Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda akiwa katika picha ya pamoja na watoto waliogawiwa magodoro na vitanda. Picha na Hemedi Munga
Hemedi Munga, Irambadc
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda akiwaasa Wazazi kuendelea kumuomba Mungu atuondolee ugonjwa wa covid 19 pamoja na kuchukua tahadhari, hivyo kunawa maji tiririka, kuvaa barakoa na kukaa kwa kuachiana nafasi. Picha na Hemedi Munga
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Chacha Kehogo akiwatambulisha Viongozi mbalimbali walioambatana na Mkuu wa Wilaya ya Iramba,
Iramba. Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda amegawa magodoro na vitanda kwa watoto 58 wanaolelewa na kituo cha Maendeleo ya Mtoto na Kijana kilichopo chini ya kanisa la EAGT Kiomboi.
Mwenda amegawa vifaa hivyo leo Ijumaa Julai 9, 2021 katika viwanja vya Kanisa la EAGT liliopo Mjini hapa.
Amewataka walezi wa watoto hao kuhakikisha wanatunza vizuri vitanda na magodoro vilivyogarimu Tsh 11.1 milioni ili viweze kudumu kwa muda mrefu.
“Ndugu zangu ! Mungu amewachagua nyinyi katika wengi kupata msadaa huu wa magodoro na vitanda, hivyo mwende mkavitunze viweze kuwanufaisha kwa muda mrefu” amesema Mwenda na kuongeza kuwa
“Niwaombe ndugu zangu kuendelea kumuomba Mungu atuondolee ugonjwa wa covid 19 pamoja na kuchukua tahadhari, hivyo tunawe maji tiririka, kuvaa barakoa na kukaa kwa kuachiana nafasi.”
Pia amewataka Wazazi kuendelea kuwalea watoto vizuri ili waendelee kupata elimu itakayowasaidia kupambana na mazingira mbalimbali katika maisha yao.
Akiongea katika hafla hiyo fupi, Mchungaji wa Kanisa la EAGT, Robert Kijanga amesema kuwa suala la kuwasaidia watoto yatima ambao wamepoteza wazazi wao kwa namna tofautitofauti ni suala la muhimu katika jamii yetu.
“Lazima tufanye haya kwa sababu maadili ya kimungu yametufundisha kutoa zaka na sadaka ili kupata baraka za Mungu.” Amesema Mchungaji Kijanga
Mapema akisoma historia fupi ya kuanzishwa kituo cha Maendeleo ya Mtoto na Kijana, Mratibu wa Kituo, Emmanuel Kadama amesema kuwa Shirika limejikita kuwasaidia watu wanaoishi katika mazingira magumu ili kuwakomboa katika umasikini ulio katika nyanja ya kiroho, kiakili, kimwili, kiuchumi na kijamii.
Kituo kinaidadi ya watoto na vijana 297 wanojipatia huduma mbalimbali kwa lengo la kuwanusuru toka katika umasikini.
Aidha Kanisa limefanikiwa kuanzisha chuo cha ufundi kwa lengo la kuendelea kuwainua watoto kupata ujuzi wa kushona, ualimu wa elimu ya awali, elimu ya afya, ufundi magari, uchomeleaji na elimu ya kompyuta.
Kwa upande wake mmoja wa walezi wa watoto hao, ameushukuru uongozi wa Kanisa hilo kwa kufanikisha zoezi la kuwagawia vitanda na Magodoro.
Aidha ameahidi kuwa watavitunza vifaa hivyo ili viweze kuwanufaisha watoto kwa muda mrefu.
Kituo cha Maendeleo ya Mtoto na Kijana chenye namnba za usajili T20686 kilianzishwa mwaka 2014 kwa ushirikiano wa Kanisa na Shirika la Compassion International Tanzania lenye makao yake Makuu Jijijni Arusha.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.