Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa amesikiliza kero na changamoto mbalimbali za watumishi wa wilaya ya Iramba Mkoani Singida na kuzitolea majibu.
Dkt. Mwanjelwa amezungumza na watumishi mbalimbali wa wilaya ya Iramba katika kikao kilichofanyika leo Alhamisi Januari 8, 2020 katika ukumbi mkubwa wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba mjini hapa.
Katika kikao hicho Dkt. Mwanjelwa amewataka waajiri kote nchini kutenga muda wa kutoa elimu kwa watumishi waliopo katika mamlaka zao.
“Ninawaagiza waajiri wote nchini muwatendee haki watumishi waliopo katika mamlaka zenu, inaelekea watumishi wengi hawajui haki zao kiasi ambacho hushindwa kuelewa sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma hivyo kusababisha malalamiko mengi yasio kuwa ya msingi”
“Nanyi watumishi wa umma mnapaswa kushukuru kuwa mmekuwa watumishi wa umma, kuwa mtumishi wa umma ni hadhi kubwa kwa serikali inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli hivyo utumishi wa umma ni neema mnapaswa kuitendea haki”
“ Utumishi wa umma ni fursa kwa kuwa kila idara na sekta zinahitaji rasilimali watu kufikisha huduma kwa wananchi,” alisisitiza Dkt. Mwanjelwa
Pia amewataka kuwa wavumilivu wakati serikali inazifanyia kazi changamoto mbalimbali za utumishi huku akiwataka kuacha kuiga yasiofaa na kuwa na tabia ya kushauriana haswa pale unapoona mwenzio anafanya vibaya.
Akiongelea suala la uhamisho wa watumishi amewataka kutumia utaalamu wao kuboresha mapato ya serikali kama sehemu hiyo ilikuwa na changamoto ya kuwa na mapato hafifu.
Hata hivyo amewataka waajiri wote nchini kuwatendea haki watumishi wote wanaotaka kuhama kuwaidhinishia uhamisho wao nasio kuziweka barua zao katika droo kwani uhamisho hutolewa na katibu mkuu wa wizara inayohusika.
Akitoa kero yake kwa niaba ya maafisa Tarafa wa wilaya hiyo , Afisa Tarafa wa Tarafa ya Shelui Nicolas Makoye amemuomba Naibu Waziri huyo kuwasaidia kupata ofisi kwani ofisi wanazofanyia kazi ni chakavu na haziko kiofisi.
Naye mtumishi kutoka idara ya mifugo na uvuvi, Deogratius Isagala ameiomba serikali kuongeza kasi ya kulipa stahiki mbalimbali ikiwemo ya kukaimu ukuu wa idara au kitengo.
“Mheshimiwa Naibu Waziri ninaiomba serikali kuanzisha programu maalumu ya kimkakati ya kuwaandaa wastafu miaka sita kabla ya kustafu ili kuwajengea dira na mwelekeo mzuri katika maisha baada ya kustafu utumishi wa umma, sekta ya wastaafu iliyoboreshwa inaweza ikawa fursa muhimu katika eneo la mapato na maendeleo ya nchi,” alifafanuwa Isagala
Pia Afisa Mtendaji wa kata ya Tulya , Mwajuma Lugambwa amesema kuwa hawajawahi kulipwa madeni yao licha ya kuambiwa yalikwisha hakikiwa na kupelekwa TAMISEMI.
“Mheshimiwa Naibu Waziri tunaiomba serikali kutupatia usafiri kwani tunafanya kazi katika mazingira magumu kwa kuwa baadhi ya kata ina vijiji vingi na viko mbalimbali kiasi ambacho kufanya utendaji wetu kutofikia malengo tuliyojiwekea,” alisema Lugambwa
Wakuu wa idara mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba wakimfuatilia kwa makini Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa wakati akizitolea majibu kero na changamoto mbalimbali za watumishi wa wilaya ya Iramba Mkoani Singida. Picha na Hemedi Munga
Wakuu wa idara na watumishi mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba wakimfuatilia kwa makini Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa wakati akizitolea majibu kero na changamoto mbalimbali za watumishi wa wilaya ya Iramba Mkoani Singida. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.