Na Hemedi Munga
tehama@irambadc.go.tz
Singida - Iramba. Mkuu wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida, Suleiman Mwenda amempongeza Mkurugenzi Mtendaji, Mhandisi Michael Matomora kwa kutilia mkazo suala la mapato na kutamani kuona bajeti ya Iramba inavuka Tsh 1.4 bilioni.
Mwenda ametoa pongezi hizo leo Ijumaa Januari 28, 2022 wakati alipokuwa akiongea na Madiwani katika kikao cha Baraza la Madiwani kota ya pili ya mwaka wa fedha 2021/2022 katika ukumbi mdogo wa Halmashauri hiyo mjini hapa.
“Waheshimiwa Madiwani pamoja na wataalamu wote niwaombe tusimamie vyanzo vyetu vya mapato tunaouwezo wa kukusanya fedha nyingi sana katika Halmashauri yetu.” Alisema Mkuu huyo wa wilaya
Aidha, alifafanua vyanzo mbalimbali vya ukusanyaji wa mapato ikiwemo kuanzisha chanzo cha kuingiza mifugo katika hifadhi mbalimbali hasa wafugaji ambao wamehamia katika hifadhi hizo bila ya kufuata sheria na utaratibu.
Pia aliahidi kuwa katika kipindi cha uongozi wake atahakikisha chanzo cha madini ya dhahabu kinazalishwa kufikia gramu laki sita (600,000) kwa mwaka ukilinganisha na kiwango cha gramu laki tatu na kumi na tisa elfu ( 319,000) ambazo zilikuwa zinazalishwa kwa mwaka katika miaka ya nyuma.
“Tukipata uzalishaji wa namna hiyo ni hakika gawio lake litakuwa kubwa, hivyo huenda nusu ya bajeti ya Iramba ikawa inatoka katika chanzo cha madini.” Alisema
Kufuatia maono hayo ya kuinua Iramba kuwa na bajeti kubwa, Mwenda amewaomba Madiwani wote kuhakikisha wanasimamia shughuli za maendeleo katika kata zao ikiwemo ukusanyaji wa mapato.
Halikadhalika, Mwenda amewataka watendaji wote kuhakikisha wanatimiza wajibu wao na kufanya utoaji wa huduma kwa wananchi zinakuwa nyepesi hatimaye wananchi wakiwemo wajasiriamali kutamani kufanya kazi na Halmashauri yao.
“Nitoe wito kwa watendaji wenzangu wa serikali tunapokuwa tunawasaidia wananchi kuhakikisha tunafuata sheria, kanuni na taratibu.” Alisema
Akiongea katika Baraza hilo Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Innocent Msengi alisema kuwa chanzo cha kuingiza mifugo ni kizuri, hivyo watakaa katika vikao vyao kuona namna bora ya kupitisha sheria ili kuweza kukusanya chanzo hicho.
Aidha, amewataka watendaji hao kuendelea kudumisha ushirikiano walionao ili kuhakikisha wanafikia malengo ya kuinyanyua Halmashauri hiyo katika ukusanyaji wa mapato.
“Niwaombe sana ndugu zangu vikao hivi vitakuwa vinatija ikiwa tutarudi katika vikao vijavyo halafu tukaona kunamabadiliko makubwa wa haya ambayo tumekubaliana.” Alisema Msengi
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo akiongea katika Baraza hilo, Mhandisi Michael Matomora alifafanua namna ambavyo anapambana kuhakikisha Halmashauri hiyo haipati hati yenye mashaka wala hati chafu katika Hesabu za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali.
“Mheshimiwa Mwenyekiti naomba kutoa ufafanuzi kuwa ili madokezo yapite katika ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji lazima yafuate utaratibu na kanuni za matumizi ya fedha za serikali.”Alisema Matomora na kuongeza kuwa
“Ni lazima tukakusanye mapato kwa sababu hatuwezi kutumia fedha kama hatujakusanya.”
Halikadhalika, alibainisha kuwa fedha ya serikali uliyoiweka katika bajeti na ukaikusanya usipoitumia ni kutengeneza hoja ya ukaguzi.
“Mimi siwezi kuzuia fedha ya serikali isitumike kwa sababu itakuja hoja kuwa Mkurugenzi Mtendaji hatumii fedha na hiyo hoja mimi siwezi kuikubali.” Alisisitiza
Aidha, aliongeza kuwa ataendelea kusimamia matumizi ya fedha za serikali yaliokuwa halali kwa sababu ya kuhakikisha Halmashauri inapunguza hoja za ukaguzi.
Pia amewataka wananchi wote katika Halmashauri hiyo, kufikisha mapendekezo yao ambayo yanatakiwa kuingia katika bajeti ya mwaka 2022/2023.
“Huu ni wakati wa bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023, hivyo nitoe wito kwa wananchi wote kuwa kama kuna mwananchi anaushauri anaalikwa kutoa ushauri kuwa nini Halmashauri ifanye katika mwaka wa fedha.” Alitoa wito Matomora
Baraza la Madiwani limekaa kikao chake cha kota ya pili katika mwaka wa fedha 2021/2022.
MWISHO
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.