Hemedi Munga Irambadc
Iramba. Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda amemuagiza Kamanda wa TAKUKURU, Ahmed Sungura kumkamata na kumuhoji Mwenyekiti wa Kijiji cha Msai Kata ya Mtoa Wilayani Iramba Mkoa wa Singida.
Mwenda ametoa agizo hilo leo Jumanne Agosti 24, 2021 punde baada ya kusikiliza kero ya Wananchi alipotembelea kijijini hapo.
Akitoa kero kwa niaba ya wananchi wa kijiji hicho mbele ya Mkuu huyo wa Wilaya, Mwenyekiti wa kitongoji cha Lutamla, Ngasa Kasema, amewasilisha kuwa Wananchi wa kitongoji hicho wanalalamikia fedha zao walizochanga mwaka 2018 kwa ajili ya kuwekewa alama za utambulisho wa mipaka katika ardhi (beacon) ili kutambulisha eneo la malisho na ulimaji la wanakijiji hao.
Ameainisha kuwa Wananchi hao walichangishwa kila moja takribani laki tano (500,000) kwa watu kumi na tisa (19) na kufanya jumla ya Tsh milioni tisa na laki tano (9, 500, 000 ).
Ngasa amesema kuwa hivi karibuni kumewekwa alama za utambuzi wa mipaka katika ardhi (beacon) ndani ya makazi ya watu bila ya Wananchi kuhusishwa, hivyo kuliona tukio hili kuwa ni la kifisadi na kumuomba Mkuu huyo wa Wilaya kuutatua mgogoro huo ili wananchi wapate haki yao.
Kufuatia kero hiyo, Mkuu huyo wa Wilaya, akatoa agizo kwa TAKUKURU kumkamata Mwenyekiti wa Kijiji hicho pamoja na kila aliye husika katika kuchukua fedha hizo kuwahoji ili kuhakikisha haki ya wananchi inarejeshwa kwa Wananchi.
“Niagize kuwa mpaka kufikia tarehe 15 Septemba mwaka huu fedha za hawa Wananchi ziwe zimerudi na mimi nitarudi tarehe hiyo hapa kwa ajili ya kikao” amesisitiza Mwenda
Katika hatua nyingine Mwenda amewataka wananchi hao kuwa na imani na Serikali inayoongozwa na Mhe, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa sababu hivi karibuni imewaletea fedha milioni mia nne (400,000,000) kwa ajili ya kujenga kituo cha Afya kata ya Mtoa, hivyo kuondoa kabisa changamoto ya upatikanaji wa huduma za Afya.
Akiongelea Zahanati iliyojengwa na Wananchi wa kijiji hicho na kuiomba Serikali kuwaunga mkono kuimalizia, Mwenda amewatoa hofu wananchi hao na kuwahakikishia kuwa Serikali tayari imeleta takribani milioni themanini (80,000,000) kwa ajili ya kukamilisha Zahanati hiyo.
Akiongea na Mwandishi wetu, Mwenyekiti wa Kijiji cha Msai, Samwel Shillah amekanusha kuwa hakuchangisha fedha yoyote kutoka kwa wananchi hao.
“Mimi sijachangisha fedha ya aina yoyote, ispokuwa kwa fedha yangu mwenyewe nimenunua simenti kwa makubaliano na serikali ya kijiji na Muhtasari ninao” amekanusha Sillah
Kwa upande wake mmoja wa Wananchi waliohudhuria Mkutano huo, Yustina Klementi amemuomba Mkuu huyo wa Wilaya kuwasaidia kwa sababu wamekuwa wakionewa sana na Serikali ya kijiji chini ya Mwenyekiti huyo.
“Mhe, Mkuu wa Wilaya hata kero hii tunayoiwasilisha kwako nafahamu kwa tabia ya Mwenyekiti wetu atakuwa na uadui kwa aliye wasilisha kero hii, tusaidie!” ameomba Klementi
Changamoto hiyo imedaiwa kuibuka baada ya Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kuweka alama nyingine za utambauzi wa mipaka katika ardhi (beacon) kwa ajili ya eneo la kuhuisha msitu katika mbonde la Wembere na makazi ya Wananchi Wilayini humo.
MWISHO
Viongozi wa Kijiji cha Ujungu Wilayani Iramba wakimvika uchifu na kumuomba Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda kuwa Mlezi wa Kijiji hicho punde alipofanya ziara Kijijini hapo. Picha na Hemedi Munga
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda akiagiza wananchi wa Kijiji cha Ujungu kutunza miti iliyopandwa na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) . Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.