Na Hemedi Munga
tehama@irambadc.go.tz
Singida - Iramba. Mkuu wa wilaya ya Iramba mkoani Singida, Suleiman Mwenda amewaomba waandishi wa historia kuendelea kuenzi na kuthamini mchango uliotolewa na wanawake kabla na baada ya Tanzania kupata uhuru.
Mwenda ametoa ombi hilo leo Jumanne Machi 08, 2022 wakati akihutubia maelfu ya wananchi waliohudhuria katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliofanyika kiwilaya katika viwanja vya Shule ya Wasichana Tumaini mjini hapa.
“Ni bahati mbaya sana kutotaja mchango uliofanywa na mwana mama shupavu kabla na baada ya uhuru wa Taifa letu Hadija Kamba ambaye aliwahi kusema na kudai kizazi cha haki na usawa kwa maendeleo endelevu.” Alisema Mwenda
Aidha, aliongeza kuwa kauli mbiu hii “Kizazi cha haki na usawa kwa maendeleo endelevu” ambayo leo tunajivunia ni kauli ya kishupavu na ukomavu iliyosemwa na mwana Mama Hadija Kamba ambaye ni mmoja wa waasisi wa Taifa la Tanzania na Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho kinaongoza nchi yetu.
Kwa mara ya kwanza Hadija Kamba alisikika akitajwa mwaka 1985 na Mwalimu Julius K. Nyerere wakati akiwahutubia wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM katika ukumbi wa Diamond Jubilee akiwa anawaaga na kuwatangazia rasmi kuwa anangatuka katika nafasi ya urais na kubaki kuwa Mwenyekiti wa CCM.
Mwalimu Nyerere alisema kuwa katika miaka 24 ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuna mwanamama ambaye alikuwa akimshangaza kwa sababu ni mwanamama ambaye alipambana enzi za ukoloni ili kulipatia Taifa uhuru.
“Katika kina mama waliokuwa mstari wa mbele katika mapambano enzi za Ukoloni katika siku ngumu na za hatari ni Hadija Kamba.” Alisema Mwalimu Nyerere
Baada ya kupata uhuru Mwalimu Nyerere alimwita Hadija Kamba nakutaka kumpa cheo ingawa alikataa na kuyasema maneno ya kishujaa ambayo leo siye tunajivunia.
“Lengo la kushiriki na kuingia katika mapambano ya kuondoa Ukoloni ilikuwa ni kuhakikisha tunapata jamii ya haki na usawa, hivyo nimeridhika kabisa kwa sababu lengo langu limetimia kwa sababu sasa Waafrika wanathaminiwa katika nchi zao na hawatawaliwi tena.” Alisema Kamba
Kauli hiyo ilimfanya Mwalimu nyerere kusema kuwa sio watu wengi walioshiriki mapambano hayo na hawakuwa wanalenga kupata madaraka ispokuwa ni wa chache akiwemo Hadija Kamba.
“Kwa bahati mbaya sana historia yetu kipindi cha Ukoloni, mapambano dhidi ya Ukoloni na hata katika kupata uhuru wetu hawatajwi wanawake hawa muhimu walioshiriki kwa namna moja au nyinginge kuhakikisha tunapata uhuru wetu.” Alikumbusha Mwenda na kuongeza kuwa
“Historia yetu imetaja sana wanaume kama vile wakati wanaume wakipambana hawakuwa na akina mama hawa, hivyo ni wakati sasa kwa waandishi wetu kuenzi na kuthamini michango iliyofanywa na wanawake hawa katika kulijenga Taifa letu” Alisisitiza
Akiongelea michango muhimu inayofanywa na Wananwake nchini, Mwenda alisema kuwa tunaye Mama ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambaye kwa kipindi cha miezi michache amefanya mambo makubwa ambayo hayajawahi tokea katika historia ya nchi yetu.
Aidha, alifafanua kuwa katika kipindi cha awamu ya kwanza ya urais hadi ya tano kwa wilaya ya Iramba kulikuwa na vituo vya afya vitatu laniki katika kipindi cha Rais Samia tayari Iramba inajenga vituo vya afya vitano na maendeleo haya ni katika wilaya zote za nchi yetu.
Kwa upande wa barabara kwa mara yakwanza katika kipindi hichi cha Rais Samia Iramba ilipata Tsh 6.5 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa barabara huku fedha nyingi yakwanza kuja wilaya ya Iramba tangu kupata uhuru ni Tsh 800 milioni.
Pia, katika nishati ya umeme tayari Mkandarasi ameishapatikana ambaye atamalizia vijiji 14 vilivyokuwa havina umeme, hivyo ni dhahiri sasa Iramba itakuwa haina kijiji ambacho hakina umeme.
Halikadhalika, kwa upande wa madarasa kwa ajili ya wanafunzi Iramba ilifanikiwa kupata fedha na kujenga madarasa 67 huku madarasa zaidi ya elfu kumi na tano (15,000) kwa Tanzania nzima.
Katika kuhakikisha mama anatuliwa ndoo kichwani na maji yanapatikana kwa urahisi takribani Tsh 4.8 bilioni zinatekeleza miradi mbalimbali ya maji nakuifanya Iramba kufikia asilimia 52 ambapo wakati Rais Samia anaingia madarakani Iramba ilikuwa na asilimia 26.
“Kwa kweli kwa ushahidi na takwimu hizi ninashawishika kusema kuwa tukiwaamini wanawake katika nafasi za uongozi tutapata matokeo chanya.” Alisema
Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati Tendaji Taifa ya Chama cha Walimu (CWT), Mwl. Ulumbi Shani alisema kuwa ukimuelimisha mama utakuwa umelielimisha Taifa. Hivyo tunaendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa sababu ni Mama ambaye anaendelea kututangazia kwamba kinana mama tunaweza katika nyanya zote.
“Ni hakika kwamba Mama ni chanzo cha kila fani na nichanzo cha mafanikio ya kiuchumi, kijamii na kisiasa katika familia na Taifa kwa ujumla.” Alisema Shani
Naye Sara Mitula Mkazi wa Kinampanda wilayani hapa alimuomba Mkuu huyo wa Wilaya kuendelea kutokomeza unyanyasaji wa jinsia ambao wamekuwa wakikutana nao katika mazingira tofauti tofauti hasa katika makabila ambayo bado yanatekeleza mfumo dume.
Aidha, Sara ameitaka jamii kutambuwa kuwa maendeleo endelevu ni lazima yahusishe jinsia zote kwa kuzingatia haki na usawa ili kukuza uchumi wa jamii na Taifa.
MWISHO.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Mhandisi Michael Matomora akiwa na Mwnyekiti wa Halmashauri hiyo Innocent Msengi wakicheza mziki kuwaunga mkono wakina mama katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliofanyika katika viwanja vya shule ya wasichana Tumaini kata ya Kinampanda Wilayani Iramba Mkoa wa Singida. Picha na Hemedi Munga
Hivi ndivyo wanawake walivyopendeza katika picha ya pamoja wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliofanyika katika viwanja vya shule ya wasichana Tumaini kata ya Kinampanda Wilayani Iramba Mkoa wa Singida. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.