Na Hemedi Munga
tehama@irambadc.go.tz
Singida - Iramba. Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Lemomo Kiruswa amempa wiki moja Mkuu wa wilaya ya Iramba mkoani Singida Suleiman Mwenda kwa kushirikiana na Kaimu Afisa Madini mkoa wa Singida kutatua mgogoro wa duara namba 22 kati ya wanaodaiwa kuwa wawekezaji na wanachama wa duara hilo.
Dkt. Kiruswa ametoa agizo hilo leo Jumanne Januari 18, 2022 wakati alipofanya ziara ya kujitambulisha na kusikiliza kero katika kijiji cha Nkonkilangi wilayani hapa.
“Ninakuagiza Mkuu wa wilaya kwa kushirikiana na Kaimu Afisa Madini Singida kutatua mgogoro huu na ifikapo tarehe 30 januari tupate taarifa kuwa hapa hakuna mgogoro.” Aliagiza Naibu waziri huyo na kuongeza kuwa
“Kati ya vitu ambavyo hatuitaji kuviona katika hii sekta ni migogoro tunahitaji kuielea hii sekta kwa kuhakikisha hakuna migogoro ili wachimbaji wanufaike na ikitokea kuna mgogoro sumbufu unaosababisha wachimbaji kutopata rasilimali hii tutaifuta hiyo leseni.”
Amewahakikishia wachimbaji hao kuwa serikali inahitaji kuona kuwa kila mmoja anapata haki yake na katu serikali haitaji kuona wachimbaji wanagombana.
Akiongelea kuhusu maombi ya namna bora kuwasaidia kutoa maji yanayodaiwa kuwa ni kero kubwa inayosababisha wachimbaji kutumia gharama kubwa na kutopata manufaa kwa sababu ya maji, alisema kuwa wanahitaji kuainisha mahitaji yote ya vifaa hivyo na kuviweka katika mkakati wa serikali kwa ajili ya kuvipata ili kusaidia kutatua changamoto hiyo.
Halikadhalika, amewaahidi wachimbaji hao kutuma timu ya wataalamu kutoka wizarani itakayowasaidia wachimbaji kubaini miamba sahihi ya kuchimba ili kupata madini kwa wepesi.
Akiongea katika eneo hilo la mgodi mkuu wa wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda alisema kuwa wachimbaji wadogo hao katika mwaka wa fedha 2020/2021 wemeweza kuuza gramu 319,000 katika soko la madini Shelui na kuweza kuingizia serikali kiasi cha Tsh 37 bilioni.
Aidha ametumia nafasi hiyo kumuomba Naibu waziri huyo kuwasaidia wachimbaji hao kupata vifaa vitakavyowasaidia kuondoa maji ili waweze kuchimba dhahabu kwa njia nyepesi.
Akijibu hoja za wachimbaji Kaimu Afisa madini mkoa wa Singida, Chone Malembo amewataka wachimbaji hao, kero walizonazo wakae kuzizungumzia ili wazitatue kwa sababu hakuna kinachoshindikana katika mazungumzo.
Malembo alibainisha sifa za kupata leseni kwa mujibu wa kifungu cha nane cha sheria ya madini kuwa ni mtua kuwa mtanzania mwenye umri usiokuwa chini ya miaka 18, hajawahi kushitakiwa na kutangazwa na mahakama kama aliyekosa, tini namba, picha mbili za paspoti na kitambulisho aidha cha udereva, kura au cha taifa.
Kwa upande wake mmoja wa wachimbaji katika duara hilo namba 22, Zahara Abdilahi alisema kuwa kwa nini wao kama viongozi wa Ushirika wa Ukombozi hawachukui asilimia ya ofisi, hivyo anaomba leo hilo lipatiwe ufumbuzi.
Naye Samora Omari anayedaiwa kuwa mwekezaji wa duara namba 22 kuhoji kuwa ninani anastahiki kuwa na leseni ya kuchimba madini kwa kuzingatia sheria za nchi ya Tanzania.
MWISHO
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.