Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Linno Mwageni kumsimamisha kazi mara moja Afisa Ugavi na Manunuzi, Ibrahimu Nkumbi kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za Mfuko wa Jimbo la Iramba Magharibi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake leo Alhamisi Februari 27, 2020 Mkuu wa Wilaya hiyo Emmanuel Luhahula amesema kuwa Ibrahimu Nkumbi ambaye ni Afisa Ugavi na Manunuzi wa Halmashauri hiyo ametumia utaalamu wake vibaya kumdanganya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Linno Mwageni kwa kutoa nyaraka ambazo zinaonesha kuwa vifaa vya ujenzi vimekwisha pokelewa na Halmashauri hiyo wakati mpaka leo hakuna vifaa vyovyote vilivyonunuliwa na kupokelewa.
“ Kuanzia sasa ninakuagiza Mkurugenzi Mtendaji kumsimamisha kazi Afisa huyo, huku akiiagiza Ofisi ya kuzuwia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) kuchunguza tuhuma za ubadhilifu wa fedha hizo,” ameagiza Luhahula
Mkuu huyo wa Wilaya amesema katika tuhuma hiyo jumla ya shilingi milioni 34,984,500 ilisemekana kuwa zilitumika kununua saruji mifuko 600 na bati 877.
Luhahula alipata tetesi za ubadhirifu wa fedha hizo ambapo ilimlazimu kuunda Timu ya Watu Watano ili kuchunguza ubadhirifu huo na kubainika kuwa fedha hizo zimelipwa kwa mzabuni Kiteka General Supply ambayo inamilikiwa na Wifredi Kizanga Diwani wa Kata ya Tulya.
“ Kikao cha kamati ya Mfuko wa Jimbo kilicho keti Desemba 19 mwaka jana kiliazimia kuwa vifaa vilivyoagizwa visigawiwe popote hadi pale kamati itakapotembelea maeneo yenye uhitaji. Hata hivyo Januari 20 mwaka huu Halmashauri ilifanya malipo ya shilingi 34, 196,610 kupitia hati ya malipo ya Januari 07, 2020 kwa mzabuni Kiteka General Supply kinyume na sheria ya manunuzi namba 7 ya mwaka 2016, na sheria hii inakataza taasisi kufanya biashara na mtumishi au kiongozi wake kwa kukwepa mgongano wa kimaslahi,”
“ Uchunguzi unathibitisha kuwa Afisa Manunuzi na Ugavi Ibrahimu Nkumbi ametumia utaalamu wake vibaya kwa kumpotosha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya kwa kutofuata sheria za manunuzi wakati wa mchakato wa manunuzi ya vifaa vya mfuko wa Jimbo. Aidha kwa kutumia utaalamu wake alimdanganya Mkurugenzi Mtendaji kuwa vifaa vilivyonunuliwa vimeishafika Halmashauri, kwa taarifa hiyo ilimlazimu Mkurugenzi Mtendaji kuunda kamati ya Watu Watatu ili wakakague vifaa hivyo vilivyonunuliwa, hata hivyo kamati hiyo haikukagua stoo ya Halmashauri na badala yake ilikagua stoo ya mzabuni Wilfred Kizanga na kuandika taarifa kuwa vifaa vimenunuliwa kama ilivyoagizwa,” amebainisha Luhahula
Aidha timu hiyo ya Watu Watano ilioteuliwa na Mkuu huyo wa Wilaya ilabaini kuwa sheria ya manunuzi ya umma, kanuni za kudumu za utumishi wa umma, na muwongozo wa mfuko wa jimbo zimekiukwa kwa maksudi kwa lengo la kufanyia biashara fedha za serikali zilizo tolewa kwa ajili ya maendeleo ya Jimbo.
Katika uchunguzi huo timu hiyo imetoa mapendekezo kuwa watuhumiwa waliohusika na ubadhilifu huo wachukuliwe hatua za kinidhamu na Muajiri wao.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya ameagiza vyombo vinavyohusika kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini kama kuna jinai iliyoisababishia serikali hasara ya fedha baada ya serikali kulipwa kwa mfanya biashara ambaye hajakabidhi vifaa hadi sasa licha ya wataalamu wa Idara ya Manunuzi na Mipango kuonesha kuwa vifaa hivyo vimekwisha pokelewa na Halmashauri hiyo.
Pia ameiagiza Idara ya Elimu kuhakikisha inalipa madai ya Walimu ifikapo februari 28, 2020.
“ Ninaiagiza Idara ya Elimu mpaka kufikia kesho iwe imelipa madai ya Walimu na wasipowalipa nitawashughulikia,” amesisitiza Luhahula
Hata hivyo ametoa maelekezo kuwa vituo vya Afya Ndago na Kinampanda vianze kufanya kazi mara moja.
Akihitimisha maongezi yake na Waandishi wa Habari, Luhahula amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutimiza ahadi aliowaahidi wananchi wa shelui Desemba 2019 kuwapa 250 milioni kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya Shelui.
Mkuu wa wilaya amethibitisha kuwa Rais Dkt, John Pombe Magufuli amekwisha leta 400 milioni tangu Januari mwaka huu, huku akimshauri Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kuharakisha ujenmzi wa kituo hicho kwa kutumia Suma JKT au Magereza.
Mwisho
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.