Mafunzo ya Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST), yametolewa kwa watumishi mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba wakiwemo, Wakuu wa Idara na Vitengo, Waalimu Wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari, Waganga Wafawidhi wa Hospitali, Zahanati na Vituo vya Afya kuanzia Januari 27, 2025, lengo ikiwa ni kuongeza ufanisi na uaminifu katika kufanya manunuzi Serikalini.
Mafunzo hayo ya siku mbili, yametolewa na wawezeshaji kutoka Mamlaka ya Udhibiti na Ununuzi wa Umma (PPRA) Kanda ya kati na Magharibi ambao ni Bw. Lusekelo Kamwela na bi. Anna Bulele, ambapo kupitia mafunzo hayo watumishi wamepata nafasi ya kufundishwa namna ya kutumia mfumo huo wa manunuzi na kuelezea changamoto wanazo kumbana nazo pindi watumiapo mfumo huo, na kupatiwa majibu juu ya changamoto hizo.
Akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Ndugu Michael Agustino Matomora, ameshukuru uwepo wa mafunzo hayo kutoka PPRA na kuwaagiza watumishi waliopata mafunzo kwenda kuwapa Elimu Mafundi ujenzi na wazabuni walio katika maeneo yao kuhusu faida za matumizi ya mfumo kwao ikiwa ni pamoja na kuwasaidia kujisajili katika Mfumo huo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma.
“Nendeni mkawashawishi Mafundi walio katika maeneo yenu kujisajili katika Mfumo na mkawawasaidie kufungua akaunti na jinsi ya kufanya shughuli zote katika Mfumo ili wakashindanie kazi katika Mfumo.” Alisema Matomora.
Mafunzo hayo yamemalizika rasmi Januari 28, 2025 ikiwa ni siku ya pili, ambapo wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na baadhi ya wasaidizi kutoka katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri, nao wamepatiwa mafunzo.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.