Na Hemedi Munga
tehama@irambadc.go.tz
Singida - Iramba. Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Iramba mkoani Singida, Samwel Joel amewaagiza viongozi wote wa wilaya hiyo kuwa karibu na miradi ambayo inatekelezwa ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na ubora unaotakiwa.
Joel ametoa agizo hilo leo Ijumaa Desemba 24, 2021 wakati akiwa katika ziara ya Kamati ya Siasa ya wilaya hiyo punde baada ya kutembelea na kukagua mradi wa karavati linalojengwa katika barabara ya Songambele – Misuna kata ya Ndago wilayani hapa.
“Kwa kweli ninaendelea kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan. Ni fedha nyingi ametuletea Iramba, hivyo niwaombe viongozi wenzangu kuwa karibu na miradi hii ili itekelezwe kwa wakati na thamani yake iweze kuonekana. Tunahitaji kuona thamani ya fedha ya mradi huu.” Aliagiza Joel
Alibainisha kuwa eneo hilo kuwa na karavati litasaidia mbuga hiyo iweze kupitisha mazao ya dengu kwa urahisi na hivyo kuweza kuwanufaisha wananchi kiuchumi.
“Niwaombe watekelezaji wa mradi huu, kuukamilisha kwa wakati ili kutimiza azma ya Serikali inayoakisi matakwa ya jamii.” Alisema
Akiongea katika ziara hiyo Mkuu wa wilaya hiyo ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya, Suleiman Mwenda amemuahidi Mwenyekiti wa Kamati hiyo kuwa maagizo yote aliyotoa Serikali itayatekeleza kwa wakati na kiwango bora ili kutimiza azma ya Serikali kuihudumia jamii kwa kurahisisha mawasiliano.
Awali akiwasilisha taarifa fupi mbele ya Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa Meneja wa TARURA wilayani hapa, Evance Kibona alisema kuwa Serikali inatekeleza mradi wa karavati lenye urefu wa mita 16.6 na upana wa mita 8.8 huku likiwa na milango mitatu lenye jumla ya gharama ya Tsh 201.9 milioni.
Kibona alisema kuwa ujenzi wa mradi huu ulianza Oktoba 6, 2021 ambapo kwa sasa ujenzi umefikia asilimia 67 na kutarajia kukamilika mapema ifikapo Aprili 5, 2022.
Aidha alifafanua kuwa ujenzi ukikamilika utachangia wanacnhi kupita katika barabara hiyo hata wakati wa mvua na hivyo kuendelea na shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa kijiji cha Usure, Songambele, Misuna na Mbelekese.
Kwa upande wake Diwani wa Kata hiyo, Ernest Kadeghe alisema kuwa wananchi wa kata hii wanamshukuru sana Mhe Rais kwa kuleta mradi huu ambao unafungua mawasiliano wakati wote.
“Kwa kweli wananchi wameitikia na kuunga jitihada zote kila zinapohitajika katika mradi huu na mingineyo.” Alisema Kadeghe
Naye mmoja wa vibarua wanaojenga karavati hilo, Ashrafu Rashidi aliwaasa vijana wenzake kuacha tabia ya kuchagua kazi badala yake kila ajira za muda na za kudumu zinapopatikana kuendelea kupambana ili maisha yaende.
Pia alimshukuru sana Mhe Rais kwa kuleta fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ambayo imesababisha vijana wanajipatia ajira na kuepukana na tabia za udokozi na kujiingiza katika madawa ya kulevya.
MWISHO
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.