Hemedi Munga Irambadc
Iramba. Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda ametoa ofa ya kwenda katika Hifadhi ya Taifa yoyote Nchini kwa walimu wa Shule ya Sekondari Lulumba waliofaulisha Wanafunzi wa kidato cha Sita kwa asilimia mia moja mwaka 2021.
Mwenda ametoa ofa hiyo leo Ijumaa Julai 30, 2021 wakati wa hafla fupi ya kuwapongeza Walimu pamoja na Wanajumuiya wa Shule ya Sekondari Lulumba iliyopo Mjini Kiomboi Wilayani Iramba Mkoa wa Singida.
Akiongea katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya amewapongeza wanajumuiya ya Sekondari ya Lulumba kwa kumuheshimisha na kuuheshimisha Mkoa wa Singida kufuatia kuingiza katika kumi bora Kitaifa somo la fizikia kushika nafasi ya 5 kati ya 462 na somo la jiografia kushika nafasi ya 7 kati ya 750 huku masomo yote 7 yakiongoza kimkoa.
“Ndugu wanajumuiya mpenipa heshima kubwa ambayo ninahitajika kuilinda na kuiendeleza kwa kutimiza mtazamo wangu wa kwanza wa elimu katika uongozi wangu wilayani hapa.” Ameshukuru Mwenda na kuongeza kuwa
“Ni nyinyi Walimu ndio mtakaonivusha hapa, hivyo fahamuni kuwa tunayo kazi kubwa ya kuimarisha na kuyaendeleza mafanikio haya.”
Kufuatia ufaulo huo, Mwenda ametoa ofa ya kwenda katika Mbuga yoyote ya Wanyama Tanzania na kukaa huko kwa muda wa siku tatu, akiamini kuwa Walimu hao baada ya kurejea watakua na ari na kasi mpya itakayowezesha matokeo ya mwakani shule ya Lulumba kuingia katika kumi bora kitaifa.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya amewahakikishia Walimu kuwa atakuwa mstari wa mbele kutatua changamoto zao wakati na mahali popote utakapohitajika msaada wake.
Awali akitoa taarifa fupi mbele ya Mkuu huyo wa Wilaya, Mkuu wa Shule ya Sekondari Lulumba, Jeremia Kitiku amesema kuwa Shule imekuwa inapata mafanikio ya kupanda kwa ufaulu wa kidato cha sita mwaka hadi mwaka.
Akifafanua ufaulu huo, Kitiku amesema kuwa mwaka 2018/2019 walifaulu wanafunzi 71 sawa na asilimia 100, mwaka 2019/2020 walifaulu wanafunzi 151 sawa na asilimia 100 na mwaka 2020/2021 walifaulu wanafunzi 130 sawa na asilimia 100.
Aidha Kitiku amebainisha mikakati ambayo itawasaidia kufikia malengo ya kuingia kumi bora kitaifa mwakani kuwa ni kuhakikisha walimu wanajiandaa ipasavyo na kufundisha kila kipindi ili kumaliza mada mapema na kufanya marejeo, kuandaa mitihani mingi ya ndani na nje kwa vidato vya mitihani, kuwa na vikao vya tathimini vya mara kwa mara kwa kila ngazi na idara na kushirikiana na shule nyingine za ndani na nje ya wilaya yetu ili kukuza ufanisi wa walimu na wanafunzi.
Jumuiya ya Shule ya Lulumba imekuwa ikitoa motisha ya chai, chakula cha mchana na fedha kutokana na namna mwalimu atakavyopata daraja, jambo mbalo limekuwa chachu ya mafanikio hayo.
Akiongea na Mwandishi wetu, Mwalimu wa Taaluma wa Shule hiyo, Nyakusuma Sospeter amesema kuwa Shule imewatunuku motisha Tsh 5.6 milioni Walimu mbalimbali waliofaulisha kwa kupata daraja la A na B.
Amefafanua kuwa Walimu waliofaulisha kidato cha pili wamepata laki tano na tisini (590,000), kidato cha nne 2.1 milioni, kidato cha sita 1.9 milioni na Idara mbalimbali kupata laki tisa elfu saba na mia tano (907,500).
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari wa Halmashuri hiyo, Godfrey Mwanjala amesema kuwa mafanikio hayo yanatokana na upendo na ushirikiano walionao kati yao na Utawala, hivyo amewaomba wadumishe mwenendo huo ndio utakaowawezesha kufuta daraja la 3, 2 na zero.
Naye mmoja wa walimu wa Shule hiyo, Madamu Sarafina amemuahidi Mkuu huyo wa Wilaya kuwa matoke ya kidato cha sita mwakani wataingia katika kumi bora Kitaifa.
Shule ya Sekondari Lulumba kwa sasa inawanafunzi 971 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita ambapo 370 ni wasichana na 601 ni wavulana.
MWISHO
Mkuu wa Shule ya Lulumba Sekondari, Jeremia Kitiku akifafanua ufaulu wa kidato cha sita kuwa mwaka 2018/2019 walifaulu wanafunzi 71 sawa na asilimia 100, mwaka 2019/2020 walifaulu wanafunzi 151 sawa na asilimia 100 na mwaka 2020/2021 walifaulu wanafunzi 130 sawa na asilimia 100. Picha na Hemedi Munga
Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari, Godfrey Mwanjala akiwataka wanajumuiya ya Lulumba Sekondari kudumisha mafanikio ya ufaulu yanatokana na upendo na ushirikiano walionao kati yao na Utawala, hivyo mwenendo huo ndio utakaowawezesha kufuta daraja la 3, 2 na zero. Picha na Hemedi Munga
Walimu mbalimbali wa Lulumba Sekondari wakifuatilia nasaha za viongozi mbalimbali wakati wa hafla fupi ya kuwapongeza Walimu pamoja na Wanajumuiya wa Shule ya Sekondari Lulumba iliyopo Mjini Kiomboi Wilayani Iramba Mkoa wa Singida. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.