Na Hemedi Munga
tehama@irambadc.go.tz
Singida - Iramba. Mkuu wa wilaya ya Iramba mkoani Singida, Suleiman Mwenda amewasihi wananchi wa kijiji cha Ndulungu kuwa na subira wakati serikali ikiendelea kupanga na kutekeleza mikakati ya kuwaletea wananchi hao miradi ya maendeleo.
Mwenda ameyasema hayo mwishoni mwa juma hili wakati alipokutana na wananchi wa kijiji cha Ndulungu wilayani hapa.
Usia huo unatokana na agizo alilolitoa Mkuu huyo wa wilaya wiki moja iliyopita kuitaka Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Ndulungu kukubaliana kuchagua kati ya takribani Tsh 350 milioni zinazotarajiwa kutengeneza barabara kijiji cha Ndulungu na takriban Tsh 250 milioni kwa ajili ya kujenga kituo cha afya kijiji cha Mwandugyembe ndani ya kata hiyo.
Miradi hii ilidaiwa kuzua mgogoro kati ya wananchi wa kijiji cha Mwandugyembe kunakotarajiwa kujengwa kituo cha afya huku kijiji cha Ndulungu itengenezwa barabara, jambo ambalo wananchi wa kijiji cha Ndulungu hawakukubaliana nalo wakidai kuwa miradi mingi inapelekwa katika kijiji cha Mwandugyembe.
Akieleza maamuzi ambayo yalifikiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya kata hiyo, Kijiji cha Ndulungu na Kamati ya Maendeleo ya kata hiyo, Mwenda alisema CCM waliamaua kituo hicho cha afya kijengwe Mwandugyembe kwa sababu ndio maelekezo ya muongozo toka serikali kuu. Huku muhtasari wa kijiji cha Ndulungu wakiamua kuwa kituo hicho kijengwe Ndulungu wakati muhtasari wa Kamati ya Maendeleo ya Kata wakiamuwa kuwa kituo hicho kijengwe kijiji cha Mwandugyembe.
“Hivyo ndugu zangu ni dhahiri serikali kuu walizingatia sababu nyingi za kujenga kituo cha afya Mwandugyembe, hata maamuzi ya CCM pamoja na Kamati ya Maendeleo ya kata yamehitaji kituo hicho kijengwe Mwandugyembe, hivyo niwaombe wananchi wa Ndulungu kuwa na subira serikali itajenga kituo cha afya Ndulungu kadri uwezo utakavyoruhusu.” Aliomba Mwenda
Aidha, aliongeza kuwa serikali itafikisha huduma ya afya katika kila kijiji ndani ya kata huku akitolea mfano wa huduma ya umeme ambayo kwa wilaya ya iramba yenye vijiji 74 ambapo vijiji 60 vinaumeme na vijiji 14 tayari mkandarasi ameisha patikana kufikisha umeme katika vijiji hivyo.
Akitoa shukrani mbele ya mkuu huyo wa wilaya Mwenyekiti wa Chama cha Mpinduzi (CCM) wa kata hiyo, Said Hassan aliomba kuwa jambo hili liendelee kuelezewa vizuri zaidi.
“Nikushukuru Mkuu wa wilaya na timu yako kwa namna ambavyo umejitahidi kulielezea na kutatua mgogoro huu, hivyo tunaomba kadri uwezo utakavyokuwa ukipatikana basi tuelekeze maendeleo kijiji cha Ndulungu.” Alisema
Kwa upande wake mmoja wa wananchi wa kijiji hicho, Mwanaidi Nyauli alisema kuwa yote yalioongelewa na Mkuu huyo wa wilaya yamezidi kuwatia uchungu.
“Kwa kweli tunamachungu kwa sababu mnada umepelekwa Mwandugyembe, sekondari imejengwa Mwandugyembe na sasa kituo cha afya kinajengwa Mwandugyembe, Jamani serikali tunaomba mtuonee huruma na sisi wa Ndulungu mtufanyie hima tupate kituo cha afya.” Alisema
Naye Jafari Kamoko akasema kuwa kituo cha afya kilipaswa kijengwe Ndulungu kwa sababu Mwandugyembe tayari wamepata mnada na shule ya sekondari.
Aidha, alieleza kuwa swala la kila kitu kinapelekwa Mwandugyembe kinafanya wananchi waone kuwa kuna upendeleo.
MWISHO
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.