Mkuu wa wilaya ya Iramba Mhe.suleiman Mwenda amehadhimisho siku ya ukimwi duniani katika kijiji cha ujungu, leo tarehe 1 Desemba, 2021 akiongea na Wananchi Mhe, Mwenda amewashukuru viongozi na wananchi wa Wilaya ya Iramba kwa kubeba jukumu la kuwa mwenyeji wa Maadhimisho haya ya Siku ya UKIMWI Duniani kwa Mwaka huu wa 2021 “nitoe shukrani za pekee kwa Viongozi, Wadau na wananchi wote wa Wilaya ya Iramba kwa kukubali kubeba jukumu la kuwa mwenyeji wa Maadhimisho haya ya Siku ya UKIMWI Duniani kwa Mwaka huu wa 2021, yanayofanyika Kiwilaya hapa Ujungu. Napenda pia kuwashukuru nyote kwa kunipa heshima ya kuwa Mgeni Rasmi katika maadhimisho haya. Ahsanteni sana.
Aidha, niwapongeze vikundi vyote kwa burudani mbalimbali na ushuhuda kutoka kwa watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI. Nimefarijika na yote niliyoyaona na kusikia.
Umoja wa Mataifa uliamua siku ya tarehe 01 Desemba ya kila mwaka kuwa siku ya Kimataifa ya Maadhimisho ya UKIMWI Duniani. Lengo la Maadhimisho haya ni kupima na kutathmini kiasi cha utekelezaji wa malengo na maazimio mbalimbali kuhusu Mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI. Aidha, siku hii hutumika kwa malengo MATATU yafuatayo:-
Kuhamasisha na kuelimisha jamii juu ya namna ya kujikinga na maambukizi mapya ya VVU,
Matumizi sahihi ya dawa za ARV kwa watu wanaoishi na VVU pamoja na
Kupinga unyanyapaa na ubaguzi.
Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani kwa mwaka huu wa 2021 ni “ZINGATIA USAWA. TOKOMEZA UKIMWI.TOKOMEZA MAGONJWA YA MLIPUKO” Kaulimbiu hii inasisitiza ushiriki na ushirikishaji wa Kimataifa, Kitaifa na Jamii katika shughuli za udhibiti wa VVU na UKIMWI kuanzia kwenye upangaji mikakati, upatikanaji wa rasilimali na utoaji wa huduma za VVU na UKIMWI kwa makundi yote ya wanaume, wanawake, vijana walio katika umri wa balehe wenye umri wa miaka 15-24, akinamama wajawazito na wanaonyonyesha pamoja na watoto wao katika kuzingatia upimaji wa afya zao.
Wakati Dunia ikiadhimisha Siku hii ya UKIMWI ambayo leo ni Miaka 42 iliyopita tangu ugundulike rasmi duniani, kila mmoja wetu akumbuke kwamba VVU na UKIMWI bado upo, na achukue hatua za makusudi ya kupambana na janga hili, kwa kuwa hakuna dawa ya kuponya UKIMWI pia hakuna CHANJO. Hivyo kila moja wetu achukue tahadhari ili kupunguza maambukizi mapya
Katika wilaya yetu maambukizi ya VVU na UKIMWI bado yapo, hii ni kutokana na uwepo wa shughuli nyingi za mwingiliano wa kiuchumi kwa mfano uwepo wa machimbo ya madini, maeneo ya uvuvi, vituo vya magari makubwa n.k.Niwaombe viongozi wa kata zote kuweka Mikakati mahususi ya kudhibiti maambukizi mapya ya VVU.
Kushamiri wa maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI miongoni mwa Wanaume, Wanawake na Vijana wenye umri kati ya miaka 15 – 49 ni mkubwa. Kwa mwaka 2021 yaani kuanzia (Januari – Oktoba) Waliopimwa ni watu 49,229 Wanaume 16,378 na wanawake 32,851 kati yao 814 waliogundulika kuwa na maambukizi ya VVU sawa na asilimia 1.6 wanaume walikuwa 300 sawa na asilimia 0.6 Na Wanawake walikuwa ni 514 sawa na asilimia 1.0.
