Na Hemedi Munga
Singida - Iramba. MKUU wa wilaya ya Iramba mkoani Singida, Suleiman Mwenda amemshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa fedha alizoipatia Wilaya ya Iramba kutekeleza miradi ya maendeleo.
Mwenda ametoa pongezi hizo leo Jumapili 16, 2022 wakati akisoma taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/2025 kwa kipindi cha kuanzia julai hadi Disemba katika ukumbi mkubwa wa Halmashauri hiyo mjini hapa.
“Takribani 20 bilioni zimeletwa katika Wilaya hii kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo, kiwango hichi ni kikubwa sana, hivyo tunayo sababu ya kumshukuru Rais wetu Samia Suluhu Hassan.” Alisema komredi Mwenda na kuongeza kuwa
“Kwa kweli ni mara ya kwanza tena kota ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2021/2022 TARURA wamepata 6.5 bilioni kwa ajili ya barabara huku bilioni 5.2 kwa ajili ya miradi ya maji na nyingine nyingi katika sekta ya afya na elimu.”
Kufuatia kupata fedha hizo nyingi, Komderi Mwenda amewataka viongozi wote ngazi mbalimbali wilayani hapa kuhakikisha wanasimamia kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ufanisi na kiwango kinachohitajika.
“Sisi serikali tunayodhima kuhakikisha tunaisimamia fedha hii iliyoletwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, Samia Suluhu Hassan ili ifanye kazi iliyokusudiwa na kukamilika kwa kiwango stahiki.” Alisema
Pia amewataka wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Wilaya wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kushirikiana na serikali katika mambo mbalimbali kwa sababu umoja wao ni ushindi katika kila jambo.
“Nitowe wito kwa viongozi wenzangu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) niwaombe tushirikiane ili kutimiza matakwa ya ilani ya Chama chetu hatimaye kuboresha maisha ya wananchi ambao wamekichagua chama hichi na kukipa serikali.”
Aidha akiongelea kuhusu maisha yake ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Komredi Mwenda alisema kuwa anamshukuru Rais Samia kwa kumteua na kumuamini kuwa Mkuu wa wilaya hiyo, kazi ambayo itamfanya kuendelea kuvaa vazi la kijani ambalo analipenda tangu akiwa chipukizi katika chama hicho.
“Niseme kweli moja ya kitu kilichonifanya kuipenda CCM na kuingia katika kundi la chipukizi la chama hicho nikiwa darasa la pili ni nyimbo ambazo zilizokuwa zikiimbwa na Komredi Kaptain John Komba aliyekuwa Mbunge wa Mbinga Magharibi na muimbaji mkuu wa nyimbo za siasa nchini Tanzania.” Alisema
Akiongea katika mkutano huo kwa niamba ya wajumbe wote wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo, Ashel Joel ameipongeza serikali ya amwamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia kwa kuipatia fedha nyingi wilaya hiyo.
“Nimpongeze Rais wetu kwa kweli haijawahi tokea kupokea fedha nyingi kiasi hichi katika wilaya yetu ya Iramba kwa ajili ya miradi mbalimbali.” Alipongeza na kuongeza kuwa
“Tuko pamoja na mama na tutaendelea kuwa pamoja naye, tunaendelea kumpongeza kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuliongoza taifa letu, mungu ampe afya njema ili aendelee kututumikia sawa na mapenzi yake.”
Kwa upande wake mmoja wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, Diwani wa kata ya Ntwike, Albert Makwala akiongea kwa niaba ya wajumbe hao alisema kuwa wameipokea taarifa ya utekelezaji wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na hivyo wapo tayari kuijadili na kutoa maagizo kwa wataalamu.
Aidha anaishukuru serikali kwa kuitengea kata hiyo 460 milioni kwa ajili ya kufungua barabara ya kutoka Kiomboi kwenda Ntwike na kushauri kuwa wataalamu wa TARURA wangeanza na kivuko.
Naye Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama hicho kata ya Kiomboi, Israel Shimba akashauri kuhusu kumalizia Zahanati ambayo ilijengwa katika kata hiyo ili kuwasaidia akinamama wajawazito kupata huduma kwa haraka katika kituo hicho badala ya kupelekwa hospitali ya kiomboi ambayo inadaiwa kuwa mbali na wakazi hao.
MWISHO
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.