MWENGE WA UHURU WALETA NEEMA SINGIDA, DKT. MWIGULU NCHEMBA ATOA WITO WA UMOJA NA KUIUNGA MKONO SERIKALI
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndg. Ismail Ally Ussi, amempongeza Waziri wa Fedha na Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), kwa usimamizi madhubuti wa utoaji wa fedha katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Singida na nchini kote.
Akizungumza wakati wa ukaguzi na uwekaji wa jiwe la msingi kwenye ujenzi wa daraja la Konkilangi pamoja na barabara ya changalawe yenye urefu wa kilomita 1.5 katika Wilaya ya Iramba, Ndg. Ussi alisema:
“Kufuatia usimamizi mzuri wa fedha za maendeleo zinazotolewa na Serikali, tumeona matokeo chanya hususani katika miradi ya miundombinu, maji, afya, elimu, umeme na huduma nyingine muhimu zinazokuza ustawi wa jamii kiuchumi. Hongera sana Dkt. Nchemba kwa kazi kubwa unayoifanya ya kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki.”
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), alisisitiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha huduma muhimu zinawafikia wananchi kote nchini kwa mujibu wa Ilani ya CCM 2020–2025.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonyesha uongozi thabiti katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi kwa kuboresha mazingira ya huduma za kijamii na kiuchumi kwa manufaa ya Taifa,” alisema Dkt. Nchemba.
Aidha, Dkt. Nchemba alitoa wito kwa wananchi kuendelea kuiunga mkono Serikali katika jitihada zake za kuwaletea maendeleo na akalaani vikali vitendo vya uchochezi vinavyolenga kuvuruga umoja wa kitaifa.
Katika mbio hizo wilayani Iramba, Mwenge wa Uhuru ulikagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi saba ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 7.8, ikiwa ni ishara ya mafanikio ya juhudi za Serikali kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.