Mkuu wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida Mh. Emmanuel Luhahula, amepokea Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2018 leo 12/08/2018 kwa shangwe, furaha, nderemo na vifijo katika kijiji cha Mugungia, Kata ya Kaselya ukitokea Manispaa ya Singida na umekimbizwa km 146.9 katika vijiji 18, kata 7, tarafa 3 na umepitia miradi 6 iliyogawanyika katika sekta za Maji, Miundombinu, Uwekezaji, Elimu, Afya, Kilimo na ufugaji. Miradi 2 imezinduliwa ambayo ni mradi wa maji Mgungia na Kituo cha mafuta Old Kiomboi. Vilevile Mwenge wa Uhuru umefungua bweni 1 la wanafunzi shule ya Sekondari Lulumba na kuweka jiwe la msingi katika miradi 2 ambayo ni barabara Makunda-Kyengege na ujenzi wa kituo cha afya Kinampanda. Mwege wa Uhuru umeona, umetembelea na kukagua Bwawa la samaki na kilimo cha mbogamboga Gereza la Kiomboi
Aidha, Mwenge wa Uhuru umetembelea na kuona shughuli 3 za maendeleo ambazo ni mapambano dhidi ya dawa ya kulevya Misigiri, mapambano dhidi ya malaria Zahanati ya Kijiji cha Uwanza na mapambano dhidi ya UKIMWI eneo la mkesha Kinampanda. Vilevile Mwenge wa uhuru umezindua Klabu ya wapinga Rushwa shule ya Sekondari Mbelekese.
Miradi yote iliyopitiwa na Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 ina thamani ya Tshs. 1,621,903,714/= wachangiaji wakiwa jamii (nguvukazi) Tshs. 193,247,031, Serikali Kuu Tshs. 684,118,796/=, Halmashauri ya Wilaya Tshs. 15,235,600/= na Wahisani Tshs. 729,302,287/=.
Mwandisi Charles F. Kabeho amepongeza juhudi za Mkuu wa wilaya ya Iramba kwa kushirikiana na watendaji pamoja na wananchi wa wilaya ya Iramba kwa utendaji kazi nzuri, Wajibu wa kila mmoja katika kutimiza majukumu yake kikamilifu kwa kutekeleza miradi ya Maendeleo na kuwaletea maendeleo wananchi wa Wilaya ya Iramba
Kiongozi wa Mbio za Mwenge uhuru kitaifa mwaka 2018 Mwandisi Charles F. Mabeho akizungumza na wananchi wa Iramba amesema uzinduzi wa mbio za mwenge wa uhuru 2018 ulianzia mkoani Geita April 2 mwaka huu na kilele ni siku ya kumbukumbu ya mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Oktoba 10, 2018 mwaka huu huko Mkoani Tanga. a
kwa miradi ambayo tumekagua katika siku hii ya leo, kwa kweli miradi yenu ilikuwa ni mizuri. Kwa asilimia kubwa jinsi mlivyoweza kufanya kazi naamini mpaka kufikia hapo watu wamefanya kazi na kutimiza wajibu wao vizuri, sijaweza kuona dosari kwa miradi yote ambayo tumeweza kuikagua kwa wilaya hii ya Iramba.” Alisema Mwandisi Kabeho.
Ndg. Dominic M. Njunwa, akiongea kwa niamba ya Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa mwaka 2018 alisema, kwa mwaka 2018 chini ya uongozi mzuri wa Mweshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Ujumbe mahususi wa mbio za mwenge wa uhuru umejikita katika sekta ya Elimu.
