Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula amewaomba Watumishi wa Mungu na Watumishi wa umma kuifanyia kazi elimu walioipata katika kikao cha mpango mkakati wa magonjwa yaliokuwa hayapewi kipaumbele katika ukumbi wa Mkuu wa Wilaya ya Iramba.
Luhahula ametoa ombi hilo leo Ijumaa Machi 6, 2020 wakati akifungua kikao hicho kwa ajili ya mafunzo mafupi ya ugonjwa wa minyoo na madhara yake kwa jamii katika Ukumbi wa Mkuu wa Wilaya mjini kiomboi.
Mkuu huyo wa Wilaya amewaomba Watumishi wa Mungu kuendelea kuiombea Iramba na Taifa zidi ya Ugonjwa ambao unaendelea kutawala.
“ Niwaombe Watumishi wa Mungu kuendelea kutuombea sisi na Taifa kwa sababu ya ugonjwa ambao unaendelea kutawala,” ameomba Luhahula
Akisoma taarifa fupi ya utekelezaji wa unyweshaji wa dawa ya minyoo tumbo na kichocho inayotekelezwa na Mpango wa Taifa wa magonjwa yaliokuwa hayapewi kipaumbele, Grace Kiunsi amesema wamepanga kufikia asilimia 100% ya walengwa walioko shuleni.
Amesema kitengo cha magonjwa yaliokuwa hayapewi kipaumbele chini ya CHMT ya Halmashauri hiyo itaendelea kutekeleza zoezi la utoaji wa kinga tiba kwa watoto wenye umri wa kwenda shule kwa kuzingatia maelekezo ya Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto.
Zoezi la utoaji wa kinga tiba litafanyika mach 16 hadi 17, 2020 kwa kugawa dawa ya aina moja ya minyoo tumbo kwa walengwa 66,186 wenye umri wa miaka 5 hadi 15.
Idadi hiyo imeongezeka ukilinganisha na mwaka jana ambapo jumla ya walengwa 57,746 walipatiwa kinga tiba ya minyoo ya tumbo na kichocho huku wasichana wakiwa 32,037, wavulana 32,137 na watoto wenye umri wa kwenda shule ambao hawapo shuleni 386.
Naye Mratibu wa magonjwa yaliokuwa hayapewi kipaumbele wa Halmashauri hiyo, Dkt. Msengi Ntanagala amesema kuwa dawa hiyo inatibu minyoo ya mviringo, minyoo ya mjeledi na minyoo ya safura ambayo uambukizwa kwa kula mayai ya minyoo hiyo kutoka kwenye udongo au kupenya kwenye ngozi.
Pia amebainisha baadhi ya madhara yatokanayo na minyoo hiyo kwenye haja kubwa, kwenye ini, kwenye utumbo na kwenye ubongo.
Akijibu swali lililoulizwa na mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Dkt Ntanagala amesema kuwa wanaolengwa ni watoto kwa sababu athari ya maambukizo ni kubwa mno kutokana na tabia zao za kuchezea udongo, mchanga na ulaji wa matunda bila kuyasafisha.
Kwa upande wake mchungaji wa kanisa la Evangelist Assembles of God la mjini hapo, Robert Kijanga amewaomba Wataalamu kufika katika nyumba za ibada ili kutoa elimu hiyo.
“Sisi watu wa dini tunawakaribisha katika nyumba zetu za ibada kuongea na jamii ili kufikisha elimu hii,” ameomba Kijanga
Katika mafunzo hayo, viongozi wa dini mbalimbali walitumia fursa ya kuiombea Wilaya ya Iramba na Taifa kwa ujumla kuepukana na ugonjwa unaoendelea kuenea kwa sasa duniani pamoja na janga la nzige.
MWISHO
Grace Kiunsi akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa unyweshaji wa dawa ya minyoo tumbo na kichocho mbele ya wajumbe wa kikao cha mpango mkakati wa magonjwa yalikuwa hayapewi kipaumbele. Picha na Hemedi Munga
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula akisikiliza taarifa ya utekelezaji wa unyweshaji wa dawa ya minyoo tumbo na kichocho mbele ya wajumbe wa kikao cha mpango mkakati wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele. Kushoto kwake ni katibu tawala wa wilaya hiyo, Pius Songoma na kulia mwa Mkuu huyo wa Wilaya ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri hiyo, Emmanuel Makwaya. Picha na Hemedi Munga
Mchungaji wa kanisa la Evangelist Assembles of God, Robert Kijanga akichangia mada baada ya taarifa ya utekelezaji wa unyweshaji wa dawa ya minyoo tumbo na kichocho mbele ya wajumbe wa kikao cha mpango mkakati wa magonjwa yalikuwa hayapewi kipaumbele. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.