Na Hemedi Munga
tehama@irambadc.go.tz
Singida - Iramba. Mkuu wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida, Suleiman Mwenda amemuagiza Afisa Ardhi wilaya ya Iramba, Valerian Msigala kulipima eneo la Maluga linalodaiwa kuwa na mgogoro tangu kutoka katika siasa za vijiji na ujamaa ili kujua ukubwa wa eneo hilo na kutatua mgogoro huo.
Mwenda ametoa agizo hilo leo Jumatano Januari 26, 2022 wakati alipokuwa akiongea na wananchi wa kijiji cha Maluga wilayani hapa.
Akiongea na wananchi hao mkuu huyo wa wilaya amewaeleza kuwa kila mmoja atapata haki yake kwa kuhakikisha kuwa baada ya kutoa hekari 50 zinazodaiwa kumilikwa na mzee Amosi Shigimbi ambaye kwa sasa ni marehemu na mgogoro huo kuibuliwa na wajukuu wake.
“Niwahakikishie ndugu zangu kuwa wiki hii wataalam wa ardhi watakuja kutuonesha mipaka ya eneo hilo ili kufahamu eneo linalobaki ili kila mmoja apate ardhi aendeshe maisha yake kwa utulivu.” Alisema Mwenda
Aidha, aliongeza kuwa tunapaswa kuwaheshimu wazee wetu kwa sababu wanapotuombea dua ndio tunaweza kupata baraka.
Akiongelea kuhusu makaburi yaliopo katika ardhi hiyo, Mwenda amewataka wananchi hao kuheshimu ndugu ambao wametangulia mbele ya haki.
“Sisi sote ni wanakijiji ni lazima tuishi katika namna ya kupendana,kusaidiana na kushirikiana kwa sababu hayo makaburi wamehifadhiwa binaadamu ambao ni wazee wa wenzako.” Alisema
Pia aliwaomba wananchi hao, kufahamu kuwa waliohifadhiwa hapo ni wazee wa wenzao na binaadamu wenzao ni vyema wangeendelea kuheshimiwa.
Kufuatia hali hiyo Mwenda amewataka wananchi hao kuheshimu makaburi ya wanaadamu ambao walifariki na kuzikwa hapo.
Awali akiwasilisha malalamiko hayo kwa mkuu wa wilaya hiyo, Elizabeth Israel alishukuru hatua zilizochukuliwa na mkuu huyo wa wilaya kwa kutatua mgogoro huo ambao umekuwa wa muda mrefu.
“Mgogoro huo uliibuka baada ya tamko la Mwl. Julius K. Nyerere kusema kuwa watu warudi katika mahame yao, hivyo walivyorudi ndio ulipatikana mwanya wa watu kumiliki ardhi ambayo isiokuwa yakwao kutokana na oparesheni ya mwaka 1974 hadi 1976.” Alisema Israel
Halikadhalika, aliongeza kuwa ndio nafasi ambayo Mzee Amosi shigimbi alirudi katika ardhi yake kama walivyorudi watu wengine katika miaka hiyo.
Kwa upande wake mmoja wa wazee waliokuepo katika miaka hiyo ya siasa ya vijiji na ujamaa, Elias Mpwai alisema kuwa eneo la kujenga nyumba miguu 70 alipewa na Amosi Shigimbi wakati huo.
“Mzee Shigimbi alinipa eneo hilo kwa sababu nilikuwa nikichunga mifugo yake, hivyo nikawa nalima eneo hilo mpaka wajukuu wangu waliponisaidia kujenga nyumba na baadae kuibomoa kutokana na mamlaka ya wakati huo.” Alisema Mpwai
Kufuatia hali hiyo, Mpwai alimueleza mkuu huyo wa wilaya kwa sasa anapata tabu kwa sababu hana sehemu ya kulima kwa lengo la kujipatia chakula, hivyo amebaki anatanga tanga.
MWISHO
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.