Na Hemedi Munga
tehama@irambadc.go.tz
Singida - Iramba. Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Iramba mkoani Singida, Samwel Joel amewataka wauzaji wa mafuta ya alizeti kando mwa barabara kuu toka Singida kuelekea jijini Mwanza kuwa waaminifu katika biashara hiyo.
Joel ametoa wito huo mwishoni mwa juma hili wakati akiongea na kikundi cha vijana kilichopata mkopo takriabani milioni 8 toka Halmashauri ya Wilaya ya Iramba kupitia mapato ya ndani na kujishughulisha na kuuza mafuta ya alizeti kando kando mwa barabara kuu eneo la Shelui wilayani hapa.
“Niwaombe ndugu zangu nyinyi kama kikundi msifanye udanganyifu katika biashara kwa sababu kufanya hivyo kunauwa biashara.” Alisema Joel na kuongeza kuwa
“Nivizuri nyinyi mjaze kipimo kilicho sawa na kuuza kwa bei yenye maslahi kwa kuzingatia ujazo wa lita 5 bei yake na lita 4 kuwa na bei yake.”
Aidha amekipongeza kikundi hicho cha vijana kwa ubunifu wa kutumia fursa za mikopo inayotolewa na Halmashauri hiyo,
Alieleza kuwa uthubutu huo utawasaidia vijana hawa na wanaowazunguka waweze kujikwamuwa kimaisha.
“Endeleeni kujituma na kuzingatia uaminifu kwa sababu biashara yoyote inajengwa na uaminifu. Hivyo muwe waaminifu sana, msifanye udanganyifu hata kidogo na hata kama mafuta yataadimika jitahidini muwe wakweli” Alisisitiza
Akiunga juhudi za kikundi hicho cha vijana Mkuu wa Wilaya hiyo, Suleiman Mwenda amekiahidi kikundi hicho kukipatia tofali 200 ili kujenga ofisi kwa lengo la kuendeleza biashara zao kisasa.
“Kwa namna ya kipekee niwapongeze maana ni vikundi vichache ambavyo Serikali inapokuwa imetoa fedha ukaona matokeo kwa kutoa marejesho yake kwa wakati namna ilivyopangwa. Alisema Mwenda
Pia amevisifu vikundi vya akina mama kwa kuwa waaminifu na pale wanapokuwa wamepatiwa fedha wanaitumia kwa namna ambavyo walivyoomba na kuwa na tabia ya kurejesha makato kwa wakati ukilinganisha na vikundi vya vijana wakiume.
Akiongea na kikundi cha vijana hao Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Innocent Msengi aliwaahidi kuwa ikiwa watakuwa wanarejesha makato yao kwa wakati endapo wataomba tena watapanuliwa wigo wa kuongeza kiwango cha fedha ili wafanye biashara yao kwa kuzingatia malengo yao.
Awali akiwasilisha taarifa fupi ya kikundi cha Jitume Grupu mbele ya Kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo, Neema Shalua alisema kuwa kikundi kimekuwa na mafanikio yakupata mkopo usio na riba takribani Tsh 8.6 milioni.
Kufuatia hali hiyo kikundi hicho kimemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuhimiza Halmashauri kutoa mikopo hiyo kwa sababu kupitia mikopo hiyo imewezesha kuinua kipato cha mwanachama mmoja mmoja ndani ya kikundi chao.
Kwa upande wake katibu wa Chama cha Mapinduzi, Mwal. Ephraim Kolimba aliwaasa vijana hao kuwa na ofisi inayotambulika.
“Naomba mtambue vijana kuwa fedha hizi mnazokopeshwa ni za Serikali, hivyo mnapokuwa na ofisi inayotambulika mnaweza pata hata viongozi wakanunua kwenu ambapo itakuwa ni sehemu ya fedha ya Serikali.” Alisema Komredi Kolimba
Naye Mwenyekiti wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi, Joseph Mnemba alimuomba Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo kutoa kipaombele kila fursa ya fedha inapokuwa imepatikana kwa vikundi ambavyo vinajituma katika shughuli za ujasiriamali.
Kikundi cha Jitume Grupu kina jumla ya Wanachama 10 na kinajishughulisha na uuzaji wa mafuta kando mwa barabara kuu itokayo Singida kuelekea jiji la Mwanza.
MWISHO
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.