Na Hemedi Munga
Singida - Iramba. MKUU wa wilaya ya Iramba mkoani Singida, Suleiman Mwenda aitisha kongamano la wadau wa madini ya dhahabu, almasi na zilkoni ili kupata wawekezaji wa uchimbaji mkubwa wenye tija kwa wananchi wa Iramba.
Mwenda ametoa wito huo leo Alhamisi Novemba 18, 2021 wakati akiongea na wamiliki mbalimbali wa leseni za kuchimba madini katika kijiji cha Nselembwe Tarafa ya Shelui wilayani hapa.
“Ndugu zangu! nitajihisi kuwa nimefanikiwa ikiwa nitaifanya wilaya hii kuwa katika kumi bora zinazozalisha madini kwa wingi nchini.” Alisema Mkuu huyo wa wilaya na kuongeza kuwa
“Wilaya yetu ya Iramba imebarikiwa rasilimali ya madini mengi takribani kata 14 kati ya 20 zote zinamadini, huku baadhi ya maeneo yakiwa namafuta.”
Alisema kuwa ipo haja ya kutafuta wawekezaji wenye teknolojia kubwa ambazo zinauhakika wa kupata madini kwa sababu madini katika ardhi hii yapo.
Halikadhalika aliongeza kuwa katika hatua za awali zimejitokeza kampuni tatu ambapo moja inatoka Uturuki na mbili zinatoka China kwa ajili ya kuja kuchimba madini kwa kushirikiana na wenye leseni.
Kupatikana wawekezaji hawa na wakafanikiwa kuanza uzalishaji, ni hakika Halmashauri hii itaongeza uwezo wa kukusanya mapato yake ya ndani.
“Ni imani yangu kuwa ukipata mwekezaji mkubwa mwenye kutumia vifaa vya kisasa vya kuvuta maji na kuchimba lazima atapata dhahabu, almasi na zilkoni kwa sababu madini haya yapo.”
Kwa upande wake kaimu Afisa Madini Mkazi Mkoani Singida, Chone Malembo amesema kuwa kongamano hilo litashirikisha makampuni makubwa ikiwemo makampuni ya GGM, SHANTA, BARIKI na TWIGA.
“Ndugu zangu sio kweli kwamba wakati wajerumani wakichimba madini hapa Sekenke walimaliza madini yote, hivyo tuyakaribishe makampuni makubwa yashiriki ili tuyaoneshe fursa tulizonazo ili waone namna gani wanaweza kushirikiana na sisi.”
Hali hii itaitangaza Wilaya ya Iramba katika sekta ya uchimbaji wa madini ambapo kimkoa Iramba inaongaza kwa uzalishaji ukilinganisha na wilaya zote saba za Mkoa wa Singida.
“Tunataka tuzitangaze hizo fursa kwa kuwakutanisha wachimbaji wadogo na makampuni makubwa ili tuvutie uwekezaji na kuinuwa uchimbaji.” Aliongeza
Pia amepiga marufuku tabia ya wachimbaji wa almasi eneo la Luzilukulu Wilayani hapa ambapo baada ya kupata madini hayo wanakwenda kuyauza Mkoani Shinyanga.
Akiongea katika mkutano huo mjiolojisti, Yuda Tadei amesema kuwa makongamano yamekuwa yakitumika katika mikoa na wilaya za jirani na kuzifanya kujulikana kwa wawekezaji.
Tadae ilifafanuwa kuwa maeneo ya Geita, Kahama, Chunya na sehemu nyinginezo walitumia makongamano hayo kutoa data za upatikanaji wa madini na hivyo kuwafanya wawekezaji kujuwa kuwa wakiwekeza kwako watapata faida.
“Niwaombe ndugu zangu tushirikiane na Mkuu huyu wa Wilaya kuitangaza Wilaya yetu kwa madini haya yaliopo yanotasha kuifanya Iramba kuwa ya mfano nchini.”
Kwa upande wake mdau wa kuchimba madini eneo la Kenkangombe wilayani hapa, Salumu Kigalula amesema kuwa wazo alilolileta Mkuu huyo wa wilaya linafaida kubwa kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla.
“Kwa kweli tunashukuru kwa kupata Mkuu wa wilaya ambaye amekuwa na mawazo ya uchumi, hivyo siye tunakuunga mkono katika kulitekeleza hili” alisema Kigalula
Naye Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye ni mchimbaji wa madini eneo la Mbuyuni , Alex Odepo amesema kuwa ni kweli wamechoka kutumia nyundo katika uchimbaji nakutamani vyombo hivyo vya kisasa katika uchimbaji ili waweze kuyapata madini hayo na kuepukana na uchimbaji wa kubahatisha.
MWISHO
Baadhi ya wadau wa kuchimba madini wakiwa katika kijiji cha Nselembwe tarafa ya Shelui wilaya ya Iramba mkoani Singida wakifuatilia kwa kina maono ya Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda kuifanya Iramba kuingia kumi bora kuzalisha kwa wingi madini ya dhahabu, almasi na zilkoni. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.