Mkuu wa wilaya ya Iramba mkoani Mhe. Emmanuel Luhahula akikabidhiwa miche ya miti 3000 ya aina mbalimbali kwa ajili ya kuboresha mazingira katika shule ya sekondari Kizaga na shule za msingi kutoka shirika la NDUGU Foundation.
Mkuu wa wilaya ya Iramba Mhe. Emmanuel Luhahula akikabidhiwa vitabu vya ziada na kiada 547 kwa ajili ya shule ya sekondari kizaga kutoka shirika la NDUGU Foundation.
Mkuu wa wilaya ya Iramba mkoani Singida Mhe. Emmanuel Luhahula, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba na Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye picha ya pamoja na wanafunzi wa shule ya sekondari Kizaga
SHIRIKA lisilo la Kiserikali linalojishughulisha na shughuli za kijamii, Ndugu Foundation lenye makao yake Makuu nchini Sweeden limetoa msaada ya vitabu vya ziada na kiada zaidi ya 3000 kwa ajili ya Shule ya Sekondari Kizaga Wilayani Iramba ,Mkoa wa Singida.
Kitengo cha mawasiliano wilayani Iramba kimeshuhudia hafla fupi juzi iliyofanyika kwenye ukumbi shule ya Sekondari Kizaga ya kukabidhi vitabu 547 vya Sekondari kwa Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mhe: Emmanuel Luhahula lengo likiwa kuwasaidia watoto wa shule hiyo kitaaluma na kuongeza ufaulu.
Akipokea msaada huo Mhe: Luhahula alimshukuru Mratibu Mkuu wa Shirika la Ndugu Foundation Winjuka Mkumbo ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kizaga ambapo Mkuu huyo wa Wilaya alimsifu kwa kujali nyumbani alikozaliwa kwani ni watu wachache wenye moyo wa kusaidia wakiwa nje ya nchi kukumbuka nyumbani na kutoa msaada kama huu.
Pamoja na kutoa msaada wa vitabu pia shirika hilo limetoa msaada wa miche ya miti mbalimbali 3000 kwa ajili ya kumuunga mkono Makamu wa Rais Mhe: Samia suluhu Hassan kutunza na kuhifadhi mazingira nchini.
Pamoja na shukrani zake Mkuu huyo wa Wilaya alitoa wito kwa wazazi wote kuhakikisha watoto wote waliofaulu kwenda Sekondari wanaenda shule kwa tarehe iliyopangwa bila kisingizio chochote.
‘’ Natoa wito kwa wananchi wote , watendaji wa vijiji na kata wenyeviti wa vitongoji na vijiji kuhakisha ifikapo Januari 31 mwaka huu watoto wote waliofaulu kuingia kidato cha kwanza wawe wameripoti shuleni na ikifika Februari Mosi mwaka huu operesheni ya kuwakamata wazazi ambao hawajawapeleka watoto wao shule, kwa kipindi hiki watoto wanaweza kuripoti shule bila sare za shule wakati wazazi wakijiandaa kushona sare ’’alisisitiza Mhe Luhahula.
Hata hivyo aliwapongeza watendaji wa kata ya Ulemo kwa kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Serikali kwa kuandikisha darasa la awali kwa asilimias 117 na darasa la kwanza asilimia 102.
Kwa upande wake Mratibu Mkuu wa Shirika la Ndugu Foundation Winjuka Mkumbo alisema Shirika hilo limeanza kazi ya kushughulikia jamii tangu mwaka 2002 ambapo shirika hilo linajishughulisha na Afya , Elimu, Mazingira na Ustawi wa jamii.
‘’ Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya , leo hii Shirika la Ndugu Foundation linakabidhi vitabu vya ziada na kiada 547 kwa ajili ya shule hii na miche ya miti mbalimbali 3000 kwa ajili ya uhifadhi na utunzaji mazingira ambapo Shule sita za Msingi za kata ya ulemo na shule ya Sekondari Kizaga zitahusika na upandaji wa miti ili kuboresha mazingira ya kata yetu lakini ukijumlisha msaasda wa vitabu tangu tuanze tumeshasaidia zaidi ya vitabu 3000 vya ziada na kiada’’ alisema Mratibu Mkumbo
Mratibu huyo alisema toka shirika hilo lianze mwaka 2002 tayari limejenga nyumba ya mganga ya moja kwa mbili kwa ajili ya Zahanati ya Misigiri, limetoa vifaa tiba kwa ajili ya zahanati hiyo.
‘’ Pamoja na shughuli nyingine za kijamii pia tumesaidia chakula magunia 120 ya mahindi kwa ajili ya chakula kwa shule 10 za Msingi na 2 za Sekondari za Mukulu na Kizaga, lakini pia shirika letu linatoa Elimu ya Wajasiriamali , na utoaji Elimu ya Ukimwi kwa jamii na uhifadhi wa mazingira’’
Shirika la Ndugu Foundation lilianzishwa na Amon Gyunda ambaye ni mzaliwa wa kijiji cha Kizaga Wilayani Iramba anayeishi Sweden na Mwenyekiti wa Shirika hilo ni Martin Gastered ambaye pia mkazi wa nchini Sweden
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.