Na Hemedi Munga
tehama@irambadc.go.tz
Singida - Iramba. MKUU wa wilaya ya Iramba mkoani Singida, Suleiman Mwenda amefanikisha askari 85 wajeshi la akiba waliohitimu mafunzo yao kupata ajira SUMAJKT.
Mwenda ameeleza hayo leo Jumatatu Novemba 15, 2021 wakati akifunga mafunzo ya askari wa jeshi la akiba katika viwanja vya shule ya msingi kata ya Ulemo wilayani hapa.
“Vijana hawa ni jeshi kamili, leo hii tukipata uvamizi wa aina yoyote katika wilaya yetu ya Iramba ninajivunia kwamba ninacho kikosi kamili cha kukituma kwenda kumsambatisha adui na adui akasambaratika.” Alisema DC Mwenda na kuongeza kuwa
“ Vijana hawa ni hazina kwa Taifa, kwa sababu wamejaa uzalendo, ukomavu , ujasiri, uhodari, na utaifa katika mioyo yao ya kulilinda na kulitetea Taifa lao.”
Hakika vijana hawa ni rasilimali na mtaji mkubwa kwa nchi ya Tanzania.
“Niwaambie ndugu zangu kwa kutambua umuhimu wa vijana hawa sikutaka wapotee tena kurudi mitaani, nimeshirikiana na msimamzi wa Jeshi la akiba kuhakikisha vijana hawa wanapata ajira, hivi ninavyoongea vijana hawa 85 wamepata ajira katika Shirika la SUMAJKT.” Alisema
Kupata ajira kwa askari hao kumetoa fundisho kwa vijana na wazazi kuhimiza vijana wao kujiunga na mafunzo ya jeshi la akiba pale mafunzo yanapokuwa yameitishwa kwa sababu mafunzo hayo ni sehemu ya kuwaandaa vijana kupata ajira na kuwa raia bora wa Taifa la Tanzania.
Katika hatua nyingine Mwenda amempongeza Diwani wa kata ya Ulemo wilayani hapo, John Peter ambaye ameshiriki na kuhitimu mafunzo hayo.
“Kwa kweli ni vijana wachache ambao ni viongozi wanatambua umuhimu wa mafunzo haya ambayo yanamfanya mtu anakuwa kiongozi mahiri, mwenye nidhamu na alioshiba utaifa.” Aliongeza
Aidha amefafanua kuwa, kufuatia serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuipatia Iramba takribani 1.3 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 47 na mengine ya shule shikizi.
“Vijana hawa wameshiriki ujenzi wa kuchimba msingi ya madarasa 15 nakufanikwa kuokoa takribani 900,000, hivyo natowa wito kwa wananchi kujifunza kwa vijana hawa kujitolea kuchimba misingi, kupeleka mchanga na kupeleka mawe ili kuhakikisha madarasa yanajengwa kwa kiwango bora na yanakamilika kwa wakati.” Alisema
Akitoa taarifa fupi ya askari hao mbele ya Mkuu huyo wa wilaya, Kapteni Eusebius Mtesigwa amesema kuwa vijana hao wako tayari wakati wote kulilinda na kulitumikia Taifa hili.
Kapteni Mtesigwa alifafanuwa kuwa askari (wanafunzi) hao wanaotimu wako 132 ambapo askari wa kike 14, askari wa kiume 118 huku askari wawili kutohitimu baada ya kukosa vigezo.
Askari hao wamefundishwa mafunzo ya kijeshi, mafunzo ya TAKUKURU, mafunzo ya Zimamoto, mafunzo ya usalama wa raia, mafunzo ya uhamiji, mafunzo ya huduma ya kwanza, mafunzo ya usomaji wa ramani, mafunzo ya ujanja wa porini na mafunzo kutoka jeshi la uhifadhi (TFS).
“Niwaombe askari mnaohitimu mafunzo kuzingatia kiapo chenu cha utii katika utendaji wenu wa kazi hasa utii, uaminifu na uhodari ili kuwa mabalozi wazuri wa jeshi la akiba na usalama.” Alisema Mtesigwa
Awali akisoma risala ya wahitimu hao, MGM Betha Japhect amemshukuru Mkuu huyo wa wilaya kwa kuwahakikishia kupata ajira, hivyo wamemuahidi kuwa watiifu, waaminifu na waadilifu kwa Taifa lao.
“Tutakuwa waadilifu, wazalendo,kufanya kazi kwa kushirikiana na kujiepusha na maadili yasiokuwa ya mtanzania.” Aliahidi
Kwa upande wake Diwani wa kata hiyo, ambaye ni mhitimu wa mafunzo hayo, John Peter amesema kuwa mafunzo hayo yameleta hamasa kubwa kwa vijana hasa baada ya zawadi mbalimbali alizozitoa Mkuu huyo wa Wilaya pamoja na ajira ya askari waliohitimu.
Akiongea na Mwandishi wetu mmoja wa wazazi wa wahitimu hao, Matha Peter amesema kuwa wako tayari kuwahimiza watoto wao kushiriki mafunzo ya jeshi la akiba kwa sababu wanapa ajira na kuwa raia wema.
“Kwa kweli tumefurahiswa sana kwa watoto wetu kupata ajira kwani tumepunguza wazururaji mitaani, Pongezi ziende kwa Mkuu wa Wilaya kwa kuungana na SUMAJKT kuwapatia vijana wetu ajira.” Alisema
MWISHO
Mkuu wa wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda akikaguwa paredi ya askari 132 wa jeshi la akiba ambao wamehitimu mafunzo yao Novemba 15, 2021 katika viwanja vya Shule ya Msingi Ulemo Wilayani Iramba mkoa wa Singida. Picha na Hemedi Munga
Mkuu wa wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda akiwa na kamati ya ulinzi na usalama wakitoa heshima kwa askari wa jeshi la akiba waliokuwa wakipita mbele yao kwa mwendo wa pole pole na wambio. Picha na Hemedi Munga
Baadhi ya askari wa jeshi la akiba wakiwa paredi wakati Mkuu wa wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda akikaguwa paredi hiyo. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.