MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, amewataka Madiwani ambao ni wajumbe wa Kamati ya Fedha na Uongozi kila mwezi kuweka agenda moja ya kujadili hoja za ukaguzi zinazoibuliwa kwenye Halmashauri zao na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Amesema hayo leo (Juni 15, 2023) kwenye Kikao Maalum cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba ambacho kiliketi kwa ajili ya kujadili hoja za CAG za mwaka 2021/2022 na za miaka ya nyuma.
Serukamba ambaye aliambatana na Katibu Tawala Mkoa wa Singida (RAS), Dkt. Fatma Mganga, amesema kama Kamati za Fedha zitajiwekea utaratibu huo wa kujadili hoja za ukaguzi za CAG kutamfanya Mkurugenzi wa Halmashauri na watendaji wake kutambua kuwa Madiwani wanafuatilia kwa karibu mambo hayo.
"Tukiwa tunafanya hivyo tutajua mzembe anayetukwamisha ni nani na ikiwa Mkuu wa Idara ataonekana amekaa zaidi ya miezi sita bila kujibu hoja za CAG ambazo zinajitokeza katika idara yake tuandikieni barua kutujukisha," alisema Serukamba.
Amesema kimsingi kuwepo kwa hoja nyingi za CAG kwenye Halmashauri ni suala la uzembe wa baadhi ya watendaji kutokuwa makini kufuatilia majukumu yao na kuagiza kila mtumishi ahakikishe anawajibika ipasavyo ili kila Halmashauri kusiwe kunajitokeza hoja za CAG.
Mkuu wa Mkoa akizungumza suala la ukusanyaji mapato katika Halmashauri ya Wilaya Iramba alisema bado hali sio nzuri hasa kutokana na baadhi ya watumishi kuendelea na tabia ya kula fedha mbichi wanazozikusanya badala ya kuzipeleka benki.
Alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Michael Matomora, kukomesha vitendo vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wenye tabia ya kufuja fedha walizozikusanya.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Fatma Mganga, alisema ushauri unaotolewa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) uwe unafanyiwa kazi na Madiwani na Watendaji badala ya suala hili linahusu viongozi tu Halmashauri.
Alisema Madiwani wahakikishe hoja za ukaguzi za CAG hazijirudii mara kwa mara kila mwaka kwani hali kama hiyo ikiwa inajitokeza itaweza kusababisha Halmashauri kupata hati mbaya.
Dkt. Mganga alisema kujitokeza kwa hoja nyingi za ukaguzi za CAG katika Halmashauri ya Wilaya ya Iramba kunatokana na kutojibiwa barua kwa wakati tatizo ambalo limejitokeza kwa Halmashauri nyingine za Mkoa wa Singida.
Hata Hivyo, aliwapongeza Madiwani na Watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba kwa jitihada kubwa walizozifanya na kupunguza hoja za CAG kutoka 113 na kubakia hoja 33.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Iramba, Michael Matomora alimhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Singida kuwa tabia ya ulaji wa fedha mbichi haitajirudia tena katika Halmashauri hiyo atakuwa anachukua hatua kali kwa Watumishi watakaobainika kufanya vitendo hivyo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Innocent Msengi, alitoa wito kwa wananchi ndani na nje ya Wilaya hiyo kujitokeza kununua viwanja vilivyotengwa na Halmashauri ili kuujenga mji wa Iramba.
Msengi alisema katika miradi ya maendeleo inayotekelezwa hivi sasa katika Halmashauri hiyo ifikapo Juni 30, mwaka huu bila shaka itakuwa umekamilika.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Innocent Msengi akizungumza kwenye Kikao Maalum cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba ambacho kiliketi kwa ajili ya kujadili hoja za CAG za mwaka 2021/2022 na za miaka ya nyuma
Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, akizungumza kwenye Kikao Maalum cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba ambacho kiliketi kwa ajili ya kujadili hoja za CAG za mwaka 2021/2022 na za miaka ya nyuma.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.