Na hemedi Munga
SINGIDA-Iramba, Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda amewatahadharisha Wenyeviti wa kamati ya Sensa ya Watu na Makazi ngazi ya Wilaya, Kata, Kijiji na Kitongoji dhidi ya mawazo finyu yanayodaiwa kuenezwa na baadhi ya watu wasiolitakia mema Taifa la Tanzania.
Mwenda ametoa tahadhari hiyo leo Alhamisi Oktoba 21, 2021 wakati akiongea na Wenyeviti wa kamati ya Sensa ya Watu na Makazi ngazi zote katika kijiji cha Nselembwe Tarafa ya Shelui Wilayani hapa.
“Ndugu zangu ili inchi iendelee inahitaji mipango na mikakati madhubuti ya maendeleo ambayo hufanikishwa na takwimu zinazoongoza kujua idadi kamili ya uhitaji ambapo Taifa linatakiwa liwahudumie, halikadhalika idadi ya wazalishaji ili Taifa liwaunge mkono katika kuzalisha.” Alisema Mkuu huyo wa Wilaya na kuongeza kuwa
“Ndugu viongozi, ni lazima sasa tuanze kujipanga kuelekea Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2022 kwa kutoa taarifa kwa wananchi wetu kuwa kutakuwa na zoezi la Sensa, zoezi la kitaifa ambapo Serikali inalitegemea, hivyo tujipange kutekeleza kwa ufanisi.”
Katika kulitekeleza hili amewataka wenyeviti hao kuhakikisha wanaunda kamati na kuanza kutoa taarifa ya utekelezaji wa Sensa ya Watu na Makazi punde baada ya kupokea taarifa hiyo.
Amewataka kufahamu kuwa Sensa ni muhimu kwa Taifa lao kwa kuwa Taifa huweza kufahamu kuwa ni huduma kiasi gani ziende kwenye maji, umeme, barabara na huduma nyinginezo ambazo Serikali huzitoa kwa raia wake.
“Taarifa hizi ambazo hueleza kuwa ni wananchi wangapi, wanapatikana wapi, wanahitaji huduma kiasi gani na wanaishi katika hali gani Serikali inahitaji taarifa hizi kwa ajili ya kuweka mipango yake vizuri.” Alisisitiza Mwenda
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya amewataka Wenyeviti hao kuwa na tabia ya kujitolea kuitumikia Serikali kwa uzalendo wa hali ya juu kwa sababu maendeleo wanayoyaona leo ni kutokana na moyo wa kizalendo ambao Mwl J.K. Nyerere Rais wakwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliujenga katika Taifa hili.
Alifafanua kuwa maendeleo na mafanikio makubwa yaliofikiwa na Tanzania na Duniani kwa ujumla yamepatikana kwa sabubu wananchi wa nchi husika walikuwa na tabia ya kujitolea.
“Napenda kuwakumbusha ndugu zangu kuwa maendeleo na usalama wa nchi ya Tanzania mnaouona ni kutokana na mioyo ya kujitolea aliyoijenga Mwl. J.K Nyerere.” Alikumbusha Mwenda
Tanzania imekuwa nchi ya amani, upendo na usalama ukilingani na nchi jirani mfano wa Kenya, Uganda, Msumbiji na Rwanda ambazo zimedaiwa kuwa na mapigano ya mara kwa mara kwa sababu za makabila na nyinginezo, huku makabila mfano wa Wayao, Wamakuwa na mengineyo ambayo hupigana kwa ajili ya maslahi binafsi.
Wakati makabila ya Wayao, Wamakuwa na mengineyo yapo nchini Tanzania lakini hawapigani kwa sababu Mwal. J.K. Nyerere alijenga misingi ya kuvumiliana na kila mmoja apate maendeleo katika Taifa hili.
Akiongea kwa niamba ya wenyeviti hao, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nselembwe Tarafa ya Shelui, Paulo Daninga amemuhakikishia Mkuu huyo wa Wilaya kuwa wataunda kamati kwa namna ambayo muongozo unavyoelekeza na kuanza uhamasishaji wa Sensa ya watu na Makazi mwaka 2022 siku chache baada ya mkutano huo.
“Asante Mkuu wa Wilaya! nikuhakikishie kuwa maelekezo yote ulioyatoa tutayafanyia kazi kwa umakini.” Aliahidi Daninga na kongeza kuwa
“Ndugu zangu viongozi niwaombe katika maeneo yenu kuhakikisha kuwa hakuna migogoro kwa sababu migogoro haileti maendeleo wakati nchi hii inahitaji maendeleo.”
Kwa upande wake Afisa Tarafa wa Tarafa hiyo, Nicholaus Makoye amewataka wenyeviti hao kuifikisha elimu ya Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2022 iliyotolewa na Mkuu huyo wa Wilaya kwa wananchi ili wawe tayari kwa zoezi hilo la kitaifa.
MWISHO
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda akiwaelekeza majukumu ya utekelezaji wa Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2022 Wenyeviti wa Sensa ya Watu na Makazi ngazi ya Wilaya, Kata, Kijiji na Kitongoji kijiji cha Nselembwe Tarafa ya Shelui Wilayani Iramba Mkoa wa Singida. Picha na Hemedi Munga
Baadhi ya Wanyeviti wa kamati ya Sensa ya watu na Makazi mwaka 2022 wakifuatilia kwa makini majukumu yao yaliokuwa yakiwasilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda. Picha na Hemedi Munga.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.