Kwa upande wa vijana kuanzia miaka 15-24 kwa kipindi cha Januari hadi Oktoba, 2021 waliopimwa 20,296 wanaume 7,349 na wanawake 12,947waliogudulika kuwa na maambukizi mapya VVU ni 151 sawa na asilimia 0.7 kati yao wanaume 35 na wanawake 116. Katika suala zima la upimaji wa hiari, idadi kubwa ya wanaopima ni wanawake ukilinganisha na wanaume. Kama takwimu zinavyoonyesha hapo juu.
Kwenye Huduma ya Matunzo na Tiba, jumla ya watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI walioandikishwa hadi kufikia Oktoba 2021 ni 11,342 ambapo kati ya hawa waliopo kwenye dawa ni 5,338 na waliobaki wamehama na wengine ni watoro. Hali hii si ishara nzuri katika mapambano dhidi ya UKIMWI, kwa sababu hiyo, naomba sana wataalam wa afya waendelee kutoa elimu ya ufuasi mzuri wa dawa.
Kama sehemu ya Mapambano hayo WAVIU pia hupima wingi wa Virusi, kwa hiyo, hadi Oktoba, 2021 Jumla ya WAVIU 3,062 wamepata huduma ya kupima wingi wa Virus vya UKIMWI na kati yao 2,935 sawa na asilimia 96 wamepata ufubavu wa VVU. Hii ni ishara nzuri kwani inaonyesha kuwa afya zao zinaendelea vizuri. Niwasihi sana WAVIU wasibweteke na kufubazwa kwa VVU na kuanza mienendo isiyofaa hivyo ni lazima tuendelee kufuata maelekezo ya wataalam ili kulinda afya zetu
Vijana ni kundi linalokabiliwa sana na changamoto ya maambukizi mapya ya VVU nchini. Takwimu za maambukizi mapya ya VVU zinaonesha kwamba asilimia 40 ya maambukizi hutokea kwa vijana na katika hao asilimia 80 ni vijana wa kike.
Kwa mujibu wa takwimu hizi, ni dhahiri kuwa kundi la vijana na hasa wa kike lipo kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi mapya. Uchambuzi wa kimazingira kuhusu takwimu hizi unaonesha kuwa sababu za vijana kuwa katika hatari ya maambukizi mapya ya VVU ni pamoja na:
Hizo ni baadhi ya sababu au vichocheo vya kuongezeka kwa maambukizo mapya ya VVU miongoni mwa vijana. Aidha, natoa wito kwa vijana wajitambue na kuthamini maisha yao kwa kujikinga na maambukizi mapya ya VVU kwa kuwa ninyi ni nguvu kazi na Taifa linawategemea. Na wale wanaoishi na VVU waendelee kutumia dawa za ARV kwa ufuasi sahihi bila kuacha ili kufubaza VVU na kuimarisha afya zao.
Katika juhudi za Mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, Mkoa ulizindua Kampeni ya “FURAHA YANGU” mwaka 2018. Lengo la uzinduzi
wa kampeni hii ambayo kauli mbiu yake ilikuwa ni ‘PIMA, JITAMBUE, ISHI’ ni kuona wananchi wa Mkoa wa Singida wanatambua hali zao za maambukizi ya VVU, hususani wanaume na makundi mengine ambayo ni Wasichana walio katika umri wa balehe, Wanawake vijana wenye umri wa miaka 15-24, akinamama wajawazito na wanaonyonyesha pamoja na watoto wao.
Wilaya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali waliopo ndani na nje ilifanya mapitio ya Mpango Mkakati wa UKIMWI wa mwaka 2015 hadi 2020. Lengo la mkakati huu ni kupunguza na kuondoa viashiria vinavyosababisha maambukizi ya VVU Maambukizi ya VVU.
