Na Hemedi Munga
Singida - Iramba. MKUU wa wilaya ya Iramba mkoani Singida, Suleiman Mwenda ameiagiza Kamati ya Maendeleo ya Kijiji cha Ndulungu kukubaliana kimaandishi kuomba kijiji hicho kuwa kata au kuiomba TAMISEMI kubadilisha matumizi ya Tsh 250 milioni zije kijiji cha Ndulungu na Tsh 355 milioni zipelekwe kijiji cha Mwandugyembe.
Mwenda ametoa agizo hilo leo Ijumaa Januari 14, 2022 wakati alipokutana na wananchi wa kijiji cha Ndulungu wilayani hapa baada ya kudaiwa kuibuka mgogoro wa wananchi wa kijiji cha Ndulungu kutokubaliana na ujenzi wa kituo cha Afya kijiji cha Mwandugyembe katika kata hiyo.
Akiongea na wananchi hao, Mwenda amewataka kuwa na subira kipindi ambacho amewapa nafasi ya kuandika muhtasari wa kubadilisha matumizi ya fedha ambazo wameletewa kwa ajili ya kutengenza barabara kijijini hapo.
“Ndugu za kuna njia mbili ya kutatua mgogoro huu ambapo moja ni kuiandikia TAMISEMI kuwaomba kufuata ushauri wa wananchi wakubadilisha matumizi ya Tsh 355 za kutengeneza barabara katika kijiji cha Ndulungu zipelekwe kijiji cha Mwandugyembe huku Tsh 250 za ujezi wa kituo cha Afya kijiji cha Mwandugyembe ziletwe kijiji cha Ndulungu.” Alisema Mkuu huyo wa Wilaya na kuongeza kuwa
“Namna ya pili ni kuandaa muhtasari wa kuomba kata ambapo tukipata kata tutapata huduma ya shule, kituo cha afya na huduma nyingine za msingi zinazostahili kuwepo katani.”
Aidha aliwataka kuwa makini wakati wakuchagua kati ya hayo waliyokubaliana ili baada ya mchakato huo kusiwepo tena malalamiko.
“Niagize kuwa jambo hili muhakikishe mnashirikisha kijiji cha Mwandugyembe, Mahola, Kipuma pamoja na Ndulungu ili kupata maamuzi yasiyokuwa na manunguniko tena.” Alisema
Katika hatua nyingine amewataka wananchi hao kuhakikisha wanalinda amani kwa sababu ndio msingi wa maisha bora na kupata maendeleo yao.
“Niwaombe ndugu zangu tunakila sababu ya kumshukuru Mbunge wetu ambaye ni Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba ambaye amekuwa akipambana kuhakikisha fedha hizi zinatufikia kupitia wizara ya TAMISEMI, hivyo tutunze amani yetu katika kutekeleza miradi hii.”
Awali akiongea katika kikao hicho, Diwani wa kata ya Ndulungu, Ndugu Jilole alisema kuwa Kamati ya Maendeleo ya Kata ya wakati wa Diwani Iddi Muyonga walikubaliana kuwa kijiji cha Mwandugyembe na Mahola pajengwe Sekondari huku kijiji cha Kipuma na Ndulungu kujengwe kituo cha Afya.
Suala ya kujenga kituo cha afya kijiji cha Mwandugyembe kilipelekea baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mahola na Ndulungu kugomea shughuli za maendeleo na hivyo kufika kwa mkuu wa wilaya kwa ajili ya utatuzi.
Kwa upande wake mmoja wa wananchi wa kijiji cha Ndulungu akifikisha kero yake kwa mkuu huyo wa wilaya, Iddi Nyauli alisema kuwa kama mkuu huyo wa wilaya asinge fika kutatua mgogoro huo basi wangekwenda kushitaki kwa mkuu wa mkoa huo.
“Nikushukuru sana kwa hekima zako kwa utatuzi wa mgogoro huu kwa sababu usinge utatua huu mgogoro tungeufikisha mpaka kwa Mhe Rais Samia.” Alisema na kuongeza kuwa
“Kama ungozi wa wilaya ungeliona kuwa kijiji cha Ndulungu hakipo wilaya ya Iramba basi tupelekwe wilaya ya Ikungi.”
Naye Zakiya Kapande mkazi wa kijiji hicho akawasilisha kero yake mbele ya mkuu huyo wa wilaya na kumuomba kuwasaidia akina mama ambao wanaumia kwa michango mbalimbali wanayoitoa kufuatia shughuli za maendeleo.
“Nikombe Mkuu wa wilaya utusaidie sisi akina mama kwa sababu yapo magumu tunayoyapitia kutoka katika serikali yetu ya kijiji.”
MWISHO
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.