SERIKALI YAWAHIMIZA WAFUGAJI MKOANI SINGIDA KULINDA MIFUGO KUPITIA CHANJO NA UTAMBUZI
Wafugaji mkoani Singida wametakiwa kushiriki kikamilifu katika zoezi la uchanjaji na utambuzi wa mifugo yao, ambapo utekekelezaji wa zoezi hilo mkoani humo limeanza rasmi leo, Julai 8, 2025, katika Kata ya Kyengege, Kijiji cha Makunda, Wilaya ya Iramba. Lengo la zoezi hilo ni kulinda mifugo dhidi ya magonjwa na kuboresha ubora wake kwa ajili ya ushindani katika soko la kimataifa.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mafunzo ya Mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambene, amesema kuwa zoezi hilo ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya uchanjaji na utambuzi wa mifugo, iliyozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 16 Juni 2025. Amesema kampeni hiyo inalenga kuongeza tija kwa wafugaji nchini, hivyo ni muhimu kulizingatia.
Dkt. Mwambene alieleza kuwa katika kampeni hiyo, wafugaji watanufaika na chanjo kwa gharama ya ruzuku baada ya Serikali kutoa kiasi cha Shilingi Bilioni 216 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo kwa kipindi cha miaka mitano.
"Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alishazindua kampeni hii ya chanjo na ameridhia kuchangia nusu gharama ya chanjo ili kuwasaidia wafugaji kote nchini kuikinga mifugo yao dhidi ya magonjwa na kuimarisha biashara ya Mifugo na mazao yake katika masoko ndani na Kimataifa, hivyo wafugaji wa mkoa huu wa Singida jitokezeni na mshiriki kikamilifu kwenye kampeni hii" alisema Dkt. Mwambene.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Wilaya ya Iramba, Bw. Morton Msowoya, alibainisha kuwa aina za chanjo zitakazotolewa ni pamoja na chanjo dhidi ya homa ya mapafu kwa Ng’ombe, Sotoka kwa Mbuzi na Kondoo, pamoja na chanjo dhidi ya Kideli, Mafua na Ndui.
Baadhi ya wafugaji wilayani Iramba wameishukuru Serikali kwa kuwawezesha kupata chanjo kwa ruzuku, wakieleza kuwa kabla ya kuanzishwa kwa kampeni hiyo, mifugo mingi ilikufa kutokana na magonjwa mbalimbali.
Utekelezaji wa zoezi hilo kwa ngazi ya mkoa wa Singida unaendelea sambamba na uhamasishaji kwa wafugaji kushiriki kikamilifu, ambapo zaidi ya mifugo laki tano inatarajiwa kuchanjwa wilayani Iramba na zaidi ya milioni nne kwa mkoa mzima.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.