Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Wilaya ya Iramba Mkoani Singida imetoa semina kwa Maafisa Usafirishaji (Madereva Bajaji na Bodaboda) Juu ya kuzuia Vitendo vya Rushwa kuelekea Uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mwaka huu 2025.
Semina hiyo ilifanyika katika ukumbi mkubwa wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba tarehe 09 Oktoba, 2025.
Akizugumza wakati wa ufunguzi, Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleiman Mwenda amewataka Maafisa hao kuhakikisha wanazuia vitendo vya rushwa akisisitiza kuwa kuwepo kwa vitendo hivyo katika Jamii Kunasababisha Kuchelewa kwa Maendeleo.
"Tuungane kwa pamoja kuhakikisha kwamba tunaipiga vita rushwa ili tuweze kupata maendeleo kwa haraka. Tukiendekeza rushwa hatutapata maendeleo kwa haraka... Lazima wakati wote tujitahidi kuikataa na kuhakikisha hatujiingizi katika vitendo ambavyo vitatufanya tuweze kutoa ama kupokea rushwa katika maeneo yetu ya utendaji kazi." Alisema DC MWENDA
Kwa upande wake Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Iramba Ahmad Sungura alisema baada ya elimu kutolewa kwa maafisa hao, ni matarajio ya TAKUKURU kuwa, wataweza kufichua vitendo vya rushwa vinayotendeka katika mazingira ya kazi zao na hata kipindi hiki cha uchaguzi, kufichua waalifu wengine ikiwa ni pamoja na wahamiaji haramu na wataweza kushiriki uchaguzi mkuu 2025 kwa uhuru na amani bila kushawishiwa au kurubuniwa kwa rushwa.
Semina hiyo ya siku moja ilitolewa kwa maafisa usafirishaji 125 kati ya 181 walioalikwa ikiwawezesha maafisa usafirishaji kupata elimu kutoka TAKUKURU, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Polisi, Uhamiaji, Zimamoto na Idara ya Maendeleo ya Jamii, lengo likiwa kuwafikishia elimu ya mapambano dhidi ya rushwa chini ya kauli mbiu isemayo "Kuzuia rushwa ni jukumu lako na langu; tutimize wajibu wetu".


KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.