Na hemedi Munga
tehama@irambadc.go.tz
Singida - Iramba. Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Lemomo Kiruswa amemuagiza Mwekezaji wa kampuni ya Sunshine inayojishughulisha na kuchimba madini ya dhahabu katika kijiji cha Nkonkilangi wilayani Iramba mkoa wa Singida kuhakikisha anatoa ajira kwa wanawake.
Dkt Kiruswa ametoa agizo hilo leo Jumanne Januari 18, 2022 wakati alipofanya ziara katika kampuni hiyo inayochimba madini ya dhahabu katika kijiji cha Nkonkilangi wilayani hapa.
“Sisi serikali tutaendelea kukusaidia kuweka mazingira rafiki, hivyo hakikisha jamii inayokuzunguka inafurahi.” Alisema Naibu Waziri huyo na kuongeza kuwa
“Waajiri vijana wa hapa na hasa wanawake wanapohitajia ajira wape ajira kwa sababu wanaouwezo wa kufanya kazi.”
Jambo la wawekezaji kutoa ajira kwa jamii inayowazunguka linaifurahisha serikali.
Aidha amewahakikishia wawekezaji katika sekta ya madini kote nchini kuwa serikali imeweka mazingira rafiki yenye amani, usalama kwa kuzingatia taratibu, sheria na kanuni za nchi ili wazalishe wapate fainda, jamii zinufaike na serikali pia ifaidike.
“Ndugu zagu niwaambie kuwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan ametutuma kuwafikishia wawekezaji katika sekta zote ujembe kuwa Rais amefungua dirisha la kuwekeza katika sekta mbalimbali zitakazokuza uchumi, njooni muwekeze mpate faida na serikali ipate faida.” Alisema na kuongeza kuwa
“Tutafanya kila linalowezekana kuweka mazingira rafiki kwa sababu tunawapenda wawekezaji.”
Pia amewataka wawekezaji hao kuendelea kulipa kodi na kudumisha mahusiano mazuri kati yao na jamii inayowazunguka.
Lengo la serikali ni kuona wawekezaji wasiwe chanzo cha migogoro na badala yake walete neema na wao wapate neema.
Akiongea katika ziara hiyo Mkuu wa wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda amemuhakikishia Naibu Waziri huyo kuwa serikali ya kijiji imekuwa mstari wa mbele kumsaidia kutatua migogoro inayodaiwa kuibuka katika mgodi huo.
Awali akiwasilisha taarifa yake mwekezaji wa kampuni ya Sunshine inayochimba madini ya dhahabu katika kijiji hicho, Ndugu Narcis alisesma kuwa anatoa shukrani kwa Mkuu wa Wilaya hiyo kwa kuwa mara wanapopata tatizo huwa analitatua na wanapohitajia msaada huwa wanaupata haraka.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kijiji hicho, Mohammed Abasi akamueleza Naibu Waziri huyo kuwa wanamuomba mwekezaji huyo kuanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa Zahanati na kujenga madarasa katika shule mpya ya msingi katika kata hiyo kwa sababu tayari amaeanza uzalishaji.
“Kwa kweli mwakezaji huyu hana shida kabisa, hivyo kwa sababu ameanza uzalishaji tunamuomba ahakikishe anatekeleza makubaliano yetu ya kujenga Zahanati na madarasa katika shule mpya ya msingi.” Alisema Abasi.
Naye mmoja kati ya watumishi wa kampuni hiyo anayelinda eneo la kuwekea maji yanayodaiwa kuwa na chembechembe za kemikali, MG 4281 alisema kuwa katika kampuni hiyo kunachangamoto nyingi huku akitolea mfano wa kutokuwa na vifaa vya kuvaa mikononi pindi wanapo safisha eneo hilo.
“Tunaiomba serikali kuliangalia hili suala kwa sababu tunafanya kazi ambayo sio sahihi na ambayo ni hatarishi sana.” Alisema
MWISHO
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.