Na Hemedi Munga
Singida - Iramba. Mkuu wa wilaya ya Iramba mkoani Singida, Suleiman Mwenda amesema kuwa hakuna kama Rais Samia kwa namna ambavyo ametakeleza miradi ya maendeleo ya zaidi ya takribani Tsh 90 bilioni katika Tarafa ya Ndago ndani ya mwaka mmoja wa utawala wake.
Mwenda ameeleza mafanikio hayo leo Jumatatu Machi 28, 2022 punde baada ya kukagua miradi ya maendeleo katika kata sita za Tarafa ya Ndago wilayani hapa akiwa na kamati ya siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na kamati ya Usalama wilaya.
Ni wajibu wetu kuwaeleza wananchi kuwa serikali yenu imefanya nini ndani ya mwaka mmoja wa Rais Samia kwa sababu nyie ndio mliiweka serikali hii madarakani.
Akizungumzia sekta ya elimu msingi na sekondari, Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa serikali ndani ya mwaka mmoja imejenga madarasa, mabweni, maabara na samani nyinginezo ambapo jumla ya takribani Tsh 782.6 milioni zimetumika.
Katika kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma sahihi za afya na kwa wakati serikali ya Rais Samia ndani ya mwaka mmoja imejenga vituo vya afya katika kata ya Kisiriri, Mtoa, Mwanduigembe, Urughu na Kidaru ambapo kila kimoja kimepata takribani 500 milioni.
Pia, katika kila kituo cha afya na zahanati kuna ujenzi wa matundu ya vyoo bora unaendelea ukiwa na thamani ya takribani Tsh 98.8 milioni huku Tsh 100 milioni nyingine zikijenga Zahanati katika kijiji cha Misuna na Kaselya.
Kutimiza azma ya serikali kumtua mama ndoo ya maji kichwani na kutatua migogoro inayosababishwa na akinamama kuchukua muda mrefu katika kutafuta maji serikali ya Rais Samia ndani ya mwaka mmoja akiwa madarakani imeleta takribani Tsh 1.1 bilioni ambapo miradi hiyo ipo katika hatua za mwisho, hivyo ni dhahiri kuwa sasa wananchi wataweza kuvuta maji katika nyumba zao.
“Hawa akinamama kubeba ndoo ya maji kichwani watasahau kabisa kwa sababu maji yatakuwa yanapatikana katika nyumba zao.” Alisistiza
Aidha, aliongeza kuwa sasa hivi mwanamke akiolewa ataendelea kungaa kwa sababu maji yatakuwa yanapatikana ndani.
Akiongelea kuhusu miundombinu ya mawasiliano, Mwenda alisema kuwa katika mwaka huu mmoja wa Rais Samia aliishaleta zaidi ya Tsh 80 bilioni kwa ajili ya kujenga barabara kwa kiwango cha lami inayoanzia Kizaga, Mukulu, Ndago, Mbelekese, Sepuka hadi Singida mjini.
“Tunataka maendeleo kwa ajili ya watu wote, hivyo niwahakikishie kuwa hakuna atakayedhulumiwa wala kuvunjiwa nyumba kabla ya kupata fidia yake, kila mmoja atapata haki yake.” Alisema
Aidha, aliongeza ipo barabara ya kutoka Kata ya Mbelekese, Misuna kuelekea Tumuli barabara kuu itokayo Singida mjini kuelekea Jijini mwanza imetengewa takribani Tsh 109 milioni na ujenzi unaendelea.
Halikadhalika, kuna ujenzi wa karavati kubwa sana katika barabara ya Malango ambapo takribani Tsh 200 milioni zinajenga ili kuhakikisha watu wakati wa masika wanapita katika karavati hilo na kuendelea na shughuli zao za kiuchumi.
Yapo matengenezo ya barabara kutoka Urughu kupitia Mangole mpaka Mpugizi kilometa 9.5 kwa takribani Tsh 765 milioni huku barabara ya kutoka Mtekente kupitia Msansao hadi kijiji cha Ujungu yenye urefu wa kilometa 11.7 kwa gharama ya Tsh 999 milioni Mkandarasi anaendelea kujenga barabara hiyo.
Pia, ujenzi wa barabara ya kutoka Kibaya kupitia kijiji cha Luzilukulu hadi Kipuma yenye urefu wa kilometa 15 yenye kugharimu fedha za kitanzania Tsh 624 milioni unaendelea, hivyo hakuna kama Rais Samia.
Fedha zote hizi ni kwa tarafa ya Ndago ambayo ni kati ya tarafa zinazopatikana ndani ya Wilaya ya Iramba.
Kwa upande wake mmoja wa washiriki wa mkutano huo, Jasmini Hamisi alimshukuru Rais Samia kwa kumtua mama ndoo ya maji kichwani, hivyo wameahidi kuendelea kumuombea afya njema ili aendelee kuliongoza Taifa hili kwa weledi na manufaa makubwa.
Jasmini alisema kuwa hatua yakupatikana maji katika maeneo yao imesababisha kutokuwepo ugovi kati yao na waume zao kwani maji sasa yanatoka katika nyumba zao ukilinganisha na zamani ambapo walilazimika kutembea umbali mrefu na kukaa muda mrefu.
Naye Pili Shabani alisema kuwa anampenda sana Rais Samia nakumuomba aendelee kuwaletea miradi mingi ili wanawake waendelee kunufaika na jamii kwa ujumla.
MWISHO
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.