Na Hemedi Munga
tehama@irambadc.go.tz
Singida - Iramba. Mkuu wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida, Suleiman Mwenda amewataka wananchi wote kuyatunza mazingira kwa sababu mazingira yanatabia ya kumtunza anayeyatunza mazingira.
Mwenda ametoa wito huo mwishoni mwa juma hili wakati alipokuwa katika Bonde la Wembere kupanda miti ya gundi wilayani Iramba.
“Ndugu zangu fahamuni kuwa mazingira huwa yanatabia, ukiyatunza yanalipa fadhila na ukiyaharibu pia yanakulipa fadhila.” Alisema Mkuu huyo wa wilaya
Aidha, aliongeza kuwa moja ya majibu yanayotokona na kuyaharibu mazingira ni kuadimika kwa mvua na kujikuta nchini katika maeneo mbalimbali watu wanaangaika pamoja na kuomba maombi ili Mungu alete mvua.
Halikadhalika, alibainisha kuwa yapo mambo ambayo yamewekwa kikanuni kwamba ili mwanadamu apate mvua ni lazima awe na miti ambayo inasaidia kuwepo kwa mvua.
“Nitoe wito ndugu zangu tupande miti, tuitunze na kuilinda ili ikistawi iweze kutuletea mvua.” Alisema
Ni hakika kila mtu anategemea mvua kwa sabubu uwepo wa mvua ndio unasaidia wakulima kuweza kulima na kupata chakula ambacho hufukuza njaa, hivyo ili kuikimbiza njaa ni lazima tuitunze misitu yote.
Kufuatia upandaji wa miti unaondelea wilayani hapo, Mkuu huyo wa wilaya amewataka wafugaji na wakulima wote kuwa wahakikishe wanatunza misitu hiyo kwa sababu ikiwa hawatatunza watachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Ndugu zangu siwezi kuona zaidi ya milioni mia mbili (200,000,000) zimeingizwa katika mpango huu na serikali kupanda miti zinaharibika kwa sababu ya watu wachache wasiotakakufuata sheria na kanuni tulizojiwekea, nitakuwa mkali mimi pamoja na kamati yangu ya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na TFS kuwachukulia hatua.” Alionya Mwenda na kuongeza kuwa
“Wapelekeeni ujumbe watu wote kuwa miti hii tumepanda ni kwa manufaa yetu sio kwa manufaa ya watu wengine, hivyo tuitunze ili itutunze.”
Awali akitoa taarifa fupi wakati wa zoezi lakupanda miti likiendelea Meneja wa Wakala wa Misitu Tanzania wilayani hapa, Shabani Nyamasagara alisema kuwa tayari wamekwisha panda miti laki mbili (200,000) katika hekari 500 na kubakiwa na miche 50 ambayo itapandwa kukamilisha hekeri 625.
Nyamasagara alisema kuwa wanapanda miti katika hifadhi ya msitu wa Wembere kwa sababu hapo awali ulikuwa na miti ya migunga ambayo ilikuwa inazalisha gundi lakini misitu hiyo iliharibiwa.
Pia alisema wanapanda miti hiyo ikiwa ni jitihada za kurudisha uoto wa asili pamoja na kupambana na uharibifu wa mabadiliko ya tabia ya nchi.
“Mheshimiwa Mkuu wa wilaya pamoja na zoezi hili lakupanda miti pia TFS imezalisha ajira ya zaidi ya watu mia moja (100) kwa kila siku hasa katika kipindi cha kuotesha miti na wakati wa kupanda miti.”
Aidha, aliongeza kuwa wanaiomba jamii zinazoishi pembezoni mwa hifadhi hizo kuona kuwa uwepo wa misitu hiyo ni sehemu ya kutengeneza ajira kwa vijana na kuweza kujipatia kipato.
Kwa upande wake diwani wa Kata ya Urughu, Simon Tyosela aliomba kuwa msitu huo wanaoupanda kuwa endelevu kwa sababu unasaidia kutoa ajira.
Pia alimuomba meneja wa TFS kuhakikisha kuwa msitu huo uwe na wale wadudu wanaosaidia kuzalisha gundi ili gundi ipatikane kwa wingi.
Naye mmoja wa wananchi ambaye anaishi pembezoni mwa hifadhi hiyo, Shabani Juma aliwaomba wananchi wenzake kuwa watunze miti ya Migunga ambayo wanaipanda kwa sababu miti hiyo itawasidia hapo baadaye.
“Kwa kweli nipo hapa katika zoezi la kupanda miti nikijivunia kuwa miti hii itanisaidia baadaye pamoja na kuboresha mazingira, hivyo natoa wito kwa wananchi wenzangu kuwa tuyapende mazingira yetu yatatusaidia baadae.” Alisema
MWISHO
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.