Hemedi Munga Irambadc
Iramba. Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda amemuagiza Afisa Elimu Kata ya Kisiriri kuwaandikia barua Walimu wote wanaokaa nje ya kata hiyo wawe wamekwisha hamia katika vituo vyao vya kazi ifikapo Agasti 10, mwaka huu.
Mwenda ametoa agizo hilo leo Alhamisi Julai 29, 2021 wakati akiwa katika ziara yake ya kusikiliza kero na kuzitatua katika kata ya Kisiriri Wilayani hapa.
“Kuanzia leo hii nimeagiza Walimu wote waishi katika kata hii, ambaye hawezi kuishi hapa kijijini atuandikie barua kuwa kazi imemshinda, sisi tutatafuta walimu wengine maana kuna vijana wengi sana wanamaliza vyuo vikuu wanahitaji kazi mahali popote.” Ameagiza Mkuu huyo wa Wilaya
Katika hatua nyingine, Mwenda amewataka wananchi kukata kadi ya CHF ili wasitozwe tena fedha yoyote wanapokuwa wamekwenda hospitali, kituo cha Afya au Zahanati.
“Ndugu zangu wananchi hakuna utaratibu wa mtu anayekua na kadi ya CHF kutakiwa kutoa tena shilingi elfu kumi anapokwenda Zahanati au hospitali ya Wilaya.” Amesema Mwenda na kuongeza kuwa
“Tukubaliane kuwa wananchi hawa wakate kadi za CHF halafu waone faida ya kuwa na kadi ya CHF pale watakapoumwa wanapata dawa itawafanya wahamasishane wao kwa wao kukata kadi ya CHF na kila mmoja atakua na kadi kwa kuwa anahitaji huduma ya matibabu na anayapata.”
Aidha amepiga marufuku kuwapiga faini wakinamama ambao wanajifungulia nyumbani. Hata hivyo amewahamasisha akina mama hao kujifungulia Hospitali.
“Kutoza faini kwa mzazi aliyejifungulia nyumbani ni jambo ambalo limesitishwa, hivyo ninawatangazia rasmi kupitia mkutano huu kwamba tozo hizi zimesitishwa, hivyo mtu yoyote atakayeendelea kutoza mimi nitashughulika naye.” Amepiga marufuku Mkuu huyo wa Wilaya
Halikadhalika amewaomba wananchi hao kumpa ushirikiano.
“Ndugu zangu Wananchi! tukifanya kazi kwa ushirikiano tutapata maendeleo” Ameomba Mwenda
Hayo yote yamekuja baada ya wananchi hao kuibua kero mbalimbali mbele ya Mkuu huyo wa Wilaya ambapo alizitatua papo hapo.
Akijibu kero za Wananchi Afisa Ustawi wa Jamii kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Happines Alex amesema kuwa tayari Serikali ilikwisha leta fedha za dawa, hivyo dawa zipo katika vituo vyote na Hospitali.
Kwa upande wake mmoja wa Wananchi aliewasilisha kero yake mbele ya Mkuu huyo wa Wilaya, Pelepetuwa Makala amemshukuru Mkuu huyo wa Wilaya kwa kuja katika kata yao na kutatua kero zilizokuwa zikiwakabili hasa kwa upande wa afya na elimu.
“Napenda kumshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kutuhakikishia kuwa kero ya upatikanaji wa dawa sasa imekwisha na katika upande wa Walimu kuhakikisha wanakaa katika vituo vyao vya kazi.”
Naye muinjilisti wa kanisa la KKKT Kisiriri, Daudi Napegwa amesema kuwa ujio wa Mkuu huyo wa Wilaya umeleta hamasa, faraja na matumani mapya kwa wananchi kwa sababu kero ambazo walizokuwa nazo zimepata majibu stahiki toka kwa mkuu huyo wa Wilaya.
“Ninamshukuru sana mkuu wetu wa Wilaya kwa sababu ujio wake umefanya tuone suala la umeme, upatikanaji wa maji, walimu kukaa katika vituo vya kazi, upatikanaji wa dawa katika vituo vya afya na hospitali vimepata majibu stahiki.” Amesema Napegwa.
Mkuu wa Wilaya amefanya ziara kata ya kisiriri, Old Kiomboi, Kaselya, Ndulungu na akitarajiwa kufika katika kila kata zilizopo katika Wilaya hiyo.
MWISHO
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda akiwahutubia wananchi waliohudhuria mkutano uliofanyika kata ya Kisiriri leo Julai 29,2021. Alipofanya ziara katani hapo. Picha na Hemedi Munga
Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Happines Alex akiwatoa hofu wananchi juu ya masuala mbalimbali yanayohusu afya wilayani hapo. Picha na Hemedi Munga
Wananchi mbalimbali waliohudhuria mkutano wa Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda alipofanya ziara kata ya Kisiriri Wilayani hapo. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.