TRA IRAMBA YAVUKA MALENGO YA UKUSANYAJI KODI KWA ASILIMIA 130, YAWASHUKURU WALIPAKODI
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wilaya ya Iramba imetoa shukrani kwa walipakodi Wilayani Iramba kwa ushirikiano katika suala la ulipaji kodi, hali iliyowezesha mamlaka hiyo kuvuka malengo ya ukusanyaji kodi kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwa mafanikio ya asilimia 130.
Akizungumza Julai 1, 2025 katika hafla fupi ya kutoa shukrani kwa walipakodi iliyofanyika katika maeneo ya Kiomboi, Misigiri na Shelui, Kaimu Meneja wa TRA Wilaya ya Iramba, Bw. Detrick Andrew, alisema kuwa ushirikiano kati ya wafanyabiashara, wananchi na mamlaka hiyo umechangia kwa kiasi kikubwa kufikiwa kwa mafanikio hayo.
“Kwa mwaka wa fedha 2024/25, TRA Iramba imevuka malengo ya makusanyo kwa miezi yote kumi na mbili, ambapo lengo lilikuwa Shilingi 3,191,272,402 na tumekusanya Shilingi 4,137,436,842, sawa na asilimia 130 ya ufanisi,” alieleza Bw. Andrew.
Kaimu Meneja huyo pia aliwakumbusha wafanyabiashara umuhimu wa kutoa risiti kila wanapouza bidhaa au huduma, huku akiwaasa wananchi kudai risiti kila wanaponunua.
“Ndugu zangu wafanyabiashara na wananchi, mafanikio tunayoyapata yanatokana na ushirikiano wenu. Tuhakikishe tunatoa na kudai risiti ili tuendelee kujenga taifa letu,” alisisitiza.
Kwa upande wake, mmoja wa wafanyabiashara kutoka Kiomboi, Bi. Bernice Msuya, aliipongeza TRA kwa mbinu zake shirikishi na rafiki katika ukusanyaji wa kodi.
“Tunawashukuru TRA kwa kutumia mbinu rafiki. Tumekuwa tukipewa elimu ya umuhimu wa kulipa kodi kwa wakati, jambo ambalo linatuwezesha kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa,” alisema Bi. Msuya.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.