Na Hemedi Munga
tehama@irambadc.go.tz
Singida - Iramba. Mkuu wa wilaya ya Iramba mkoani Singida, Suleiman Mwenda amewaagiza wamiliki wa mabucha, wachinjaji na wauzaji wa nyama kuuza kilo ya nyama mchaganyiko kwa Tsh 7000 na kilo ya nyama isiyokuwa na mifupa kwa Tsh 8000.
Mwenda ametoa agizo hilo leo Jumatano Aprili 6, 2022 wakati alipokuwa akiongea na wamiliki wa mabucha, wachinjaji na wauzaji wa nyama katika ukumbi mdogo wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba.
Agizo hilo linakuja ikiwa ni siku chache baada ya Mkuu huyo wa wilaya kufanya uchunguzi wa bei za kuuza nyama kwa kilo moja katika wilaya za Ikungi, Singida Manispaa na Mkalama ambako kote huko wamekuwa wakiuza kilo moja ya nyama kwa Tsh 7000.
Wakati wilayani Iramba hali ikiwa ni tofauti ambapo katika eneo la Mtekente kilo moja ya nyama ikiuzwa kwa Tsh 7000, Shelui Tsh 7000, Misigiri Tsh 7000, Oldi Kiomboi 7000 na Mjini Kiomboi ikiuzwa katika baadhi ya bucha kwa Tsh 8000, 9000 hadi 10,000 kwa kilo moja.
Ndani ya wilaya moja bidhaa moja ina bei tofauti tofauti kitu ambacho sio rafiki hata kama tuko katika soko huria, hivyo ipo haja ya kuwa na bei ya juu elekezi kwa wilaya nzima.
“Ni jambo la ajabu kabisa katika Jiji la Mwanza kilo moja ya nyama inauzwa Tsh 7000 halafu hapa Kiomboi kilo moja ya nyama inauzwa kwa Tsh 9000 mpaka 10000, hivyo tunakubaliana kuwa kiwango cha bei ya juu ya kilo moja ya nyama itakuwa Tsh 7000.” Alisisitiza Mkuu huyo wa wilaya nakuongeza kuwa
“Bei elekezi kwa sasa ni Tsh 7000 na hatutegemei kukuta bucha katika wilaya yetu inauza kilo moja ya nyama kwa bei zaidi ya Tsh 7000.”
Aidha, Mwenda alisema kuwa wanahitaji kuona katika wilaya hiyo katika siku za usoni wanapata machinjiyo ya kisasa ambayo yatakuwa yakiwezesha wanyama kuchinjwa hapo na kufungasha kwa ajili ya kuunza ndani ya wilaya, mkoa, Tanzania nzima na nje ya nchi.
Pia, alionesha kusikitika baada ya kuona ongezeko kubwa la bei ya nyama wakati anafika akiwa mkuu wa wilaya hiyo, kilo ya nyama ilikuwa ikiuzwa kwa Tsh 6000.
Halikadhalika, Mwenda amemuelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kuhakikisha katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 wanatenga fedha kwa ajili ya kujenga machinjio ya kisasa katika kila tarafa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kila nyama inapimwa na daktari ili kuthibitisha usalama na ubora wake.
Katika kuhakikisha nyanja ya mifugo inachangia katika mapato ya Halmashauri, Mkuu wa Wilaya hiyo kwa kushirikiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Mhandisi Michael Matomora walifanikiwa kuinua mapato yanayotokana na kuuza mifugo katika minada kutoka kwenye Tsh 16 hadi 18 milioni kwa makusanyo ya jumla ambapo kwa sasa imefikia Tsh 40 hadi 50 milioni.
Akiongea katika kikao hicho Mkuu wa jeshi la Polisi wilayani hapa Henry Makwasa amewataka wafanyabiarasha hao kutoa taarifa ya watu wanaouza nyama mitaani ili jeshi la polisi liwachukulie hatu kwa sababu hao ndio wanaodaiwa kuwa na tabia ya kuiba mifugo na kuchinja bila ya kufuata utaratibu.
Makwasa alimshauri Mkuu wa Idara ya Mifugo Dkt Dotto Thomas kuendesha oparesheni ya kuchanja mifugo ili mifugo hiyo iweze kunenepa na kuepukana na minyoo kwa sababu kufanya hivyo kutasaidia Iramba kuwa na ng’ombe wenye afya na ubora mkubwa.
Kwa upande wake mmoja wa wauzaji wa nyama wilayani hapa, Zakaria Shila alithibitisha kuwa wao katika maeneo yao wanauza kilo ya nyama kwa Tsh 6000 hadi 7000 kwa sababu wakiuza zaidi ya Tsh 7000 ua 8000 hakuna atakayenunua.
Naye Asha Juma mfanyabiasha ya mamantilie alimshukuru mkuu huyo wa wilaya kwa agizo la kupunguza bei ya kilo ya nyama iuzwe Tsh 7000 kwa sababu hapo awali walikuwa wakipata changamoto ya kununua kilo moja ya nyama kwa Tsh 8000, 9000 hadi 10000 kwa baadhi ya bucha mjini Kiomboi.
MWISHO
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.