Pamoja na mafanikio makubwa tuliyoyapata, bado kuna mambo mengi yanayohitaji kufanyika ili tuweze kufikia adhima yetu ya kumaliza kabisa janga la UKIMWI. Hii ni pamoja na kuzuia maambukizi mapya sambamba na kuzuia vifo vinavyotokana na UKIMWI na hatimaye tuanze kuona gharama za kudhibiti VVU na UKIMWI nchini zikipungua.
Wilaya yetu imefanikiwa kufikia malengo ya 95 TATU (95:95:95) hasa katika 95 ya pili na ya tatu. Kwa kujikumbusha tu ni kwamba
95% ya kwanza inalenga kuhakikisha kuwa asilimia 95 ya WAVIU wanajua hali zao;
95% ya Pili wanaojua hali zao wanaanza kutumia dawa za kufubaza makali ya VVU mapema na
95% ya Tatu walioanza dawa za kufubaza VVU kinga zao za mwili zinaimarika.
Natoa wito kwa wadau wote katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, tuongeze jitihada sana katika kuhamasisha upimaji wa VVU ili tufikie lengo katika 95 ya kwanza. Vilevile, tuendelee kujitathmini katika maeneo yote matatu ili palipo na changamoto tuweze kurekebisha na kuimarisha na penye mafanikio tuongeze nguvu zaidi. Aidha mipango yetu ya baadaye ionyeshe wazi jinsi tutakavyofikia Tanzania isiyokuwa na maambukizi mapya UKIMWI ifikapo mwaka 2030.
Sote tunafahamu kwamba unyanyapaa umekuwa ni kikwazo kikubwa katika kutekeleza mipango tuliyojiwekea wenyewe katika kutokomeza UKIMWI. Serikali kwa upande wake, imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya kampeni za kuelimisha kuhusu madhara ya unyanyapaa na ubaguzi kupitia vyombo vya habari na majukwaa mbalimbali. Hata sasa kuna kampeni zinaendelea kupitia wasanii, mitandao ya kijamii pamoja na hotuba za viongozi. Huo ni mtizamo potofu na unahitaji kukomeshwa.
Nawasihi Watanzania wenzangu, tuache kabisa tabia za unyanyapaa na ubaguzi. Elimu iendelee kutolewa kwa njia mbalimbali kuanzia ngazi ya familia ili watu wajue ukweli kuhusu VVU/UKIMWI pamoja na kujua jinsi ya kuwahudumia watu wanaoishi na VVU ili kuondoa mtazamo hasi.
Aidha,Niwasihi Viongozi wa Dini, Wanasiasa na Viongozi wa Serikali katika ngazi zote, endeleeni kusemea na kukemea unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya WAVIU na kuhimiza upendo na huruma miongoni mwao.
Katika kufikia mafanikio hayo niliyokwisha yataja, hatukuwa peke yetu. Wapo wadau mbalimbali ambao wamekuwa bega kwa bega na Serikali katika kuhakikisha tunashinda vita hivi dhidi ya VVU na UKIMWI. Hivyo basi, nitumie fursa hii kutoa shukrani za dhati kwao
Napenda kuhitimisha kwa kuwakumbusha kwamba UKIMWI bado ni Janga la Taifa na Kimataifa na la KIDUNIA, hivyo ni vyema kila mmoja kuwa na wajibu wa kuchukua tahadhari stahiki na kuendeleza mapambano dhidi ya Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI. Sambamba na hilo niendelee kuwakumbusha wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya UVIKO 19 na kwenda kupata chanjo dhidi ya UVIKO 19 katika vituo vya Afya
Mwisho ninawashukuru tena kwa maandalizi mazuri na ushirikiano wenu mlionesha katika maadhimisho haya. Ninaomba Mungu aendelee kutulinda. “ZINGATIA USAWA. TOKOMEZA UKIMWI.TOKOMEZA MAGONJWA YA MLIPUKO”
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.