Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula ameipongeza TAKUKURU kwa kuokoa takriban Tsh 13.6milioni za Wakulima wa pamba ambao ni Wanachama wa Chama cha Msingi cha Ushirika Jikomboe AMCOS ambazo zilikua zimepotezwa na viongozi 7 wa AMCOS hiyo msimu wa 2018/2019.
Luhahula ametoa pongezi hizo leo Juni 10, 2020 wakati alipokua akikabidhiwa pesa hizo na Mkuu wa Taasisi ya kupambana na kuziwia rushwa (TAKUKURU) Wilayani Iramba, Ahmad Sungura katika kijiji cha Kikunku Tarafa ya Shelui Wilayani humo.
Akiongea na Wanachama wa AMCOS hiyo waliokua wakidai pesa hizo, Mkuu huyo wa Wilaya amevipongeza Vyombo vya Usalama vya Wilaya hiyo.
“Ninavipongeza sana Vyombo vya Usalama katika Wilaya yetu kwa kuwa wameshirikiana nakufanikisha kuokoa pesa hizi,” amesema Luhahula na kuongeza
“Kampuni ya ununuzi ilitoa pesa zote za Wakulima kwa Viongozi wa AMCOS, lakini Viongozi wa Jikomboe AMCOS wakala hizo pesa, hivyo kusababisha Wakulima kukosa pesa zao.”
Baada ya kubaini kuwa Wakulima wa kijiji hicho hawakupata pesa zao kwa sababu ya Viongozi wao wasiokua waadilifu tulilikabidhi kwa TAKUKURU.
“Ninampongeza tena Mkuu wa TAKUKURU Iramba kwa kulifanikisha hili, na leo tumekuja kifua mbele kuwalipa pesa zenu zote baada ya kuwabana Viongozi wa AMCOS waliokula na kuzirudisha,” amesema
Halikadhalika, Luhahula amewaasa Wakulima hao kuhakikisha wanazitumia pesa hizo vizuri bila ya kuwasahau wakinamama ambao walioonesha uvumilivu na waume zao halafu mkaenda tafuta Wanawake wengine.
“Tafadhalini msiseme leo tumepata pesa zetu tunakwenda kuzipiga faini na kuoa mke mwingine, hao Wanawake mlioteseka nao kusubiria wakapate faida hiyo,” ametilia mkazo Mkuu wa Wilaya
Katika hatua nyingine, Luhahula amemuagiza Afisa Ushurika wa Wilaya hiyo, Heriman Kimario kuwachukulia hatua Viongozi wa AMCOS wilaya nzima wasiokua waadilifu na waaminifu huku akiwataka watendaji wa vijiji vyote kuwafichua Viongozi hao wasiokua waadilifu ili kuuwekea hashima Ushirika.
Akifafanua namna ya walivyoweza fanikisha malipo ya pesa hizo, Kamanda wa TAKUKURU wa Wilaya hiyo, Amhad Sungura amesama baada ya kupokea taarifa ya upotevu wa Tsh 13.6milioni za mauzo ya pamba ya Chama cha Ushirika Jikomboe AMCOS chenye namba ya usajili SIR/0737B toka kwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya hiyo Mei 4, mwaka huu, uchunguzi ulifanyika nakubaini kuwa viongizi 7 wa AMCOS wamezipoteza pesa hizo.
Sungura amesema msimu wa 2018/2019 Jikomboe AMCOS ilikusanya pamba kutoka kwa wanachama wake kilo 106,820 zenye thamani ya Tsh 128.18milioni ambapo zilinunuliwa na kampuni ya Biosustain (T) LTD na kulipa pesa zote kwa Jikomboe AMCOS.
TAKUKURU ilibaini kuwa kunawakulima ambao ni wanachama wa Jikomboe AMCOS 64 waliouza pamba yao kilo 11,318 zenye thamani ya Tsh 13.6milioni hawakulipwa pesa zao.
Kufuatia uchunguzi huo, TAKUKURU imeweza kuokoa Tsh 13.6milioni na kuzikabidhi kwa Mkuu wa Wilaya hiyo kwa lengo la kuwagawia wakulima hao.
Kwa upande wake mmoja wa waathirika wa upotevu wa fedha hiyo, Amani Bernad amesema kuwa Viongozi wa AMCOS waliohusika na upotevu huo wa pesa wanapaswa kutumbuliwa kwa sababu wamewasababishia Wakulima hao hali ngumu ya maisha na kujikuta wanashindwa kulima vizuri kilimo cha mpunga kutokana na hali ya mvua ya mwaka huu.
“Hawa Viongozi hawafai na wangetakiwa kutumbuliwa kwa kuwa wametuhujumu, kutukandamiza na kuturudisha nyuma ili kuchagua wengine watakaoleta maendeleo katika kijiji chetu,” amesema Bernad
Pia, ameishukuru Serikali kwa kuanzisha mfumo mpya katika msimu wa mwaka huu ambao unamtaka mkulima kufungua akaunti benki ambapo ataweza kapata pesa yake ndani ya masaa 48 punde baada ya kuuza mazao yake.
Naye Fatuma Elia muhanga wa upotevu wa pesa hiyo, ameipongeza Serikali kwa kurahisisha mfumo wakulipa pesa za wakulima baada ya kuuza mazao kupitia akaunti za benki au namba za simu, hivyo kumfanya mkulima kulipwa hata kwa njia ya simu.
MWISHO
Kamanda Mkuu wa TAKUKURU Wilayani Iramba, Ahmad Sungura akimkabidhi Mkuu wa Wilaya hiyo, Emmanuel Luhahula Tsh 13.6milioni zilizokua zimepotezwa na Viongozi 7 wa Jikomboe AMCOS baada ya kuwa wameuza pamba kwa kampuni ya Biosustain(T) LTD na kulipwa fedha zote. Picha na Hemedi Munga
Fedha za Wakulima wa Pamba kijiji cha Kikunku Tarafa ya Shelui Wilayani Iramba zilizokua zimepotezwa na Viongozi 7 wa Jikomboe AMCOS baada ya kuwa wameuza pamba kwa kampuni ya Biosustain(T) LTD na kulipwa fedha zote. Picha na Hemedi Munga
Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Herman Kimario akigawa pesa za Wakulima wa Pamba kijiji cha Kikunku Tarafa ya Shelui Wilayani Iramba zilizokua zimepotezwa na Viongozi 7 wa Jikomboe AMCOS baada ya kuwa wameuza pamba kwa kampuni ya Biosustain(T) LTD na kulipwa fedha zote. Picha na Hemedi Munga
Baadhi ya Wakulima wa Pamba kijiji cha Kikunku wakisubiri kugawiwa pesa walizokua wameuza pamba msimu wa 2018/2019.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.