Aidha ameongeza kwa kusema Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 umebeba ujumbe muhimu kwa mustakabali wa elimu katika Taifa letu usemao “ELIMU NI UFUNGUO WA MAISHA, WEKEZA SASA”. Ujumbe huu unaambatana na ujumbe wa kudumu wa mapambano dhidi ya UKIMWI chini ya kaulimbiu; “Mwananchi Jitambue: Pima afya yako sasa”, Mapambano dhidi ya Malaria chini ya kaulimbiu; “Shiriki kutokomeza Malaria kwa manufaa ya jamii” Mapambano dhidi ya dawa za kulevya chini ya kaulimbiu; “Tuwasikilize na kuwashauri watoto ili wasitumie dawa za kulevya”, na Mapambano dhidi ya Rushwa chini ya kaulimbiu “Kataa Rushwa-Jenga Tanzania”. Alisema Ndg. Dominic.
Ameongeza kwa kusema kuna mafanikio makubwa ya serikali katika sekta ya Elimu kuhakikisha vijana wakitanzania wanapata Elimu pasipo kuwa na kero hasa upande wa michango. Serikali ya awamu ya tano imehakikisha Vijana wote wenye umri wa kwenda shule wanaandikishwa ili wapate fursa ya Elimu. Pamekuwepo ongezeko kubwa sana la wanafunzi, kwa wanafunzi wa awali ongezeko likiwa ni Zaidi ya 1,600,000 kutoka wanafunzi 1,300,000 mwaka 2015, huku kwa upande wa wanafunzi wanaohitimu darasa la Saba na kujiunga na masomo ya sekondari ongezeko likiwa ni wanafunzi Laki 5 kutoka wanafunzi Laki 3.
Vile vile katika uwekezaji wa serikali katika masomo ya Sayansi kama vile Fizikia, Kemia na Baiolojia kwa kuhakikisha kunakuwapo na mazingiira mazuri kwa ajili ya usomaji wa masomo hayo. Serikali imesambaza vifaa vya masomo ya sayansi kwa shule zipatazo 1,625 za Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania ambazo hazikuwa na vifaa hivyo vya masomo ya Sayansi na Hisabati na kuzisaidia shule hizo na wanafunzi kufanya mitihani yao ya masomo ya Sayansi kwa vitendo na si tena kwa Nadharia na kuongezeka kwa ufaulu wa masomo ya sayansi kwa shule nyingi za Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania.
Mwenge wa Uhuru ni chombo/Tunu pekee ya Taifa iliyo asisiwa na rais wa kwanza Mwl.Julius Kambarage Nyerere 1961, ikiwa ni ishara ya kuwepo kwa Taifa uhuru la Tanganyika.
Mara baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, mwaka 1964, Tanganyika iliungana na Zanzibar na kupata Taifa moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliuwasha Mwenge wa Uhuru na akamkabidhi Luteni Alexander Ngwebe Nyirenda na kikosi cha Vijana wenzake wakaupeleka Mwenge wa Uhuru juu ya Mlima Kilimanjaro.
Luteni Alexander Nyirenda alipandisha Bendera na Mwenge wa uhuru juu ya mlima Kilimanjaro usiku wa kuamkia tarehe 9 Desemba mwaka 1961 ambapo baada ya Uhuru wa Tanganyika na kuwashwa kwa Mwenge wa Uhuru, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na viongozi wenzake wa awamu ya kwanza walielekeza juhudi zao katika kuwaunganisha Watanzania na kuweka misingi imara ya kulijenga taifa huru la Tanganyika; kudumisha amani, upendo, umoja, mshikamano na kuweka sera za kukabili maadui ujinga, umaskini na maradhi.
Baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa mwaka 1964, Mwenge wa Uhuru uliendelezwa kuukimbiza katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kujenga na kuimairisha misingi ya amani, umoja, uzalendo, upendo, mshikamano na kuhamasisha shughuli za maendeleo katika jamii zetu na kupeleka kwa Watanzania wote ujumbe maalum uliokusudiwa na Serikali kila mwaka.
Mkuu wa wilaya ya Iramba mkoani Singida Mhe. Emmanuel Luhahula akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhe. Paskasi Muragili leo Agosti 12, 2018 katika Kijiji cha Mgungia kata ya Kaselya kwa ajili ya kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeo katika wilaya ya Iramba.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.