Na Hemedi Munga
tehama@irambadc.go.tz
Singida - Iramba. Mkuu wa wilaya ya Iramba mkoani Singida, Suleiman Mwenda aliwaeleza wajasiriamali kazi kubwa na mafanikio lukuki yaliopatikana wilayani Iramba ambayo ameyafanya Rais Samia ndani ya mwaka mmoja wa uwongozi wake.
Mwenda alieleza mafaniko hayo mwishoni mwa juma hili wakati alipokuwa akifunga mafunzo ya ujasiriamali yalioendeshwa na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) katika ukumbi mdogo wa mikutano wilayani hapa.
Akielezea kuhusu takwimu za watu nchini, alisema kuwa akina mama ni wengi ukilinganisha na wananume.
“Wanawake ni kundi muhimu sana kwa sababu ukimuelimisha na kumuwezesha mwanamke unakuwa umeiwezesha na kuielimisha jamii” Alisema Mwenda
Aidha, alilipongeza Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) kwa kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa akina mama 49 na wanaume 8 ambao hivi karibuni wataanza kuzalisha matokeo chanya yatakayoinufaisha jamii.
Halikadhalika, alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Mhandisi Michael Matomora kwa kutenga takribani Tsh 140 milioni kwa ajili ya akinamama, vijana na watu wenye mahitaji maalumu.
“Ni dhahiri kuwa mitaji na teknolojia hii mlioyoipata kutoka SIDO inawawezesha kuendesha shughuli za kusindika karanga, vitunguu, nyanya, mvinyo na kutengeneza keki, hivyo mazao yetu yataongezeka thamani na kuwakwamuwa wajasiriamali wetu katika nyanja ya uchumi.” Aliongeza
Kufuatia mafunzo hayo, Mwenda alitumia jukwaa hilo kuwataka wajasiriamali kutumia fursa ambazo zinakuja katika wilaya ya Iramba kupitia mradi wa bomba la mafuta, uwepo wa mafuta katika Bonde la Wembere, madini ya dhahabu na madini ya almasi yaliogundulika hivi karibuni.
“Sisi kama wajasiriamali nilazima tujipange kuzitumia fursa ambazo Rais Samia anazileta kwetu, hivyo tujipange kuuza vyakula, kupeleka vifaa vya ujenzi na shughuli za ulinzi.” Alisema
Halikadhalika, tunayo matarajio ya kupata kiwanda kikubwa cha mbolea wilayani hapa, hivyo tunatarajia kubadilisha maisha ya wananchi kupitia shughuli mbalimbali na muingiliano wa watu watakaohudumu katika kiwanda hicho.
Katika hatua nyingine yamafaniko yaliopatikana wilayani hapa baada ya kutimia mwaka mmoja wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Mkuu huyo wa wilaya alielezea mafanikio lukuki yaliyopatikana Iramba katika utawala wa Rais huyo.
Alifafanua kuwa wakati Rais Samia anaingia madarakani upatikanaji wa maji wilayani Iramba ulikuwa asilimia 26 lakini ndani ya mwaka mmoja wa utawala wake upatikanaji wa maji umefikia asilimia 59 ambapo kuna miradi mikubwa ya maji yenye thamani ya takribani 4.8 bilioni inatekelezwa katika maeneo tofauti tofauti.
Katika sekta ya afya tangu kupatikana kwa uhuru wilaya ya Iramba ilikuwa na vituo vya afya 3 lakini ndani ya mwaka mmoja wa Rais Samia ameweza kujenga vituo vya afya 5 ambapo kila kimoja kinagharibu takribani Tsh 500 milioni.
Pia, aliongeza kuwa katika Hospitali ya wilaya kunaujenzi unaendelea wenye thamani ya takribani Tsh bilioni moja.
Akiongelea kuhusu sekta ya elimu, Mwenda alisema kuwa Rais Samia alileta takribani Tsh 2 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa ambapo wilaya imefanikiwa kujenga vyumba vya madarasa 57 nakufanikiwa kutokomeza upungufu wa madarasa wilayani hapa.
Katika sekta ya nishati wilaya ya Iramba ilikuwa na vijiji 46 vyenye umeme na vijiji 14 ambavyo havina umeme ambapo tayari Rais Samia aliishaleta fedha kwa ajili ya kumalizia vijiji 14 vipate umeme na kufanya vijiji vyote vya wilaya hii kuwa na umeme.
Aidha, aliongeza kuwa kupatikana umeme wilayani hapa kutawezesha wajasiriamali wadogo kufanya shughuli za usindikaji wa bidhaa mbalimbali wakati wote na popote hatimaye kuweza kujikwamuwa kiuchumi.
Akiongelea kuhusu sekta ya barabara na miundombinu, alisema kuwa wilaya imepata zaidi ya Tsh 80 bilioni kwa ajili kutengeneza barabara kwa kiwango cha lami inayoanzia Kizaga, Mukulu, Ndago, Mbelekese hadi Singida mjini.
“Haya ni mafanikio makubwa sana ambayo tunajivunia na hivyo tutaendelea kuwasimamia watumishi wenzetu ili kutimiza azma ya viwango na mafanikio ambayo Taifa linategemea kuyapata.” Alisisitiza
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Mhandisi Michael Matomora aliwahimiza wajasiriamali hao kuyaingiza mafunzo walioyapata kivitendo ili kupata viwanda vingi nchini.
“Nendeni mkayatumie mafunzo haya kama mwanzo wa kutengeneza viwanda vikubwa vilivyo katika ndoto zenu.” Aliagiza
Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo kwa niaba ya wanafunzi wote, Emmanuel Yohana alimshukuru Rais Samia kwa kufanikisha kufadhili mafunzo haya kupita Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) lililofandhiliwa na Shirika la elimu (TEA).
Yona alisema kuwa wamefanikwa kujifunza kwa nadharia na vitendo na hivyo wanauwezo wa kuzalisha bidhaa mbalimbali zinazohitajika katika jamii yao.
MWISHO
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.