Na Hemedi Munga
tehama@irambadc.go.tz
Singida - Iramba. Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba mkoani Singida, Innosent Msengi amemuagiza meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) kuhakikisha Mji wa kiomboi unapata barabara za lami.
Msengi ametoa agizo hilo leo Januari 7, 2022 katika Baraza la Madiwani wakati wakupitisha rasimu ya bajeti ya matengenezo ya barabara kwa mwaka wa fedha 2022/2023 lililofanyika katika ukumbi mdogo wa Halmashauri hiyo mjini hapa.
“Nikuombe Meneja wa TARURA utusaidie tupate barabara za lami katika mji wetu wa Kiomboi na hiyo itakuwa ni heshima kwa wilaya hii kwa sababu wilaya hii ni kongwe ukilinganisha na wilaya nyingine Tanzania.” Alisema Msengi na kuongeza kuwa
“ Kwa kweli tunamshukuru sana Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kushauri kuwa bajeti ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) kuwa inajadiliwa na Madiwani kwa sababu wao ndio wawakilishi wa wananchi ili wananchi wapate kufahamu yanayopangwa kuhusu barabara za maeneo yao.”
Akiongea katika Baraza hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Mhandisi Michael Matomora alisema kuwa kupita kwa bajeti hiyo kwa Madiwani itasaidia wananchi kuifahamu bajeti ya barabara na kujuwa kuwa ni nini serikali inataka kufanya katika kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuhusu barabara.
Awali akiwasilisha taarifa ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) katika Baraza la Madiwani, Meneja wa TARURA Evance Kibona alisema kuwa rasimu ya bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 imeandaliwa kwa kuzingatia miongozo ya matengenezo ya barabara na mpango wa kitaifa wa miaka minne wa ujenzi na matengenezo ya barabara wa TARURA.
Kibona alifafanua kuwa wilaya ya Iramba inaomba kutengewa takriban Tsh 14.9 bilioni kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ukilinganisha na Tsh 7.1 bilioni ambazo zilitengwa kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya matengenezo ya barabara na ujenzi wa vivuko.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Mbelekese Wilayani hapa, Omari Shabani alisema kuwa wamefurahishwa sana na namna ambavyo Rais Samia amewaletea fedha nyingi kwa ajili ya miradi mbalimbali.
“Kwa kweli tunampongeza sana Rais Samia kwa kutuletea fedha nyingi kupitia TARURA ambazo zitaibadilisha wilaya ya Iramba.” Alisema Shabani na kuongeza kuwa
“Sisi kama madiwani tutashirikiana na TARURA kuhakikisha fedha zilizotolewa zinatengeneza barabara kwa kiwango kinachotakiwa.”
Naye Diwani wa kata ya Shelui Wilayani hapa, Agness Amos alisema kuwa wako tayari kusimamia utekelezaji wa bajeti hii, hivyo wanaiomba TARURA kuhakikisha wanasimamia ipasavyo kutengeneza barabara kwa kiwango kinachokidhi thamani ya fedha zilizotolewa.
Wilaya ya Iramba ina mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 743.55 ambapo kilomita 286.69 ni barabara za wilaya, kilomita 454.38 ni barabara za malisho na kilomita 2.48 ni barabara za jamii.
Mtandao huo una kilomita 1.5 barabara za lami, kilomita 1.5 barabara za zege, na kilomita 224.36 barabara za changarawe.
MWISHO
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.