Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Serikali ya Tanzania imesema shule zote za awali, msingi na sekondari zitafungwa kwa siku 30 kuanzia leo Jumanne Machi 17, 2020 ili kuzuia kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya Corona ( COVID–19)
Maamuzi hayo yametolewa na Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa leo Jumanne Machi 17, 2020 wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Amesema wanafunzi wa kidato cha sita walipaswa kuanza mitihani Mei 4, 2020 lakini na wawo watapaswa kusubiri Wizara ya Elimu ifanye utaratibu mwingine kulingana na matokeo ya hali ya maambukizi ya virusi vya Corona.
Amesema mikusanyiko yote mikubwa ya ndani na ya nje isio yalazima imesitishwa kuanzia sasa ikiwamo shughuli za michezo, matamasha ya muziki, mikutano mbalimbali ikiwamo ya shughuli za kisiasa, mahafali na shughuli nyingine za kijamii.
Waziri Mkuu huyo amezitaka Wizara na Taasisi zisitishe semina, warsha, makongamano na mikutano yote hapa nchini ambayo inahusisha washiriki toka nchi zenye maambukizi makubwa.
“ Watanzania wenye safari zisizo za lazima kwenye nchi zenye maambukizi makubwa wanashauriwa wasitishe safari hizo,” amesisitiza Majaliwa
Akibainisha hatua nyingine zinazochukuliwa na serikali ili kuudhibiti ungonjwa huo, Waziri Mkuu amesema, “Serikali imesitisha michezo yote inayokusanya makundi ya watu ikiwamo ligi kuu ya Tanzania (VPL), Ligi Daraja la Kwanza (FDL), Ligi Daraja la Pili (SDL) na aina nyingine. Wizara ya Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo iziandikie taasisi zake.”
Halikadhalika, amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha maeneo yote yalioainishwa na kutengwa kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa endapo watajitokeza katika maeneo yao yanakuwa na mahitaji yote muhimu na kuhudumiwa ipasavyo.
Pia, Waziri Mkuu amesema serikali tayari imetoa Sh500 milioni kati ya Sh1 bilioni zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya mbio za Mwenge wa Uhuru zilizokuwa zianze Aprili 2, 2020.
“ Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameahirisha mbio za Mwenge wa Uhuru zilizokuwa zianze Aprili 2 mwaka huu na kuagiza sh1 bilioni zilizokuwa zimeandaliwa kwa ajili ya shughuli hiyo, zipelekwe Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa ajili ya maandalizi ya kujiweka tayari kudhibiti maambukizi ya Corona. Serikali tayari imetoa milioni 500.”
Akizungumzia hatua zilizochukuliwa baada ya mgonjwa wa kwanza kubainika kuwapo nchini Tanzania, Waziri Mkuu amesema Serikali imechukua hatua ya kumchukuwa mgonjwa huyo na kumuifadhi kwenye eneo maalumu kwa ajili ya kumpatia huduma.
“ Pia, Serikali imefanya ufuatiliaji wa watu waliokutana na mgonjwa huyo tangu aingie nchini na kuwaweka kwenye karantini ya siku 14, pia kuchukuwa sampuli kwa ajili ya kubaini kama wameambukizwa virusi hivi,” amesema
Ugonjwa huu umeingia nchini baada ya Mtanzania mwenye miaka 46 aliyesafiri kwenda nchi za Ubeligiji, Sweden na Denmark hivi karibuni, kupimwa na kuthibitika kuwa na virusi vya Corona (COVID–19).
Akifafanua hatua zaidi zinazochukuliwa, Waziri Mkuu amesema licha ya hatua ambazo zimechukuliwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamaii, Jinsia, Wazee na Watoto Serikali itaimarisha ukaguzi na ufatiliaji wa wasafiri wanaoingia nchini kupitia viwanja vya ndege, bandari na mipaka ya nchi kavu ili kuwabaini wasafiri wenye dalili za ugonjwa na viashiria vya hatari.
“Tutaimarisha uwezo wa kupima sampuli kwa watu wanaohisiwa kuwa na viashiria au dalili za ugonjwa huo ambapo maabara yetu ya Taifa kwa sasa inauwezo wa kutoa majibu kwa haraka,” amesema
Amesema serikali inaendelea kuwajengea uwezo (mafunzo) watumishi wa sekta ya Afya ili kukabiliana na magonjwa ya milipuko ikiwemo namna ya kutoa tiba, kuchukua sampuli, uelimishaji na kuzingatia kanuni za Afya.
“ Serikali imetenga hospitali maalum za Mloganzila (Dar es Salaam), kituo cha Buswelu (Mwanza) na hospitali ya Mawenzi (Kilimanjaro), Mnazi Mmoja (Zanzibari) na Chake Chake (Pemba) kwa ajili ya kutoa huduma kwa waathirika.”
Ameiagiza Wizara ya Afya kuhakikisha vifaa vya kinga ikiwamo vimiminika vya kudhibiti maambukizi (Hand sanitizer) vinapatikana katika maduka yote husika na kwa bei ya kawaida huku akitahadharisha kuwa serikali itachukua hatua kwa wafanyabiashara watakaobainika kufanya uranguzi wa vifaa hivyo.
Aidha, amewataka watanzania kuzingatia ushauri unaotolewa na serikali na kupuuza taarifa za uzushi zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
“ Watanzania tuache mzaha wa kutumia mitandao ya kijamii kufanya upotoshaji wa jambo hili,” ameongeza Waziri Mkuu
Amewaomba viongozi wa dini waendelee kushirikiana na serikali kuwaelimisha waumini wao wote kuzingatia tahadhari ya ugonjwa huu huku akivitaka vyombo vyote vya habari kushirikiana na serikali kutoa elimu kwa umma kuhusu kujikinga na Corona bila ya kufanya upotoshaji wala kuipa jamii hofu.
Amewataka wananchi watoe taarifa kuhusu uwepo wa mgonjwa au kupata ufafanuzi kuhusu ugonjwa huu kupitia namba za bure za 0800110124, 0800110125 na 0800110037.
MWISHO
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.