SHULE YA SEKONDARI LULUMBA MSHINDI WA 3 MASHINDANO YA YOUNG SCIENTISTS TANZANIA
Mkuu wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida, Suleiman Yusuph Mwenda, ameipongeza Shule ya Sekondari Lulumba kwa kushika nafasi ya tatu katika mashindano ya Young Scientist Tanzania (YST) yaliyofanyika Septemba 18, 2025, katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mashindano hayo yalikutanisha shule 45 kutoka maeneo mbalimbali nchini, ambapo nafasi ya kwanza ilichukuliwa na Tabora Boys, nafasi ya pili St. Joseph Cathedral, huku Shule ya Sekondari Lulumba ikishika nafasi ya tatu kitaifa.
Akizungumza wakati wa kukabidhiwa kombe hilo Septemba 26, 2025, DC Mwenda alisema "matokeo hayo ni fahari kubwa kwa wilaya na uthibitisho wa juhudi endelevu za Shule ya Lulumba katika taaluma." Aliongeza kuwa kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitano shule hiyo imeendelea kuongoza katika matokeo ya kitaaluma kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa, kanda hadi taifa. Aidha, aliahidi kutoa zawadi kwa wanafunzi wawili ambao ni Elisha Amos Lugomela (kidato cha 3 PCM) na Onesmo Filbert Mhonzu waliowakilisha shule kwa usimamizi wa mwalimu Joshua Mahindoni, ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wao.
Kwa upande wake, mwanafunzi Onesmo Mhonzu (Kidato cha Sita, PCB) aliishukuru shule na viongozi waliowawezesha kushiriki, akibainisha kuwa uzoefu walioupata utawasaidia kuongeza ujuzi wa kisayansi na maandalizi ya kazi za baadaye.
Shule ya Sekondari Lulumba ilishiriki kupitia kundi la AGRICULTURAL SCIENCE kwa mada "URBAN-BEES ECOLOGICAL AND GENETIC IMPACTS ON POLLINATOR POPULATION,” ambayo iliiwezesha kushinda Kombe, medali ya dhahabu na cheti cha ushindi kwa wanafunzi na shule pamoja na zawadi ya fedha taslimu.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.