Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Kondakta wa basi la MJ Safari, Mohammed Hussein amefariki dunia kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata kwenye ajali iliyotokea kijiji cha kizonzo kata ya Shelui Wilayani Iramba Mkoa wa Singida.
Kifo hicho kimetokea kutokana na ajali iliyotokea leo Ijumaa Machi 27, 2020 ikihusisha Lori na Basi la abiria katika barabara kuu iendayo Mwanza toka Singida Wilayani Iramba.
Akitoa taarifa fupi mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula, Daktari Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Abel Mafuru amesema kuwa wamepokea majeruhi 11 ambao wamepatiwa matibabu na kuwa wanaendelea vizuri.
“ Tumepokea majeruhi ambapo Mohammed Hussein amefariki kutokana na majera aliyoyapata yaliosababisha kutoka damu nyingi,” amesema Mafuru na kuongeza
“ Majeruhi wanne tunawapeleka Hospitali ya Mkoa wa Singida kwa ajili ya matibabu zaidi kutokana na namna walivyoumia.”
Majeruhi ambao wamepatiwa rufaa kwenda Hospitali ya Mkoa wa Singida ni Mohammed Salehe (45), Ramadhani Said (44), Hassan Iddi na Hoja Nkindikwa(24).
Mafuru amewataja majeruhi ambao wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya hiyo kuwa ni Said Ally (45), Zakaria Mdundu (50), Amina Nkimiye(53) na dada yake, Sara na mtoto wake ambaye hakupata majeraha yoyote.
Mkuu wa Wilaya hiyo amewapongeza madaktari na manesi kwa namna walivyotoa huduma kwa majeruhi hao huku akiwapa pole na kuwatakia majeruhi hao kupona haraka.
Aidha Mkuu huyo ametembelea eneo ambalo ajali ilitokea na kuwataka wananchi kudumisha usalama na kuendelea kuliombea eneo hilo kwa kuwa kumekua na ajali za mara kwa mara.
Halikadhalika, amewakumbusha kuendelea kufuata maelekezo ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya korona.
Kwa upande wake Mkuu wa Kituo cha Polisi Tarafa ya Shelui, Afande Haule amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo nakwamba chanzo cha ajali ni dereva wa lori lenye usajili namba T939 CBW alipokuwa analipita gari dogo (overtaking) na kugongana uso kwa uso na basi la MJ Safari lenye usajili namba T779 AWJ.
Lori hilo lililokuwa limebeba ngano likitoka Dar es Salaam kwenda Nchini Rwanda likapinduka huku basi hilo lililokuwa likitokea Geita kwenda Dar es Salaa likiharibika vibaya.
Naye mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo,Nkende Ndimalala mkazi wa Kizonzo ameiomba Serikali kuweka bamzi (matuta) eneo hilo kwa kuwa gari zimekuwa zikipita kasi sana, hivyo kusababisha ajali za mara kwa mara.
MWISHO
Lori likiwa limeanguka baada ya kugongana uso kwa uso na basi la MJ Safairi kijiji cha Kizonzo Tarafa ya Shelui Wilayani Iramba. Picha na Hemedi Munga
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula akiwajulia hali majehuri waliolazwa Hospitali ya Kiomboi Wilaya ya Iramba. Picha na Hemedi Munga
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Mwl. Linno P. Mwageni akiwajulia hali majehuri waliolazwa Hospitali ya Kiomboi Wilaya ya Iramba. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.