Hemedi Munga Irambadc
Singida - Iramba. MKUU wa Wilaya ya Iramba,
Suleiman Mwenda amempongeza Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Mhandisi Michael Matomora kwa kununua kifaa cha upimaji wa mipaka ya ardhi (DGPS S86 RTK) kitakachowezesha Wananchi kupata Hati miliki ya viwanja vyao na kuepuka migogoro ya ardhi Wilayani Iramba Mkoa wa Singida.
Mwenda ametoa pongezi hizo leo Jumanne Oktoba 12, 2021 wakati akiongea na Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi na timu yake toka katika Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi walipotembelea Ofisi ya Mkuu huyo wa Wilaya Mjini hapa.
Amebainisha kuwa mpaka kufikia leo maombi ya Wananchi waliyoomba kupimiwa viwanja vyao ili waweze kupata hati miliki yamefikia takribani zaidi ya elfu nne (4000).
“Wananchi wemekuwa na hamu yakupata hati ya umiliki wa maeneo yao kwa sababu migogoro yao mingi ya kifamilia imekuwa ikisababishwa na ardhi.” amefafanua Mwenda
Katika hatua nyingine amempongeza Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi kwa kutuma timu maalumu kwa ajili ya upimaji wa vijiji vyote Wilayani Iramba nakuifanya Wilaya hii kuwa ya mfano kati ya Wilaya zote nchini Tanzania.
“Ndugu viongozi karibuni Iramba, tuhakikishe kuwa kila mmoja katika Wilaya hii anamiliki ardhi kihalali” amesisitiza Mkuu huyo wa Wilaya na kuongeza kuwa
“Tunataka wananchi waweze kuibadilisha ardhi hiyo kuwa mali kamili itakayowawezesha kupata mikopo katika benki mbalimbali na kuepukana na mikopo ya watu wajanja wajanja.”
Mikopo ambayo imekuwa ikiwafanya wananchi hao kubaki wakiwa ni masikini kutokana na kuuza mazao yao kwa njia ya mikopo iliyokuwa rahisi hasa kabla ya mavuno na kutakiwa kulipa punde wanapokuwa wamevuna mavuno yao na kuwafanya washindwe kunufaika na kuinufaisha Serikali.
“Kwa hiyo tunakwenda kwenye zoezi la urasimishaji wa ardhi ili wananchi wamiliki ardhi kihalali na kumaliza migogoro yote” amebainisha Mwenda na kufafanua kuwa
“Wananchi watakaopata hati miliki ya ardhi kihalali itawasaidia kusomesha watoto wao, kuchukuwa mikopo ya kibiashara, mikopo ya kilimo na kufanya mauziano ya kisheria hasa katika maeneo yenye madini.”
Halikadhalika, Mwenda amemshukuru Mhe, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa timu aliyoiunda iliyoongozwa na Mhe, Waziri Lukuvi kwa maamuzi ya kuwaacha wananchi katika maeneo ambayo wamekwisha anzisha vijiji katika maeneo hayo, hivyo hakuna sababu ya kuwahamisha isipokuwa waachwe waendelee na maisha yao.
Aidha katika maeneo ambayo yamebaki yalindwe kwa kuyawekea mipaka ya ardhi ili Mazingira hayo yawalinde wananchi, jambo ambalo limewafanya wananchi wote Wilayani hapa kufarahia maamuzi hayo na kumshukuru Mhe Rais.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Obed Katonge amemshukuru Mkuu huyo wa Wilaya kwa kuwakaribisha na kuwaruhusu kufanya shughuli za urasimishaji wa makazi.
Amemuhakikishia Mkuu huyo wa Wilaya kuwa watafanya kazi hiyo kwa umakini na kutaribu shughuli za kuandaa mipango ya uratibu kwa kushirikiana na Halmashauri nchini na taasisi za Serikali.
Pia kundaa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji, kanda, wilaya na taifa ili ardhi iweze kupimwa na kuwawezesha wananchi kumiliki ili iwaletee maendeleo ya uchumi.
“Tumekuja hapa Iramba ili kuweka mikakati ya kupanga na kupima ardhi ili kuhakikisha wananchi wanapata hati miliki.” Alisema Katonge
Naye Afisa Mipango miji toka katika tume hiyo, Abdallah Magombana amewaasa maafisa wanaohusika na mazingira kuhakikisha kuwa shughuli za uchimbaji wa madini hazileti athari kwa wananchi.
MWISHO
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda akipeana ufafanuzi na Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi toka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi Dodoma, Obed Katonge wakati walipotembelea ofisi ya Mkuu huyo wa Wilaya. Mbele yao ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Mhandisi Michiael Matomora. Picha na Hemedi Munga
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda akipokea ufafanuzi toka kwa Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi toka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi Dodoma, Obed Katonge wakati walipotembelea ofisi ya Mkuu huyo wa Wilaya. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.