Na Hemedi Munga
tehama@irambadc.go.tz
Singida - Iramba. Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini nchini kuanza zoezi la kufuatilia leseni ambazo wahusika wake wamezishikilia bila kuzifanyia kazi ya uchimbaji wa madini ili taratibu za kuzifuta zifanyike haraka.
Dkt Kiruswa ametoa agizo hilo leo Jumamosi Februari 19, 2022 wakati wa kongamano la wadau kujadili fursa na changamoto kwenye sekta ya madini lililofanyika katika ukumbi mkubwa wa mikutano wilayani Iramba mkoa wa Singida.
“Nitoe wito kwa wamiliki wa leseni za kuchimba na kutafiti madini wazifanyie kazi kabla ya Wizara kwa kushirikiana na Tume ya Madini kuzifuta ili ziwe huru kwa wachimbaji waliotayari kuzifanyia kazi ambao wataweza kuipatia serikali mapato.” Alitoa wito Naibu Waziri Kiruswa
Aidha, aliongeza kuwa Wilaya ya Iramba inafursa za kuwekeza kwa wachimbaji wadogo kupata mitambo na vifaa vya kutoa maji, mikopo, vifaa vya umeme na genereta, hivyo aliwakaribisha wawekezaji kuwekeza katika nyanja hizo.
Pia alifafanua kuwa fursa zilizopo katika sekta ya madini zinaenda sambamba na fursa za kilimo, mifugo na uvuvi kwa sababu migodi huitaji bidhaa za kilimo na mifugo kwa ajili ya chakula.
Sekta ya madini imeongeza mchango katika Pato la Taifa kutoka asilimia 3.8 mwaka 2015 na kufikia asilimia 7.9 mwaka 2021.
Kufuatia mchango huo, Dkt Kiruswa aliwataka wachimbaji wote nchini kuacha tabia ya kutorosha madini kwa sababu serikali ipo macho masaa 24 badala yake wachimbaji waendelee kulipa tozo za serikali bila shuruti.
Hatua hii itaiongezea serikali tija na nguvu kuwahudumia wananchi kwa kujenga miundombinu ya barabara, mawasiliano na huduma za kijamii.
Dkt. Kiruswa alibainisha kuwa kutoa huduma hizo kumesababisha Mataifa mbalimbali duniani kuiamini serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ambapo Februari 18 mwaka huu alipata fedha takribani Tsh 1.15 trilioni toka Kamisheni ya umoja wa Ulaya ili zitumike katika miradi ya maendeleo na kuongeza ajira kwa vijana.
“Niwahakikishie wananchi kote nchini kuwa kongamano hili ni alama inayodhihirisha umuhimu wa sekta hii katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi na watu.” Alisisitiza
Katika hatua nyingine Dkt Kiruswa amewataka viongozi wa Iramba na maeneo mengine nchini kukamilisha agizo la serikali la upangaji wa postikodi kwa ajili ya anuani za makazi ili kurahisisha mawasiliano na utoaji wa huduma za msingi kwa wananchi.
Halikadhalika, amewataka wananchi kote nchini kuwa tayari kuhesabiwa katika zoezi la sensa ya watu na makazi ifikapo Agasti mwaka huu ili kuiwezesha serikali kupanga mipango ya maendeleo ya wananchi wake.
Akiongea katika Kongamano hilo Mkuu wa wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda alisema kuwa Wilaya ya Iramba inarasilimali nyingi za aina mbalimbali za madini na hivyo kuahidi kuifanya Iramba kuingia kumi bora Tanzania kwa uzalishaji wa Madini.
Mwenda alifafanua kuwa mwaka jana Wilaya ya Iramba ilizalisha madini ya dhahabu takribani gramu 319,000 na kuingizi serikali zaidi ya Tsh 37 bilioni.
“Huu ni mchango mkubwa na nimuhimu utambulike, hivyo ninaamini sasa tunatoka katika hali ya kutotambulika kama wilaya inayozalisha dhahabu na kuwa wilaya ya kwanza inayozalisha dhahabu Tanzania.” Aliahidi
Aidha, aliongeza kuwa wilaya ya Iramba inakata 20 ambapo kati ya kata hizo kata 16 zote zina madini ya dhahabu, hivyo upo uwezekano wa kata zote zikawa na madini.
Wakitoa changamoto anuai na michango yao wachimbaji waliohudhuria Kongamano hilo, Rajina bile alimuomba mkuu huyo wa wilaya kuwapatia wanawake enoa ambalo wanawake watachimba madini kwa sababu wanawake nao wako mstari wa mbele katika sekta ya madini.
“Ni kweli wanaume tuko nao hawatunyanyasi wala kutunyanyapaa na mimi ni Mwenyekiti wa Mgodi wa Uwema naongoza wanawake lakini tunahitaji mgodi utakaomilikiwa na wanawake tu.” Aliomba Bile
Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Nkonkilangi, Mohamed Abasi alimuomba Mkuu huyo wa wilaya kuwasaidia wananchi kwa kuwataka wawekezaji wa madini katika maeneo yao kutekeleza ahadi ya miradi ya maendeleo waliyoahidi kabla ya kuchimba madini.
Pia aliomba barabara zinazokwenda migodini ziboreshwe ili wawekezaji wafike katika maeneo hayo kwa urahisi.
Walaya ya Iramba ina madini ya dhahabu, almasi, gesi asilia, chunvi, mawe ya nakshi, zircon na quartz.
MWISHO
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.