SERIKALI KUENDELEA KUIMARISHA ELIMU YA WATU WAZIMA SINGIDA
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego, amesema serikali inaendelea kuwekeza katika miundombinu na kuajiri walimu wa kutosha ili kuongeza upatikanaji wa elimu inayofanana na mazingira ya sasa.
“Serikali yetu imeendelea kuwekeza kwa sehemu kubwa sana katika ujenzi wa miundo mbinu ya kielimu, kuajiri walimu, kununua vitendea kazi kwaajili ya walimu na kuhakikisha kwamba inatengeneza mazingira bora kwa vijana kujifunzia...si tu kwamba mtu atapewa elimu ya namna ya kushona, bali atapewa pia elimu ambayo inamueleza kwamba anatumiaje teknolojia kutafuta soko, kujiunga katika makundi mbalimbali ya uwezeshaji ambayo serikali inatoa….” Alisema DC Mwenda
Pia, alisistiza umuhimu wa elimu ya watu wazima akisema, “Elimu ya Watu Wazima ni sehemu ya stadi za maisha, inamuwezesha mtu kujua mazingira ya sasa tuliyonayo na inalenga kumkomboa mwanadamu katika nyanja zote za kimaisha.”
Kwa upande wake Afisa Elimu ya Watu Wazima mkoa wa Singida, Sara Mkumbo, alisema Singida ni miongoni mwa mikoa sita iliyopata ufadhili wa Mradi wa Elimu Changamani kwa Vijana walio nje ya shule (IPOSA) kwa mwaka 2024/2025, ambao unatekelezwa katika wilaya za Iramba, Itigi, Manyoni na Mkalama na unatarajiwa kunufaisha vijana 360 wenye umri kuanzia miaka 14 na kuendelea watakaopewa mafunzo mbalimbali ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika Septemba 1, 2025 Kiomboi - Iramba halmashauri za Mkoa wa Singida ziliagizwa kutenga bajeti kila mwaka kupitia mapato ya ndani ili kuimarisha elimu ya watu wazima, elimu nje ya mfumo rasmi na elimu maalum.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.