Taasisi ya African Sport Youth Park Yafanya Kliniki ya Kusaka Vipaji vya Soka Iramba, zaidi ya watoto 62 washiriki
Iramba, Singida
Taasisi ya African Sport Youth Park* yenye makao yake makuu Masumbwe, Wilaya ya Mbogwe, Mkoa wa Geita, imeendesha kliniki ya kusaka na kukuza vipaji kwa watoto na vijana wenye umri wa miaka 10 hadi 20 katika Wilaya ya Iramba.
Kliniki hiyo iliyofanyika kwa siku tatu kuanzia Aprili 14 hadi 16, 2025 katika Uwanja wa Kiomboi, ilihusisha washiriki zaidi ya 62 kutoka kata zote 20 za Wilaya ya Iramba.
Akizungumza wakati wa kufunga rasmi shughuli hiyo, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Bw. Hamis Selemani Kilinga, alisema lengo kuu ni kuibua na kuinua vipaji vya watoto na vijana walioko shuleni pamoja na wale walioko nje ya mfumo rasmi wa elimu.
“Taasisi yetu imejikita katika kuendeleza vipaji vya watoto kupitia mchezo wa mpira wa miguu (soka), lakini pia tunawapa mafunzo ya ufundi stadi kama vile utengenezaji wa chaki, kava za magari na pikipiki, pamoja na kuwafundisha lugha za kigeni kama Kiingereza na Kifaransa,” alisema Bw. Kilinga.
Aidha, Bw. Kilinga amesema lengo la mpango huu ni kuwawezesha vijana kupata ujuzi mbalimbali utakaowaandaa kwa maisha ya baadaye, huku wakijifunza kupitia michezo na kazi za mikono.
Kwa upande wake Afisa Michezo na Utamaduni Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Bw. John Mghana amesema kuwa Halmashauri imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa Michezo katika kuikuza na kuinua vipaji mbalimbali vya Watoto na Vijana.
"Wilaya yetu Ina Vituo vinne vya Michezo kwa Wanafunzi wa Shule za Msingi na Vituo viwili vya wanafunzi wa Shule za Sekondari na Mpango uliopo ni kuhakikisha tunaendelea kuwaunganisha wanafunzi na Watoto kuhakikisha tunaendelea kuinua vipaji vyao kupitia Michezo" Amesema John Mghana.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.