazao hayo kupata soko la uhakika na lenye bei ya ushindani.
Kufuatia tangazo hilo, Nyamba ameufahamisha umma na wadau wote wa mazao hayo nchini kwamba kuanzia mwaka 2020 yatazalishwa na kuuzwa kupitia Mfumo wa Ushirika.
Pia, kutokana na mamlaka ya Wizara ya Kilimo na kwa kuzingatia sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 6 ya mwaka 2013 imetoa maelekezo 17 Wakulima na Wanunuzi wa mazao hayo kuyazingatia.
Akichangia mada katika kikao cha uzinduzi wa Mfumo wa Stakabadhi Ghalani, Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wa Wilaya hiyo, Ibrahimu Mjanaheri amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Linno Mwageni, kutengeneza programu maalumu ambayo haitachukua wiki moja kuanzia sasa itakayomuwezesha Afisa Ushirika kupita kwa viongozi wa vijiji na vitongoji ambao watafikisha elimu ya mfumo wa Stakabadhi Ghalani kwa wananchi wao.
“Halmashauri imuwezeshe Afisa Ushirika Wilaya kwenda kukutana na hao watu, maana mpango huu utatupa matokeo makubwa sana,” ameagiza Mjanaheri
“Ninaomba tuwekeze Ndago, Shelui na Kidaru ambapo tunaweza kupata mazao mengi maana tutapata fedha nyingi sana kwenye kilimo,” amesema
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Simion Tyosela amewataka viongozi hao wa AMCOS kuanza Ushirika mpya.
“Tuhakikishe tunauboresha Ushirika ambao utaleta tija katika maisha yetu, Ushirika ni Maisha,” amesema Tyosela
“Embu tuupeleke Ushirika huu, maana tukifanya vizuri mtaona namna ambavyo watu watamiminika, hivyo Ushirika kuwa na tija na kufanya maendeleo makubwa ikiwemo kuongeza mapato ya Halmashauri yetu,” ameongeza Tyosela
Katika kuhakikisha viongozi wa AMCOS wanaelewa malengo ya Serikali kwa Wakulima wa mazao hayo mada mbalimbali zimewasilishwa.
Naye Mkuu wa Idara ya Kilimo Umwagiliaji na Ushirika wa Wilaya hiyo, Marietha Kasongo amesema kuwa mfumo utakua na vituo vya kukusanyia mazao ambavyo vitakua katika AMCOS za Umoja-Mtoa, Jembe nimali-Ndago, Nsimbo AMCOS-Urughu, Malendi AMCOS-Mgongo, Lunsanga AMCOS-Mtekente, Ngusamu AMCOS-Ntwike na Maluga AMCOS-Maluga.
Amefafanua kuwa vituo vya masoko vinatarajiwa kuwa viwili ambapo ni Ghala la Nselembwe kata ya Shelui, Mtoa, Mgongo na Ntwike huku kijiji cha nguvumali kikihudumia kata ya Mukulu, Mtekente, Mbelekese, Kaselya, Maluga, Ulemo na Kyengege.
Kasongo amewataka Wakulima kufahamu kuwa wanatakiwa kuuzia mazao yao katika vituo vya ununuzi wa mazao.
Amesema Wafanya biashara watatakiwa kuomba kibali cha ununuzi wa mazao kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ambapo Mkurugenzi Mtendaji atampatia mnunuzi kituo cha kwenda kununua mazao au zao analolitaka.
Pia, Kasongo amewaonya wakulima wa mazao hayo kuwa hawaruhusiwi kuuza mazao yakiwa shambani au nyumbani, hivyo faini kubwa itatolewa kwa mnunuzi na Mkulima anayeuza mazao bila kutumia kituo maalumu.
MWISHO
Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Iramba, Ibrahimu Mjanaheri amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Linno Mwageni kumuwezesha Afisa Ushirika wa Wilaya hiyo kwenda kutoa elimu ya mfumo wa stakabadhi ghalani kwa mazao ya choroko, dengu, mbaazi, soya na ufuta kwa wananchi vijijini. Picha na Hemedi Munga
Mkuu wa Idara ya Kilimo Umwagiliaji na Ushirika wa Wilaya ya Iramba, Marietha Kasongo akiwaonya wakulima wa mazao ya choroko, dengu, mbaazi, soya na ufuta kuwa hawaruhusiwi kuuza mazao yakiwa shambani au nyumbani, hivyo faini kubwa itatolewa kwa mnunuzi na Mkulima anayeuza mazao bila kutumia kituo maalumu. Picha na Hemedi Munga
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Simion Tyosela akiwataka viongozi wa AMCOS kuanza Ushirika mpya utakaokua na tija na kuifanya Halmashauri hiyo ikusanye mapato yake. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.